Sira 45

Sira 45

Mose

1Kutoka wazawa wa Yakobo Bwana akamtokeza mtu mwema

aliyepata kibali mbele ya watu wote,

akapendwa na Mungu na watu.

Huyo alikuwa Mose ambaye ni furaha kumkumbuka.

2Bwana alimfanya mwenye utukufu sawa na malaika,

na mwenye nguvu hata akaogopwa na maadui zake.

3Kwa neno la Mose, Bwana alikomesha yale maajabu,

alimfanya atukuke mbele ya wafalme.

Bwana alimpa Mose amri kwa ajili ya watu wake,

akamwonesha sehemu ya utukufu wake.

4Kwa uaminifu na upole wake, Bwana alimweka wakfu,

akamteua miongoni mwa binadamu wote.

5Bwana alimjalia Mose kusikia sauti yake,

akamwongoza katika lile giza kubwa.

Alimpa amri zake ana kwa ana,

sheria ya uzima na maarifa,

ili kuwafunza watu wa Yakobo agano lake,

kuwafundisha Waisraeli maagizo yake.

Aroni

6Bwana alimwinua Aroni, ndugu yake Mose,

mtu mtakatifu kama Mose, wa kabila la Lawi.

7Alifanya naye agano la milele

akampa ukuhani wa watu wake.

Alimpatia mavazi ya fahari,

akamvalisha joho la utukufu.

8Bwana alimvika Aroni ukamilifu mkuu,

akamwimarisha kwa ishara za mamlaka:

Suruali, joho na vazi la kizibao kitakatifu.

9Alimzungushia makomamanga,

na kengele nyingi za dhahabu,

zitoe sauti anapotembea,

sauti zake zisikike hekaluni,

kama ukumbusho kwa watu wake.

10Alimvika vazi takatifu la dhahabu, buluu na rangi zambarau

lililotariziwa na fundi stadi,

akampa vitu vya kuonesha kauli ya kweli.

11Alimvika sufu nyekundu, iliyotengenezwa na fundi wa nakshi,

na vijiwe vya thamani vilivyochongwa kama mhuri

na kutiwa dhahabu, vyote vimetengenezwa na mhunzi wa vito;

vimeandikwa kwa ukumbusho wa idadi ya makabila ya watu wa Israeli.

12Kwenye kilemba chake alitia taji ya dhahabu,

iliyochongwa kama mhuri wa kuwekwa wakfu.

Hiyo ilinakshiwa kwa ufundi mkubwa,

kazi nzuri ya msanii,

nzuri mno kuitazama na imepambwa sana.

13Hakukuwa na vitu vizuri kama hivyo kabla yake,

wala hakuna mgeni aliyewahi kuvaa vitu kama hivyo.

Ni wazawa wake peke yao waliovivaa vitu hivyo milele,

14tambiko atakazotolea zitateketezwa nzima,

nazo zitatolewa daima mara mbili kila siku.

15Mose alimweka Aroni wakfu,

na kumpaka mafuta matakatifu.

Agano la milele lilifanywa naye na wazawa wake,

kwamba watamtumikia Bwana kama makuhani

na kuwabariki watu kwa jina lake.

16Bwana alimteua Aroni kati ya watu wote,

amtolee Bwana tambiko,

afukize ubani wa ukumbusho wenye harufu nzuri,

na kuwafanyia watu upatanisho.

17Alimkabidhi Aroni amri zake,

akampa mamlaka ya kuweka sheria na kuamua,

kuwafundisha watu wa Yakobo maamuzi yake

na kuwaangazia kuhusu sheria yake.

18Watu wa nje waliafikiana kumpinga Mose,

wakamwonea wivu kule jangwani.

Hao walikuwa Dathani, Abiramu na wenzao,

na Kora pamoja na kundi lao wakiwaka hasira.

19Bwana alipoyaona hayo hakupendezwa,

na kwa ghadhabu yake kali akawaangamiza.

Alitenda maajabu dhidi yao

akawateketeza kwa ndimi za moto.

20Kisha akamwongezea Aroni fahari yake,

na kumpa urithi wake mwenyewe:

Haki juu ya matoleo ya malimbuko.

21Chakula chao kinatokana na tambiko za Bwana;

Bwana alimpatia vitu hivyo Aroni na wazawa wake.

22Lakini Aroni hakuwa na sehemu yake ya urithi nchini,

hakuwa na fungu lake miongoni mwa watu;

maana tambiko zake Bwana ndio urithi wake.

Finehasi

23Finehasi, mwanawe Eleazari, ni wa tatu kwa fahari,

maana alikuwa na hamu kubwa ya kumcha Bwana,

akasimama imara wakati watu walipoasi,

akawa tayari kwa wema wake moyoni,

na kuwaombea Waisraeli msamaha wa dhambi.

24Kwa hiyo Bwana akafanya naye agano la amani,

kwamba atakuwa kiongozi wa mahali pa ibada na watu wake,

yeye na wazawa wawe na heshima ya ukuhani milele.

25Kulikuwa pia na agano lingine na Daudi,

mwana wa Yese, wa kabila la Yuda,

urithi wa ufalme wake ulikuwa kwa mtoto hata mtoto,

hali ukuhani wa Aroni ulirithiwa na wazawa wake wote.

26Bwana akujalie hekima moyoni mwako,

uwaamue watu wake kwa haki,

ili ustawi wao usiangamie

na fahari yao idumu vizazi vyao vyote.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania