1 Wamakabayo 3

1 Wamakabayo 3

Ushindi wa awali wa Yuda

1Yuda Makabayo akachukua nafasi ya baba yake, Matathia, akawa kamanda wa jeshi.

2Ndugu zake wote na wafuasi amini wa baba yake wakamuunga mkono, wakawa tayari kuendeleza vita vya Israeli.

3Yuda aliongeza utukufu wa watu wake.

Kama shujaa alijivika deraya yake,

akachukua silaha na kwenda vitani;

kwa upanga wake alilinda kambi yake.

4Alikuwa kama simba kwa matendo yake,

kama mwanasimba angurumaye mawindoni.

5Aliwasaka na kuwafuatia waliovunja sheria;

akawachoma moto waliowanyanyasa watu wake.

6Wavunja sheria walikufa moyo kwa kumwogopa Yuda;

waovu wote walifadhaika na kuchanganyikiwa;

kwa matendo yake alipigania na kufanikisha uhuru.

7Aliwakasirisha wafalme wengi,

lakini kwa matendo yake aliwafurahisha watu wa Yakobo;

kwa hayo atatukuzwa milele.

8Alikwenda huko na huko katika miji ya Yudea,

akiwafutilia mbali wote wasiomcha Mungu;

akaiepusha Israeli na hasira ya Mungu.

9Sifa zake zilienea hata miisho ya dunia,

aliwakusanya pamoja wale waliokuwa wanaangamia.

10Lakini Apolonio akakusanya jeshi la watu wa mataifa mengine, miongoni mwao kikiwa kikosi kikubwa kutoka Samaria, ili kuishambulia Israeli.

11Yuda alipopata habari, akatoka kukabiliana na jeshi hilo; akalishinda na kumwua Apolonio. Maadui wengi walijeruhiwa na kuuawa, na baadhi wakakimbia.

12Katika nyara zilizotekwa, Yuda alijichukulia upanga wa Apolonio, ambao aliutumia vitani siku zote za maisha yake.

13Seroni, kamanda wa majeshi ya Siria, alipata habari kwamba Yuda alikuwa amekusanya jeshi lenye askari waaminifu, waliokuwa tayari kupiga vita chini ya uongozi wake.

14Basi, Seroni akasema moyoni mwake, “Nitajipatia jina na heshima katika ufalme huu kwa kumpiga vita na kumshinda Yuda na watu wake, ambao wanaidharau amri ya mfalme.”

15Ndipo tena jeshi lenye nguvu la watu wasiomcha Mungu likaenda pamoja naye kumsaidia kulipiza kisasi kwa Waisraeli.

16Seroni alipokaribia miinuko ya Beth-horoni, Yuda akamkabili akiwa na kikosi kidogo.

17Lakini watu wa Yuda walipoona jeshi la maadui linawajia, wakamwambia Yuda: “Kitawezaje kikosi chetu kidogo kupigana na jeshi kubwa kama hilo? Isitoshe, kutwa nzima hatujala chochote, na tupo hoi!”

18Yuda alijibu, “Si vigumu, kwa kikosi kidogo kulishinda jeshi kubwa. Kwa Mungu hakuna tofauti kwamba tunaokolewa na watu wengi au wachache tu.

19Ushindi katika vita hautegemei nani ana jeshi kubwa zaidi, ila uwezo wa ushindi watoka mbinguni.

20Adui zetu wanatujia kwa vitisho na mabavu, wakipania kupora mali zetu na kuwaua wake zetu na watoto wetu.

21Lakini sisi tunapigania uhai wetu na sheria zetu.

22Bwana mwenyewe atawamaliza maadui zetu. Kwa hiyo nyinyi, msiwaogope hao.”

23Mara tu alipomaliza kusema hayo, Yuda na watu wake wakafanya shambulio la ghafla dhidi ya Seroni na jeshi lake, wakawaponda.

24Waliwafuatia katika miteremko ya Beth-horoni hadi kwenye tambarare. Huko wakawaua watu 800, na wengine wakakimbilia nchi ya Filistia.

25Baada ya hapo, watu wa mataifa mengine, kila mahali, walianza kumwogopa Yuda na nduguze.

26Sifa za Yuda zikamfikia mfalme Antioko, na watu wa mataifa waliongea juu ya Yuda na ushindi wake.

Mfalme amteua Lisia kuwa mkuu wa mkoa

27Mfalme Antioko alipopata taarifa hizo, alikasirika sana. Aliamuru majeshi yote ya milki yake yakusanyike na kuunda kikosi kikubwa.

28Alichota fedha kutoka hazina yake, akawalipa askari wake mshahara wa mwaka mzima na kuwaamuru wajiweke tayari kwa dharura yoyote ile.

29Lakini akagundua kwamba hazina yake ilikuwa haina tena akiba ya fedha. Mapato ya kodi yalikuwa yameshuka kwa sababu ya fujo na ghasia alizokuwa amesababisha ulimwenguni kwa kuondolea mbali sheria zilizokuwa zikishikwa tangu zama za zama.

30Aliingiwa na wasiwasi kwamba angeshindwa kulipia gharama za uendeshaji wa utawala wake, na asingeweza kutoatoa zawadi kama awali - kwani alikuwa mkarimu zaidi wa kutoa zawadi kuliko wafalme waliomtangulia.

31Alifadhaika sana. Hatimaye akaamua kwenda Persia kukusanya kodi kutoka mikoani na kujipatia fungu kubwa la fedha.

