1 Yohana 5

Mwenye kumtegemea Yesu huushinda ulimwengu.

1*Kila mwenye kuyategemea ya kwamba: Yesu ni Kristo, amezaliwa na Mungu. Naye kila mwenye kumpenda mzazi aliyemzaa humpenda hata yeye aliyezaliwa naye.[#1 Yoh. 4:15-16; Yoh. 8:42.]

2Hapo ndipo, tunapotambua, kama tunawapenda wana wa Mungu, tukimpenda Mungu na kufanya maagizo yake.

3Kwani kumpenda Mungu ni kuyashika maagizo yake, nayo maagizo yake si magumu.[#Mat. 11:30; Yoh. 14:15,23-24.]

4Kwani kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Nako kunakotushindisha ulimwengu ndiko kumtegemea Mungu.[#Yoh. 16:33.]

5Yuko nani anayeushinda ulimwengu, asipokuwa mwenye kuyategemea ya kwamba: Yesu ni Mwana wake Mungu?*[#1 Yoh. 4:4.]

Roho na maji na damu.

6Huyu Yesu Kristo ndiye aliyekuja mwenye maji na damu; hakuja na maji tu, ila alikuja mwenye maji na damu. Naye Roho ndiye anayeyashuhudia, kwani Roho ndiye kweli.[#Mat. 2:16; Yoh. 15:26; 19:34-35.]

7Kwa hiyo wako watatu wanaoshuhudia mbinguni: Baba na Neno na Roho Mtakatifu; nao hawa watatu ni mmoja. Tena wako watatu wanaoshuhudia nchini: Roho na Maji na Damu;

8hao watatu nao wamepatana ushahidi kuwa mmoja.

9*Tukiuitikia ushuhuda wa watu, basi, ushuhuda wa Mungu ni mkubwa zaidi, kwani ushuhuda wa Mungu ndio huo, aliomshuhudia Mwana wake mwenyewe.

10Mwenye kumtegemea Mwana wa Mungu huo ushuhuda anao mwake. Asiyemtegemea Mungu amemfanya kuwa mwongo yeye, kwani hakuutegemea ushuhuda, Mungu aliomshuhudia Mwana wake mwenyewe.[#Rom. 8:16.]

11Nao ushuhuda ndio huu wa kwamba: Mungu ametupa uzima wa kale na kale; uzima huu umo mwake Mwana wake yeye.

12Aliye naye Mwana, anao hata uzima; asiye naye Mwana wa Mungu, hata uzima hanao.

13Haya nimewaandikia ninyi mnaolitegemea Jina la Mwana wa Mungu, mpate kujua: uzima wa kale na kale mnao.[#Yoh. 20:31.]

14Kunakotupa moyo wa kumjia wenye furaha ndiko kujua, yo yote, tutakayomwomba kwa hayo, ayatakayo, hutusikia.[#1 Yoh. 3:21-22; Yoh. 14:13.]

15Nasi tukijua, ya kuwa anatusikia yo yote, tutakayomwomba, twajua: maombo, tuliyomwomba, tumekwisha kupewa.*

Yako makosa yauayo, tena yako yasiyoua.

16Mtu akimwona ndugu yake, akikosa kosa lisiloua, na amwombee; ndipo, Mungu atakapompa uzima pamoja na wakosaji wenziwe wafanyayo yasiyoua. Liko kosa linaloua; hapo sisemi, mtu amwombee.[#Mat. 12:31; Ebr. 6:4-6.]

17Upotovu wote ni wa kukosa, tena yako makosa yasiyoua.[#1 Yoh. 3:9; Yoh. 17:15.]

18Twajua: kila aliyezaliwa na Mungu hakosi, ila aliyezaliwa na Mungu hujiangalia, yule Mbaya asimguse.

19Twajua: sisi tu wa Kimungu, lakini ulimwengu wote umo katika nguvu ya yule Mbaya.[#Gal. 1:4.]

20Nasi twajua: Mwana wa Mungu amekuja, akatupa mawazo ya kumtambua mwenye kweli. Nasi tumo mwake mwenye kweli, ndimo mwake Yesu Kristo, Mwana wake. Huyu ndiye Mungu wa kweli na uzima wa kale na kale.[#Yoh. 17:3; Rom. 9:5.]

21Vitoto, jiangalieni, msije kutambikia vinyago! Amin.[#1 Kor. 10:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania