Yoshua Mwana wa Sira 33

Yoshua Mwana wa Sira 33

1Uovu haumpati yeye amchaye BWANA;

Mara kwa mara atamwokoa majaribuni;

2Aichukiaye torati hapati hekima;

Mnafiki hutikisika kama dau dhorubani.

3Mwenye ufahamu hutambua neno la BWANA;[#Kut 28:30; Sira 45:10]

Torati ni amini kama kuuliza kwa Urimu.

4Ujiweke tayari kusema, nawe utasikiwa;

Uyafunge maarifa, nawe utafanya kujibu.

5Moyo wa mpumbavu ni kama gurudumu,

Na mawazo yake huzunguka zunguka.

6Farasi dume ni kama rafiki akuchekaye,

Hulia chini ya mtu yeyote ampandaye.

Tofauti kati ya ulimwengu na mtu

7Ya nini siku moja kupita nyingine;

Nuru ya kila siku ya mwaka si ya jua?

8Kwa maarifa ya BWANA zimepambanuka.

Naye amebadili majira na sikukuu;

9Nyingine amezikuza na kuziweka wakfu,

Na nyingine amezifanya siku za kawaida.

10Hivyo watu wote wametoka katika ardhi,

Naye Adamu aliumbwa katika udongo;

11Kwa hekima yake BWANA amewapambanua.

Na kufanya njia zao kuwa mbalimbali.

12Wengine amewabariki na kuwatukuza,

Wengine amewaweka wakfu karibu naye;

Wengine amewalaani na kuwaangamiza.

Na kuwaangusha katika mahali pao.

13Kama udongo mkononi mwa mfinyanzi,

Wote wamo mkononi mwake aliyewaumba;

Njia zake ni sawasawa na mapenzi yake,

Kuwaamuru kwa kadiri ya hukumu zake;

14Wema juu ya uovu na uzima juu ya mauti,

Hivyo na mwenye haki juu ya mkosaji.

15Basi, uyafikiri hivyo

Matendo yake Aliye Juu;

Hayo ni mawili mawili,

Hili juu ya hili.

16Mimi niliamka siku hizi za mwisho, mithili ya mtu mwenye kuokota masazo nyuma ya wavuna zabibu;

17lakini kwa baraka ya BWANA nimeendelea, na kulijaza shinikizo langu sawasawa kama mvunaji.

18Fikirini ya kwamba sikufanya kazi kwa ajili yangu tu, ila kwa ajili ya wote waitafutao elimu.

19Enyi wakuu wa watu, mnisikilize; nanyi mtawalao kusanyiko mnitegee masikio yenu.

Faida ya kujitegemea

20Usimpe mwana nguvu juu yako wakati unapoishi, wala mke wako, wala ndugu, wala rafiki; nawe ukiwa bado hai, unavuta pumzi. Wala usimtolee mwingine mali zako, usije ukajuta na kuziomba tena.

21Usijitie katika uwezo wa mtu yeyote.

22Ni afadhali watoto wako wakuombe wewe, kuliko wewe kuutazamia mkono wa wanao.

23Katika matendo yako yote ukae unayo mamlaka, wala usitie ila heshima yako.

24Lakini siku ile utakapozikomesha siku za maisha yako, na hapo ujapo kufariki; utoe usia na kuugawa urithi wako.

Jinsi ya kutendea watumwa

25Malisho, fimbo na mizigo,

Kwa punda;

Chakula, mapigo na kazi,

Kwa mtumwa.

26Mpe mtumwa wako kazi, nawe utastarehe; ukimwacha hana kazi, atatafuta uhuru wake.

27Kongwa na vifungo huinamisha shingo, na kwa mtumwa mwovu kuna kushtusha viungo na adhabu kali.

28Lakini umpeleke kazini asiwe mvivu madhali uvivu hufundisha fujo tele.

29Umpe kazi itakayomjuzu, asipotii umfanyie nzito pingu zake.

30Lakini usipite kiasi kwa mtu yeyote, wala usifanye neno pasipo hukumu.

31Iwapo unaye mtumwa mmoja tu, na awe kama nafsi yako; mradi ni hasara yako ukipotewa naye.

32Iwapo unaye mtumwa mmoja tu, umtendee kama ndugu; maana usimtende mabaya aliye damu yako.

33Nawe ukimtenda mabaya akakutoroka, je! Utafuata njia ipi ili kumtafuta?

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania