Sira 4

Sira 4

1Mwanangu, usimpunje maskini mahitaji yake,

usimtamanishe bure mtu aliye fukara.

2Usimhuzunishe mtu mwenye njaa,

au kumkasirisha mtu mwenye shida.

3Usimzidishie matatizo mtu mwenye taabu,

wala usicheleweshe sadaka yako kwa maskini mwombaji.

4Usikatae kumsaidia mwombaji aliye na taabu,

wala usimpe kisogo maskini.

5Usiepe kumwangalia mtu fukara,

usimpe nafasi ya kukulaani.

6Maana akikulaani katika uchungu alio nao,

Muumba wake ataisikia sala yake.

7Ifanye jumuiya ya watu ipendezwe nawe;

inama kichwa kwa heshima mbele ya wakuu.

8Tega sikio, umsikie mtu maskini,

na kuitikia salamu yake kwa upole.

9Mkomboe anayedhulumiwa makuchani mwa mdhalimu,

wala usiyumbeyumbe unapotoa hukumu.

10Uwe baba kwa walio yatima,

na kama mume kwa mama zao wajane.

Hapo utakuwa mwana wa Mungu Mkuu

naye atakupenda kuliko akupendavyo mama yako.

Hekima ni Mwalimu

11Hekima huwatukuza wanawe,

na kuwasaidia wale wanaomtafuta.

12Ampendaye Hekima, anapenda maisha;

wamtafutao Hekima mapema, watajazwa furaha.

13Anayeambatana naye atapata heshima,

na Bwana atapabariki mahali anapokwenda.

14Wanaomtumikia Hekima, wanamtumikia Mungu Mtakatifu;

Bwana huwapenda wale wanaompenda Hekima.

15Anayemtii Hekima atayahukumu mataifa,

anayemsikia Hekima ataishi kwa usalama.

16Aliye mwaminifu atampata Hekima,

na wazawa wake wataendelea kuwa naye.

17Maana ingawa atampitisha kwanza katika njia za taabu

na kumletea hofu na hali ya woga,

akimjaribu kwa nidhamu mpaka amwamini,

na kumpima kwa kumletea maafa;

18baadaye humjia moja kwa moja na kumfurahisha

na kumjulisha siri zake.

19Lakini mtu huyo akikosea, ataondoka kwake,

na kumwacha kwenye maangamizi yake mwenyewe.

20Chukua tahadhari wakati ufaao na kuepa uovu,

wala usijiletee aibu kwako mwenyewe.

21Maana kuna aibu inayoongoza katika dhambi,

lakini kuna aibu ambayo huleta sifa na heshima.

22Usioneshe ubaguzi kwa hasara yako

au upendeleo na kujiangamiza wewe mwenyewe.

23Usiache kusema wakati unaofaa,

wala usifiche hekima yako.

24Maana hekima yako yajulishwa kwa yale unayosema,

na busara yako kwa maneno unayotamka.

25Usiupinge ukweli,

bali uwe na tahadhari juu ya kutojua kwako.

26Usione aibu kuungama dhambi zako,

usijaribu kupinga mkondo wa mto.

27Usikubali kutawaliwa na mtu mpumbavu,

wala kumpendelea mtawala.

28Pigania ukweli hata mpaka kifo,

naye Bwana Mungu atakupigania.

29Usiwe ovyo katika usemi wako,

wala mzembe katika matendo yako.

30Usiwe kama simba nyumbani kwako,

wala mwenye kuwatuhumu watumishi wako.

31Usiwe mtu wa kupokea tu,

wala kuwa mgumu wa kuwapa wengine.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania