The chat will start when you send the first message.
1Mtu mjinga huwa na matumaini ya bure na ya uongo;
ndoto humpa mpumbavu mabawa ya kuruka.
2Kama mtu anayejaribu kushika kivuli na kufukuza upepo
ndivyo alivyo mtu anayeamini ndoto.
3Ndoto ni kama kioo,
sura inayoukabili uso.
4Ni kitu gani kiwezacho kutakaswa na uchafu?
Je, ukweli waweza kupatikana kwa uongo?
5Kupiga bao, ramli na ndoto ni upuuzi;
akili huwa na mawazo kama ya mama anayejifungua.
6Usizitie maanani ndoto
isipokuwa kama zimetoka kwa Mungu Mkuu.
7Maana ndoto zimewadanganya wengi,
na wale wanaozitumaini wameaibishwa.
8Sheria ni kamilifu bila udanganyifu huo,
nayo hekima ni kamilifu kwa mtu mwaminifu:
9Mtu aliyesafiri sana anajua mengi,
na mtu mzoefu wa mengi anajua anachoongea.
10Mtu ambaye hajakumbana na matatizo hajui mengi,
lakini aliyesafiri sana amejipatia maarifa.
11Katika safari zangu nimeona mengi;
ninajua mengi kuliko niwezavyo kuyaeleza.
12Mara nyingi nimekuwa katika hatari ya kifo,
lakini nimechopoka kwa sababu ya maarifa haya.
13Wamchao Bwana wataishi,
maana tumaini lao liko kwake yeye anayewaokoa.
14Amchaye Bwana hatakuwa na woga,
hawezi kuogopa kwani Bwana ndiye tumaini lake.
15Heri mtu ambaye anamcha Bwana!
Maana anamtazamia yeye amtegemeze.
16Bwana huwaangalia kwa wema wale wampendao.
Yeye ni ngao imara na tegemeo lao thabiti;
yeye ni kinga yao mbali na upepo mkali,
ni kivuli chao wakati wa jua kali;
yeye huwalinda wasijikwae,
huwasaidia wasianguke.
17Bwana huijaza mioyo furaha,
na huyatia macho mwanga.
Yeye huwapa watu afya, uhai na baraka
18Mtu akitoa sadaka kitu kilichopatikana kwa udanganyifu
tambiko yake hiyo ina dosari.
Zawadi za wasiotii sheria hazikubaliki.
19Mungu Mkuu hakubali sadaka za wasiomcha,
wala wingi wa sadaka hauwezi kuleta upatanisho.
20Mtu atoaye sadaka kitu alichomnyanganya maskini,
ni sawa na mtu anayemuua mtoto mbele ya baba yake.
21Chakula cha maskini ni uhai wake;
yeyote anayempora maskini chakula ni muuaji.
22Kumnyanganya jirani chakula chake ni kumuua;
na kumnyanganya mwajiriwa mshahara wake ni kuua.
23Mtu mmoja akijenga na mwingine akibomoa,
je, wamefanikiwa chochote ila kutoa jasho?
24Mmoja akimwomba Mungu na mwingine akilaani,
je, Bwana ataisikiliza sauti ya nani?
25Mtu akitawadha baada ya kushika maiti, akaishika tena,
je, amepata faida gani kwa kutawadha kwake?
26Hivyo mtu akifunga kwa ajili ya dhambi zake,
kisha akaenda kufanya mambo yaleyale,
ni nani atakayesikiliza sala yake?
Tena amepata faida gani kwa kujinyenyekesha?