The chat will start when you send the first message.
1Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara?
2Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa maneno halisi ya Mungu.
3Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu?
4La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa:
“Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena,
na ukashinde unapotoa hukumu.”
5Lakini ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.)
6La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angewezaje kuhukumu ulimwengu?
7Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?”
8Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja”? Wao wanastahili hukumu yao.
9Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi.
10Kama ilivyoandikwa:
“Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.
11Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,
hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.
12Wote wamepotoka,
wote wameoza pamoja;
hakuna atendaye mema,
naam, hakuna hata mmoja.”
13“Makoo yao ni makaburi wazi;
kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.”
“Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”
14“Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”[#3:14 Za 10:7]
15“Miguu yao ina haraka kumwaga damu;
16maangamizi na taabu viko katika njia zao,
17wala njia ya amani hawaijui.”[#3:17 Isa 59:7, 8]
18“Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”[#3:18 Za 36:1]
19Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu.
20Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.
21Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia.
22Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti,
23kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu,
24wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Kristo Yesu.
25Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa.
26Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.
27Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La, bali kwa ile sheria ya imani.
28Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kupitia kwa imani wala si kwa matendo ya sheria.
29Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia.
30Basi kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani hiyo hiyo.
31Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.