1 Wamakabayo 13

1 Wamakabayo 13

Simoni awaongoza Wayahudi

1Simoni alisikia kwamba Trifo alikuwa amekusanya jeshi kubwa, kuivamia nchi ya Yudea na kuiangamiza.

2Aliona pia kwamba watu walikuwa wanatetemeka kwa hofu. Basi, akaenda Yerusalemu, akaitisha mkutano,

3na kujaribu kuwatia watu moyo, akisema: “Mnajua mambo makuu ambayo mimi na ndugu zangu na jamaa yote ya baba yangu tumeyafanya kwa ajili ya sheria na hekalu. Hali kadhalika, mnajua kuhusu vita tulivyoendesha, na mateso tuliyoyapata.

4Ndugu zangu wote wameuawa katika kupigania sheria, hekalu na taifa la Israeli; mimi peke yangu nimesalia.

5Na sasa, hakika sitajaribu kuokoa maisha yangu wakati wowote wa hatari, maana mimi sijioni kuwa bora kuliko hao ndugu zangu.

6Nitalipiza kisasi kwa ajili ya taifa langu, hekalu, wake zenu na watoto wenu, maana mataifa yote yamekusanyika kwa chuki kutuangamiza.”

7Maneno hayo yaliwatia watu moyo sana,

8nao wakajibu kwa sauti kubwa: “Wewe sasa ni kiongozi wetu mahali pa ndugu zako Yuda na Yonathani.

9Endeleza mapambano yetu, nasi tutafanya lolote utakalotuambia.”

10Basi, Simoni akawakusanya askari wote akafanya haraka kumalizia kuta za Yerusalemu na kuimarisha ulinzi wake.

11Akamtuma Yonathani mwana wa Absalomu kwenda Yopa, pamoja na jeshi kubwa. Yonathani akawafukuzia mbali watu waliokuwa Yopa, akaumiliki mji.

12Trifo akaondoka Tolemai na jeshi kubwa kwenda kuivamia Yudea. Alikuwa amemchukua Yonathani, nduguye Simoni, kama mfungwa.

13Simoni alikuwa amepiga kambi Adida, kuelekea kwenye tambarare.

14Trifo aliposikia kwamba Simoni alikuwa ameshika mahali pa nduguye Yonathani, na kwamba alikuwa amejitayarisha kupigana naye vita, akampelekea ujumbe ufuatao:

15“Nimemweka ndugu yako Yonathani chini ya ulinzi kwa sababu wakati wa utawala wake hakulipa madeni yake katika hazina ya mfalme.

16Sasa nipelekee fedha kilo 3,000, na wanawe wawili wawe mateka, ili tutakapomwachilia asije akatufanyia mapinduzi. Hapo tutamwachilia.”

17Ingawa Simoni alijua kwamba walikuwa wanamdanganya, akaagiza aletewe fedha na wana wawili wa Yonathani, kwa sababu hakutaka kuzua uadui miongoni mwa Wayahudi,

18ambao wangesema baadaye: “Kama Simoni angempa fedha na wale wanawe, Yonathani hangeliuawa.”

19Basi, Simoni akafanya kama Trifo alivyokuwa amedai, lakini Trifo alivunja ahadi yake akaendelea kumshikilia Yonathani.

20Halafu Trifo akachukua hatua ya kuivamia na kuiteketeza nchi ya Yudea. Aliizunguka Yudea kwa kupitia njia ya kwenda Adora. Lakini Simoni na jeshi lake walifuatana naye sambamba kila alikoenda.

21Wakati huo wote askari maadui waliokuwa katika ngome ya Yerusalemu walikuwa wanawatuma wajumbe kwa Trifo kumhimiza aje kwao haraka kwa njia ya jangwani, na awaletee chakula.

22Hivi, Trifo aliwaandaa wapandafarasi wake wote kwa ajili ya safari, lakini usiku ule pakawa na theluji nyingi sana, akashindwa kupanda milimani. Basi, akavunja safari hiyo, akaenda zake nchini Gileadi.

23Alipokaribia Baskama, aliamuru Yonathani auawe; Yonathani akazikwa hapo.

24Halafu Trifo akarejea nchini kwake.

25Simoni akawatuma watu kwenda kuuchukua mwili wa Yonathani, akamzika nduguye huko Modeini, mji wa babu zake.

26Kila mmoja katika Israeli alimlilia kwa uchungu mkali na kumwombolezea kwa muda mrefu.

27Simoni akajenga mnara wa ukumbusho juu ya kaburi la baba yake na ndugu zake. Mnara huo ulifunikwa mbele na nyuma kwa jiwe lililokuwa limesuguliwa vizuri, na uliweza kuonekana kutoka mbali.

28Pia alijenga piramidi saba, huku na huku, kwa ajili ya baba yake, mama yake, na nduguze wanne.

