Sira 46

Sira 46

Yoshua

1Yoshua, mwana wa Nuni alikuwa shujaa vitani,

na alimfuata Mose katika unabii.

Alikuwa, kama jina lake, mkombozi mkubwa wa wateule wa Mungu,

akawalipiza kisasi adui waliopigana nao,

ili kuwapatia Waisraeli urithi wao.

2Jinsi gani alivyokuwa na fahari alipoinua mikono yake,

na kunyosha upanga wake dhidi ya miji!

3Nani kabla yake aliyekuwa imara hivyo?

Maana yeye alipigana vita vya Bwana.

4Je, jua halikusimamishwa kwa mkono wake?

Je, siku haikurefushwa kuwa kama siku mbili?

5Yoshua, alimwomba Mungu Mkuu, Mwenye Nguvu,

wakati maadui walipomsonga kila upande.

6Naye Bwana, aliye mkuu, akamjibu,

akapeleka mvua ya mawe yenye nguvu.

Bwana alilishambulia lile taifa

na kwenye mtelemko wa Beth-horoni akawaangamiza waliompinga.

Hivyo mataifa yakaziona vizuri silaha zake,

kwamba alikuwa anapigana mbele ya Bwana,

maana alimfuata Mungu Mkuu kwa moyo wake wote.

7Katika siku za Mose, Yoshua alikuwa mwaminifu

yeye na Kalebu, mwana wa Yefune,

walisimama imara kuupinga umati,

wakawazuia watu wasitende dhambi,

na kunyamazisha manunguniko yao.

8Kati ya watu laki sita waliokuwa safarini,

ni hao wawili tu waliobakizwa,

wakawaongoza watu kwenye nchi yao wenyewe,

nchi iliyotiririka maziwa na asali.

9Bwana alimpa Kalebu nguvu,

nayo ilibaki naye hadi uzeeni.

Hivyo alikwenda mpaka nchi ya milima

na wazawa wake wakaiteka kuwa urithi wao,

10hata watu wote wa Israeli wakaona

kwamba ni vizuri kumfuata Bwana.

Waamuzi

11Kisha kulikuwa na waamuzi, kila mmoja maarufu kikwake,

ambao hawakudanyanyika kuabudu sanamu

na kumwacha Bwana.

Walikumbukwa daima kwa sifa.

12Miili yao na ipate nguvu huko makaburini,

na majina yao hao waliomcha Bwana

yadumu kwa njia ya wazawa wao.

Samueli

13Samueli alipendwa na Bwana.

Akiwa nabii wa Bwana alianzisha ufalme,

akawapaka mafuta watawala wa watu wake.

14Aliiamua jumuiya ya watu kulingana na sheria ya Bwana,

naye Bwana akawalinda watu wa Yakobo.

15Kwa uaminifu wake alithibitishwa kuwa kweli nabii,

na kwa maneno yake akawa mwonaji wa kutegemewa.

16Alimwomba Bwana, Mwenye Nguvu,

wakati aliposongwa na maadui kila upande,

akamtolea Bwana tambiko ya kondoo mchanga.

17Kisha Bwana alinguruma kutoka mbinguni,

akaifanya sauti yake isikike kwa kishindo kikubwa.

18Aliwafutilia mbali viongozi wa watu wa Tiro,

na watawala wote wa Wafilisti.

19Kabla ya usingizi wake wa mwisho,

Samueli alishuhudia mbele ya Bwana na mteule wake,

kwamba hakuwahi kuchukua mali ya mtu yeyote,

hata kama ni jozi ya viatu.

Hakuna mtu yeye aliyemshtaki.

20Hata baada ya kufariki aliendelea kutoa unabii

akamfunulia mfalme mwisho wake;

alitoa sauti kutoka kaburini,

alitoa unabii kufutilia mbali uovu wa watu.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania