The chat will start when you send the first message.
1Mtu fidhuli aweza kulinganishwa na jiwe chafu;
kila mtu akimwona hufyonya kwa sababu ya aibu yake.
2Mtu fidhuli aweza kulinganishwa na marundo ya mavi;
kila mtu anayeyagusa huyakungutia mbali.
3Ni balaa kuwa baba wa mtoto asiye na nidhamu;
na kuzaliwa kwa binti asiye na nidhamu ni hasara.
4Msichana mwenye busara hupata mume,
lakini atendaye kwa aibu humhuzunisha baba yake.
5Msichana asiye na adabu atamwaibisha baba yake na mumewe,
naye atadharauliwa na wote wawili.
6Kama vile muziki katika matanga ndivyo hadithi isiyo ya wakati wake.
Kuadhibu na kupa nidhamu ni jambo la hekima daima. [
7Watoto waliolelewa vizuri hawaonyeshi hali nyonge ya kuzaliwa kwa wazazi wao.
8Watoto ambao hawalelewi vema, watovu wa adabu na wenye kiburi ni doa kwa jamaa yao.]
9Amfundishaye mpumbavu ni kama anayeunga vigae,
au anayemwamsha mtu kutoka usingizi mzito.
10Amwambiaye mpumbavu hadithi anamwambia mtu anayepepesuka;
na mwishowe huyo atasema: “Ni nini?”
11Mwombolezee aliyekufa maana hana mwanga;
na mwombolezee mpumbavu maana hana akili.
Usimwombolezee mno aliyekufa maana amepumzika;
lakini mpumbavu, maisha yake ni mabaya kuliko kifo.
12Matanga hufanywa kwa muda wa siku saba;
lakini matanga ya mpumbavu na asiyemcha Mungu hudumu maisha yake yote.
13Usiongee mno na mtu mpumbavu;
na usimtembelee mtu asiye na akili.
Mwepe ili aweze kuepa taabu;
naye atakapojikunguta wewe hutachafuka.
Mwepe nawe utapata amani,
wala hutachoshwa na kichaa chake.
14Ni kitu gani kizito kuliko risasi?
Kitu hicho jina lake ni “Pumbavu!”
15Kubeba mchanga, chumvi na chuma
ni rahisi kuliko kumvumilia mpumbavu.
16Boriti lililofungwa imara kwenye nyumba
halitangolewa kwa mtetemeko wa nchi.
Kadhalika na moyo ulioimarika katika mashauri ya busara
hautakuwa na woga wakati wa hatari.
17Moyo ulioimarishwa na mawazo ya busara
ni kama mnara imara uliotiwa nakshi.
18Mawe madogo juu ya ukuta
hayatabaki hapo upepo ukivuma.
Kadhalika na moyo wa fikira za kipumbavu;
hautaweza kustahimili matukio ya kutisha.
19Ukilijeruhi jicho machozi yatatoka;
ukiujeruhi moyo utaondoa urafiki.
20Ukiwatupia ndege jiwe utawafukuza;
na ukimkaripia rafiki utavunja urafiki.
21Hata kama umekwisha mnyoshea rafiki yako upanga
usife moyo maana inawezekana kurudisha urafiki.
22Kama umetamka kitu dhidi ya rafiki yako
usiogope maana upatanisho unawezekana.
Lakini kutukana na kuwa na kiburi,
kusema siri na kushambulia wengine ghafla,
ni vitu ambavyo hufukuza marafiki wa mtu.
23Mfanye jirani yako akuamini wakati wa umaskini wake,
ili ufurahi pamoja naye wakati atakapopata fanaka.
Msaidie wakati anapopata mateso,
ili upate sehemu yako katika mali atakayopewa.
24Moshi ni dalili ya moto,
mvuke na moshi wa tanuri hutangulia moto;
kadhalika nayo matusi ni dalili ya mauaji.
25Sitaona aibu kumlinda rafiki
wala sitajificha mbali naye.
26Lakini ikiwa nitaumia kwa sababu yake
yeyote atakayesikia habari hiyo atamwepa.
27Nani ataniwekea mlinzi mdomoni mwangu,
na kuupiga mhuri wa busara,
ili unizuie nisije nikakosa,
ulimi wangu usije ukaniangamiza!