Zekaria 9

Zekaria 9

Hukumu juu ya adui za Israeli

1Neno la unabii:

Neno la Bwana liko kinyume na nchi ya Hadraki

na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika,

kwa kuwa macho ya watu na ya makabila yote ya Israeli

yako kwa Bwana ;

2pia juu ya Hamathi inayopakana nayo,

juu ya Tiro na Sidoni,

ingawa wana ujuzi mwingi sana.

3Tiro amejijengea ngome imara,

amelundika fedha kama mavumbi,

na dhahabu kama taka za mitaani.

4Lakini Bwana atamwondolea mali yake

na kuuangamiza uwezo wake wa baharini,

naye atateketezwa kwa moto.

5Ashkeloni ataona hili na kuogopa;

Gaza atagaagaa kwa maumivu makali,

pia Ekroni, kwa sababu

matumaini yake yatanyauka.

Gaza atampoteza mfalme wake

na Ashkeloni ataachwa pweke.

6Wageni watakalia mji wa Ashdodi,

nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.

7Nitaondoa damu vinywani mwao,

chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao.

Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu,

nao watakuwa viongozi katika Yuda,

naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.

8Lakini nitailinda nyumba yangu

dhidi ya majeshi ya wanyangʼanyi.

Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena,

kwa maana sasa ninawachunga.

Kuja kwa Mfalme wa Sayuni

9Shangilia sana, ee Binti Sayuni!

Piga kelele, Binti Yerusalemu!

Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,

ni mwenye haki, naye ana wokovu,

ni mpole, naye amepanda punda,

mwana-punda, mtoto wa punda.

10Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu

na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,

nao upinde wa vita utavunjwa.

Atatangaza amani kwa mataifa.

Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,

na kutoka Mto hadi mwisho wa dunia.

11Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya agano langu nawe,

nitawaacha huru wafungwa wako

watoke kwenye shimo lisilo na maji.

12Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini;

hata sasa ninatangaza kwamba

nitawarejesheeni maradufu.

13Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu,

nitamfanya Efraimu mshale wangu.

Nitawainua wana wako, ee Sayuni,

dhidi ya wana wako, ee Uyunani,

na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.

Bwana atatokea

14Kisha Bwana atawatokea;

mshale wake utamulika kama radi.

Bwana Mwenyezi atapiga tarumbeta,

naye atatembea katika tufani za kusini,

15na Bwana wa majeshi atawalinda.

Wataangamiza na kushinda

kwa mawe ya kutupa kwa kombeo.

Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo;

watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia

kwenye pembe za madhabahu.

16Bwana Mungu wao atawaokoa siku hiyo

kama kundi la watu wake.

Watangʼara katika nchi yake

kama vito vya thamani kwenye taji.

17Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri!

Nafaka itawastawisha vijana wanaume,

nayo divai mpya vijana wanawake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.