Zekaria 13

Zekaria 13

Kutakaswa dhambi

1“Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi.

2“Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Bwana wa majeshi. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi.

3Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana .’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.

4“Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu.

5Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’

6Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’

Mchungaji apigwa, nao kondoo watawanyika

7“Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu,

dhidi ya mtu aliye karibu nami!”

asema Bwana wa majeshi.

“Mpige mchungaji,

nao kondoo watatawanyika,

nami nitageuza mkono wangu

dhidi ya walio wadogo,

8katika nchi yote,” asema Bwana ,

“theluthi mbili watapigwa na kuangamia;

hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake.

9Hii theluthi moja nitaileta katika moto;

nitawasafisha kama fedha isafishwavyo

na kuwajaribu kama dhahabu.

Wataliitia Jina langu

nami nitawajibu;

nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’

nao watasema, ‘Bwana ni Mungu wetu.’ ”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.