32Alimteua Lisia, mtu mashuhuri wa ukoo wa mfalme, awe mwakilishi wa mfalme katika eneo lote kati ya mto Eufrate na mpaka wa Misri.

33Pia alimweka awe mlinzi wa mwanawe, Antioko wa Tano, mpaka atakaporudi mwenyewe.

34Alimweka Lisia awe mwangalizi wa tembo wote na msimamizi wa nusu ya jeshi lake, kisha akampa maelezo kinaganaga kuhusu mambo aliyotaka yafanyike, na hasa, aliyotaka wafanyiwe wakazi wa Yudea na Yerusalemu.

35Lisia aliamuriwa apeleke jeshi kuwashambulia Wayahudi, hasa Wayahudi wa Yerusalemu, ili kuvunjilia mbali nguvu zao na kuwaangamiza na kuwafutilia mbali duniani.

36Aliamuriwa awanyang'anye ardhi yao na kuwapa wageni, ambao wangefanya makazi yao katika eneo lote.

37Kisha, mfalme akaondoka Antiokia, mji wake mkuu, na nusu ya jeshi lake, mwaka 147. Alivuka mto Eufrate, akapitia katika mikoa ya nyanda za juu.[#3:37 Ni sawa na 165 K.K.]

Ushindi wa Yuda

(2 Mak 8:8-29,34-36)

38Lisia aliwachagua Tolemai mwana wa Dorimene, Nikanori na Gorgia, watu hodari miongoni mwa rafiki za mfalme,

39akawatuma waende wakaiangamize nchi ya Yudea, kwa mujibu wa amri ya mfalme. Aliwapa makamanda hao askari wa miguu 40,000, na wapandafarasi 7,000.

40Basi, wakaondoka na jeshi lao lote, wakapiga kambi karibu na Emau, kwenye tambarare.

41Wafanyabiashara wa sehemu hizo, wakiwa wamevutiwa na habari walizosikia juu ya jeshi hilo, wakachukua fedha na dhahabu nyingi na minyororo, wakaenda kambini kuwachukua Waisraeli wawe watumwa wao. Na vikosi vya askari kutoka Siria na Filistia vilijiunga na jeshi hilo.

42Yuda na nduguze waliona kwamba hali yao ilikuwa inazidi kuwa ngumu. Majeshi ya adui yalikuwa yameweka kambi katika nchi yao. Na mfalme alikuwa ameamuru wao waangamizwe kabisa.

43Lakini, wakaambiana, “Na tulijenge upya taifa letu! Tupigane kwa ajili ya watu wetu na madhabahu yetu!”

44Ndipo jumuiya nzima ikakusanyika kujiandaa kwa ajili ya vita, na kuomba msamaha na huruma kwa Mungu.

45Yerusalemu ulikuwa tupu kama jangwa;

hapana mkazi wake aliyetoka wala kuingia mjini.

Hekalu lilitiwa unajisi na wageni;

watu wageni walishika ngome ya mji,

mataifa mengine walifanya makao humo.

Furaha iliwahama watu wa Yakobo;

sauti ya filimbi na zeze haikusikika tena.

46Basi, Yuda na watu wake wakakutana na kwenda zao Mizpa, mkabala na Yerusalemu, kwa vile watu wa Israeli walikuwa na mahali pa sala hapo Mizpa siku za nyuma.

47Walifunga siku hiyo, wakavaa mavazi ya magunia, wakajitia majivu kichwani na kurarua nguo zao.

48Katika hali kama hiyo, watu wa mataifa mengine wangeagua na kuiuliza miungu yao, lakini Waisraeli walifungua kitabu cha sheria, wakatafuta mwongozo wa Mungu.

49Wakaleta mavazi ya makuhani, matoleo ya mavuno ya kwanza, na zaka. Kisha wakawaleta Wanadhiri waliokuwa wametimiza nadhiri zao.

50Ndipo jumuiya nzima ikasali kwa sauti kuu, ikisema:

“Tufanyeje na Wanadhiri hawa?

Tuwapeleke wapi sasa?

51Hekalu lako limekanyagwa kwa dharau na kutiwa unajisi,

na makuhani wako wanalia kwa unyonge.

52Na tazama, watu wa mataifa mengine wamekusanyika kutuangamiza;

nawe wazijua hizo njama zao dhidi yetu.

53Tutawezaje kukabiliana nao

kama hutupatii msaada wako?”

54Halafu wakapiga tarumbeta na kulia kwa sauti kuu.

55Baada ya hapo, Yuda akawagawa watu wake katika vikundi vya watu kumikumi, hamsinihamsini, miamia na elfuelfu. Kila kikundi alikiweka chini ya kiongozi maalumu.

56Halafu, kwa mujibu wa sheria, akawarudisha nyumbani kila mtu aliyekuwa anajenga nyumba, au amefunga ndoa siku hizo, au aliyekuwa anaotesha mizabibu, au aliyekuwa mwoga.

57Kisha, jeshi la Yuda likaondoka, likapiga kambi kusini ya Emau.

58Hapo Yuda akawaambia watu wake: “Jiandaeni kwa mapambano! Pigeni moyo konde! Mapema kesho asubuhi muwe tayari kuwapiga hawa watu wa mataifa mengine ambao wamekusanyika dhidi yetu kutuangamiza sisi na hekalu letu.

59Afadhali kwetu kufa vitani kuliko kuangalia tu kuteketezwa kwa taifa letu na hekalu letu.

60Lakini Mungu mbinguni atafanya atakavyo mwenyewe.”

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania