Sira 26

Sira 26

1Heri mume aliye na mke mwema

siku za maisha yake zitaongezwa maradufu.

2Mke mwaminifu ni furaha ya mumewe;

mumewe ataishi kwa amani miaka yote.

3Mke mwema ni baraka kubwa;

baraka anayopewa mume amchaye Bwana.

4Mtu kama huyo, awe tajiri au maskini,

daima ana furaha moyoni;

na wakati wote ni mwenye uso mkunjufu.

5Moyo wangu unayaogopa mambo matatu,

na la nne linanitisha:

Uvumi mbaya mjini, genge la waovu,

na mashtaka ya uongo.

Hayo yote ni mabaya kuliko kifo.

6Lakini daima kuna masikitiko na huzuni moyoni

mke anapomwonea wivu mke mwenzake,

na ulimi wake kumshambulia kila mtu.

7Mke mwovu ni kama nira inayokwaruza shingoni;

kujaribu kumtawala ni sawa na kushika nge.

8Mke aliyelewa husababisha hasira,

hawezi kuficha aibu yake.

9Mwanamke malaya huonekana katika macho yake,

naye hujulikana kwa kope zake.

10Uwe mkali kwa binti aliye na ukaidi,

la sivyo, akipata nafasi tu, ataitumia kujiumiza mwenyewe.

11Jihadhari na macho yake yasiyo na haya,

wala usishangae akikukosea.

12Kama vile msafiri mwenye kiu afunuavyo kinywa chake

na kunywa maji yoyote ayaonayo,

ndivyo na binti huyo atakavyoketi kila mahali

na kujifunua kwa kila mwanamume apitaye hapo.

13Mke mzuri humfurahisha mumewe,

na ujuzi wake humfanya awe na nguvu.

14Mke mkimya ni zawadi kutoka kwa Bwana,

hakuna bei ya kufaa kulingana naye.

15Mke mwenye kiasi hupendeza zaidi na zaidi,

hakuna kipimo kinachoweza kumpima mke mwenye tabia nzuri.

16Kama vile pambazuko la jua katika anga la Bwana

ndivyo ulivyo uzuri wa mke mwema na nyumba yake nadhifu.

17Kama vile taa iwakavyo juu ya kinara kitakatifu,

ndivyo ulivyo uzuri wa uso wake na umbo lake.

18Na kama nguzo za dhahabu juu ya vikalio vya fedha

ndivyo ilivyo miguu yake mizuri, juu ya nyayo imara. [

19Mwanangu, hifadhi nguvu za ujana wako, wala usiwape wageni nguvu zako.

20Jitafutie nchini kote eneo lenye rutuba, ukapande humo mbegu yako mwenyewe, ukitumainia kuwa na ukoo wako bora.

21Hivyo watoto wako mwenyewe wataishi, watakuwa mashuhuri, wakiwa na matumaini ya malezi bora.

22Mwanamke malaya ni kama mate; mke mtembezi ni kama mlingoti wa kifo.

23Mwanamke asiyemcha Mungu amepangiwa mume mkosefu, lakini mwema amepangiwa mume mcha Mungu.

24Mke asiye na aibu hufurahi kujiaibisha, lakini mke mwenye kiasi ana haya hata mbele ya mumewe.

25Mwanamke mkaidi ni sawa na mbwa, lakini mwenye haya humcha Bwana.

26Mke anayemheshimu mumewe kila mtu atamwona ana hekima, lakini anayemdharau kwa majivuno wote watamwona kuwa mwovu. Heri mume aliye na mke mwema maana siku za maisha yake zitakuwa maradufu.

27Mke wa makelele, mwenye kueneza uvumi, ni kama tarumbeta ya vita; na mume aliyejifunga na mke wa namna hiyo maisha yake ni vita.]

Mambo yaletayo huzuni

28Yako mambo mawili yanayonihuzunisha moyoni

na jambo la tatu lanikasirisha:

Askari ambaye amefilisika,

watu wenye akili wanaodharauliwa,

na mtu anayeacha unyofu na kutenda dhambi.

Huyo Bwana atamwadhibu kwa upanga.

29Ni vigumu kwa mfanyabiashara kuepa makosa,

na mchuuzi kuepa dhambi.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania