Sira 35

Sira 35

1Anayeishika sheria ametoa sadaka nyingi.

2Anayezifuata amri ametoa sadaka za amani.

3Anayerudisha shukrani anatoa sadaka ya nafaka safi;

4naye anayemsaidia maskini anatoa sadaka ya shukrani.

5Kuachana na uovu kunampendeza Bwana,

na kuacha ubaya ni kujiletea upatanisho.

6Usiende mbele za Bwana mikono mitupu,

7maana vitu hivi vyote vinatakiwa na amri;

8sadaka ya mtu mwadilifu huipaka madhabahu mafuta

na harufu yake nzuri hupanda mbele ya Mungu Mkuu.

9Sadaka ya mwadilifu hukubaliwa;

nayo haitasahaulika milele.

10Mtukuze Bwana kwa ukarimu,

wala usiwe mchoyo juu ya mazao yako ya kwanza.

11Zawadi zako zote uzitoe kwa moyo mkunjufu,

weka wakfu zaka zako kwa furaha.

12Mpe Mungu Mkuu kama alivyokupa,

uwe mkarimu kwa kadiri ulivyo navyo.

13Maana Bwana ndiye anayelipa,

naye atakulipa mara saba.

14Usijaribu kumhonga, maana hatapokea,

15wala usitegemee sadaka ulizopata kwa udanganyifu.

Maana Bwana ni hakimu, wala hana upendeleo.

Haki ya Mungu

16Bwana hataonesha upendeleo kwa maskini;

aliyekosewa anapomwomba, humsikiliza.

17Yeye hayapuuzi maombi ya yatima,

wala maombi ya mjane anapomwambia kisa chake.

18Machozi ya mjane hutiririka mashavuni mwake,

19yakimshtaki mtu aliyesababisha mateso yake.

20Anayemtumikia Bwana na kumpendeza atakubaliwa naye,

sala yake itafika mbinguni.

21Sala ya mnyenyekevu huyapenya mawingu,

nayo haitasimama mpaka imemfikia Bwana.

Hataacha kuomba mpaka Mungu Mkuu amemjibu,

22akamwokoa mwadilifu na kutoa hukumu.

Bwana hatakawia wala hatawaonesha uvumilivu,

mpaka atakapowaponda wasio na huruma,

23na huyalipiza kisasi mataifa maovu;

mpaka awaangamize wenye kiburi wengi

na kuvunjilia mbali utawala wa waovu.

24Atawalipiza kisasi watu kadiri ya matendo yao,

kila mtu kulingana na mipango yake,

25mpaka atakapoamua kisa cha watu wake

na kuwafanya wafurahi kwa sababu ya huruma yake.

26Nyakati za shida, huruma yake hupokelewa kwa furaha

kama mvua wakati wa ukame.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania