The chat will start when you send the first message.
1Utuhurumie ee Bwana Mungu wa wote;
Yafanye mataifa yote yakuogope.
Inua mkono wako dhidi ya mataifa mengine,
2uyafanye yauone uwezo wako mkuu.
3Kama ulivyotutumia kuyaonesha jinsi ulivyo mtakatifu,
vivyo hivyo yatumie kutuonesha utukufu wako.
4Nayo yatajua kama tunavyojua na sisi,
kwamba hakuna Mungu ila wewe, ee Bwana.
5Fanya tena ishara na kufanya miujiza zaidi,
ufanye mkono wako uwe na utukufu zaidi.
6Onesha hasira yako na kumwaga ghadhabu yako;
waangamize wapinzani na kuwafuta maadui.
7Iharakishe ile siku na kukumbuka kiapo chako;
8wafanye watu wasimulie matendo yako makuu.
Yeyote atakayeponyoka ateketezwe na ghadhabu yako kali,
na wale wanaowadhuru watu wako wapate maangamizi.
9Uwaponde wakuu wa maadui zako,
ambao husema: “Hakuna mwingine ila sisi wenyewe!”
10Yakusanye pamoja makabila yote ya Yakobo,
uwape mali yako kama ulivyopanga mwanzoni.
11Wahurumie ee Bwana watu wanaoitwa kwa jina lako;
Waisraeli uliowaita mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.
12Uuonee huruma mji wa hekalu lako,
Yerusalemu, mji wa pumziko lako.
13Uujaze mji wa Siyoni shangwe za matendo yako ya ajabu,
na hekalu lako lijae utukufu wako.
14Uwahakiki watu wako uliowaumba mwanzoni,
na kutimiza unabii uliosemwa kwa jina lako.
15Uwatuze wale wanaokungojea,
na manabii wako waonekane kuwa ni wa kuaminika.
16Usikilize, ee Bwana, sala ya watumishi wako,
kulingana na baraka za Aroni juu ya watu wako.
17Hivyo binadamu wote duniani watajua
kuwa wewe ndiwe Bwana, Mungu wa nyakati zote.
18Chakula chochote chaweza kuliwa,
lakini chakula kingine ni bora kuliko kingine.
19Kama ulimi upimavyo mionjo ya aina ya vyakula,
ndivyo na mwenye akili agunduavyo maneno ya uongo.
20Mwenye akili potovu atasababisha huzuni,
lakini mwenye uzoefu wa maisha atamlipa inavyofaa.
21Mwanamke aweza kuolewa na yeyote,
akini msichana mmoja ni bora kuliko mwingine.
22Uzuri wa mwanamke hufurahisha uso,
na hushinda kila kitu anachotamani mwanamume.
23Kama mwanamke ni mwema na mwenye adabu anapoongea,
mumewe ana bahati kuliko wengine wote.
24Mwanamume akipata mke amepata ubora mkubwa mno,
amejipatia msaidizi bora na nguzo ya msaada.
25Mali isiyolindwa kwa ukuta itaporwa;
ni pasipo mke, mwanamume atatangatanga na kusononeka.
26Nani atakayemwamini jambazi azururaye mji hata mji?
27Hivyo hakuna atakayemwamini mwanamume asiye na kwake,
ambaye ana malazi popote usiku unapomkuta.