29Kuzunguka piramidi hizo alitengeneza mitambo ya kusimamishia nguzo ndefundefu. Juu ya nguzo hizo aliweka silaha za aina mbalimbali, ziwe kumbukumbu ya kudumu. Kando ya silaha hizo aliweka meli za kuchongwa. Wote waliosafiri baharini waliweza kuona kumbukumbu hizo.

30Kaburi alilojenga Simoni kule Modeini lingali huko mpaka leo.

31Trifo alimtendea vibaya yule mfalme chipukizi, Antioko wa Sita, akamuua,

32na kutawala mahali pake na hivyo akawa mfalme wa Asia. Mfalme Trifo alisababisha matatizo makubwa nchini humo.

33Simoni alizijenga upya ngome za Yudea, akizizungushia kuta imara zenye minara mirefu, na milango na mapingo. Halafu akaweka akiba ya chakula ngomeni.

34Aliwatuma wajumbe kwa mfalme Demetrio wa Pili kuomba nchi yake isamehewe kodi, kwa vile Trifo alikuwa anazidi kuwanyonya.

35Demetrio akajibu kwa barua ifuatayo:

36“Mfalme Demetrio kwa kuhani mkuu Simoni, rafiki ya wafalme, kwa taifa la Wayahudi na viongozi wake: Salamu!

37Nimepokea taji ya dhahabu na tawi la mtende mlivyoniletea, nami nipo tayari kufanya nanyi mkataba wa amani, na kuwaelekeza makarani wetu wa kodi kuwasamehe nyinyi kodi.

38Makubaliano yetu ya awali yamethibitishwa, na ngome mlizojenga zitabaki mali yenu.

39Ninawapeni msamaha kwa makosa ya ukiukaji wa mkataba yaliyofanyika hadi tarehe ya leo, na ninawasamehe malipo mnayodaiwa bado ya kodi maalumu na kodi nyingine zozote zilizokuwa zinakusanywa mpaka sasa huko Yerusalemu.

40Wayahudi wote wenye sifa zinazotakiwa kwa utumishi wa mfalme wanaweza kuandikishwa. Na iweko amani kati yetu.”

41Mnamo mwaka 170 nira ya ukandamizaji ya mataifa mengine iliondolewa kwa Wayahudi.[#13:41 Ni sawa na 142 K.K.]

42Watu wakawa wanaanza kuandika taarifa zao na mikataba yao kwa maneno haya: “Katika mwaka wa kwanza wa Simoni, kuhani mkuu mkubwa, kamanda na kiongozi wa Wayahudi.”

43Siku hizo Simoni alipiga kambi dhidi ya Gazara, akauzunguka mji na jeshi lake. Aliunda mtambo wa vita, akausogeza mpaka kwenye ukuta wa mji. Halafu akaushambulia mnara mmojawapo, akauteka.

44Watu waliokuwa katika huo mtambo wa vita wakaruka mara na kuingia mjini, ghasia kubwa ikazuka Gazara.

45Wanaume, wake zao, na watoto wao wakararua mavazi yao na kupanda juu ya ukuta wa mji. Kwa sauti kubwa wakamsihi Simoni pawe na amani,

46wakisema: “Utuhurumie! Usituadhibu kama tunavyostahili!”

47Basi, Simoni akaafikiana nao na kukomesha mapigano. Lakini akawatoa wenyeji wote mjini. Halafu akazitakasa nyumba zao zilizokuwa na sanamu za miungu. Kisha, Simoni na watu wake wakaingia mjini wakiimba tenzi na nyimbo za sifa.

48Akaondolea mbali chochote kile kilichoweza kuutia mji unajisi, akawaruhusu kukaa mjini watu wale tu waliozingatia sheria. Vilevile aliimarisha ulinzi wa mji na kujijengea nyumba yake hapo Gazara.

49Watu waliokuwa katika ngome ya Yerusalemu sasa walikuwa wamezuiwa kuondoka kwenda kununua au kuuza chochote. Njaa kali ilikuwa imewakaba, na wengi wao walikufa njaa.

50Kisha walimwomba Simoni pawe na amani. Simoni akakubali, akawatoa ngomeni, na kuitakasa ngome hiyo.

51Siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa pili, mwaka171, ilifanyika sherehe kubwa mjini Yerusalemu kwa sababu lile tishio kubwa kwa usalama wa Israeli lilikuwa limeondolewa. Simoni na watu wake waliingia ngomeni huku wanapiga vinubi, matari na zeze, na kuimba tenzi za sifa na shukrani, huku wamechukua matawi ya mitende.[#13:51 Ni sawa na 141 K.K.]

52Simoni akatoa agizo kwamba siku hiyo iadhimishwe kwa furaha kila mwaka. Aliimarisha ulinzi wa mlima wa hekalu, upande unaotazamana na ngome, akaufanya mji wa Yerusalemu makao yake na ya watu wake.

53Yohane, mwanawe Simoni, alikuwa mtu mzima sasa. Hivi Simoni akamfanya kamanda wa jeshi lake lote, naye Yohane akaamua kukaa Gazara.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania