Zaburi 72

Zaburi 72

Sala ya kumtakia mfalme neema

1Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,

Na mwana wa mfalme haki yako.

2Atawaamua watu wako kwa haki,[#Isa 11:2]

Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

3Milima na iwaletee watu amani,

Na pamoja na vilima, vilete haki.

4Na atawatetea watu walioonewa,

Awaokoe wahitaji, na kumwaangamiza mdhalimu.

5Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua,

Na wakati wa kung'aa mwezi kizazi hata kizazi.

6Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa,[#2 Sam 23:4; Hos 6:3]

Kama manyunyu yainyweshayo nchi.

7Haki na isitawi wakati wa maisha yake yote,[#Isa 2:4; Dan 2:44; Lk 1:33]

Nayo amani iwepo, hadi mwezi utakapokoma.

8Na awe na enzi toka bahari hadi bahari,[#Kut 23:31; 1 Fal 4:21,24; Zab 2:8; Zek 9:10]

Toka Mto hadi miisho ya dunia.

9Wakaao jangwani na wainame mbele zake;

Adui zake na warambe mavumbi.

10Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi;[#Isa 49:7]

Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.

11Naam, wafalme wote na wamsujudie;

Na mataifa yote wamtumikie.

12Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo,

Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.

13Atawahurumia wanyonge na maskini,

Na nafsi za wahitaji ataziokoa.

14Atawakomboa kutoka kwa maonevu na udhalimu,

Maana damu yao ina thamani machoni pake.

15Na aishi maisha marefu![#Mt 6:10; 1 Kor 1:2,3]

Na wampe dhahabu ya Sheba;

Na wamwombee daima;

Na kumbariki mchana kutwa.

16Na uwepo wingi wa nafaka[#1 Fal 4:20]

Katika ardhi juu ya milima;

Matunda yake na yawayewaye kama ilivyo katika milima ya Lebanoni,

Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.

17Jina lake na lidumu milele,[#Mwa 12:3; Yer 4:2; Isa 45:23,24; Lk 1:48; Flp 2:9-11]

Pindi ling'aapo jua, umaarufu wake uwepo;

Mataifa yote na wabarikiwe katika yeye,

Na kumwita heri.

* * *

18Na ahimidiwe BWANA, Mungu, Mungu wa Israeli,

Atendaye miujiza Yeye peke yake;

19Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;

Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.

* * *

20Maombi ya Daudi mwana wa Yese, yamekwisha.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania