2 Mambo 28

2 Mambo 28

Ahazi ni mfalme mbaya.

(Taz. 2 Fal. 16.)

1Ahazi alikuwa mwenye miaka 20 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 16 mle Yerusalemu; hakuyafanya yanyokayo machoni pake Bwana kama baba yake Dawidi,

2ila akaendelea kuzishika njia za wafalme wa Waisiraeli, akatengeneza navyo vinyago vya Mabaali vilivyoyeyushwa.

3Naye yeye akavukiza bondone kwa Bin-Hinomu, hata wanawe akawatumia kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa motoni akiyafuata hayo matapisho ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli.[#5 Mose 18:9-10,12.]

4Akatambika na kuvukiza vilimani pa kutambikia napo pengine palipoinukia juu, hata chini ya kila mti uliokuwa wenye majani mengi.[#1 Fal. 14:23.]

5Kwa hiyo Bwana akamtia mkononi mwa mfalme wa Ushami, wakampiga, wakateka kwake mateka mengi, wakawapeleka Damasko. Akatiwa hata mkononi mwa mfalme wa Waisiraeli aliyempiga pigo kubwa.

6Kwani Peka, mwana wa Remalia, akaua katika nchi ya Yuda siku moja watu 120000, wote walikuwa wenye nguvu, kwa kuwa walimwacha Bwana Mungu wa baba zao.

7Hata Zikiri, fundi wa vita wa Waefuraimu, akamwua Masea, mwana wa mfalme, na Azirikamu, mkuu wa nyumba ya mfalme, na Elkana aliyemfuata mfalme kwa ukuu.

8Nao wana wa Isiraeli wakateka kwa ndugu zao 200000, wanawake na watoto wa kiume na wa kike na mali nyingi, walizozinyang'anya kwao; haya mateka wakayapeleka Samaria.

Mfumbuaji Odedi.

9Huko kulikuwa na mfumbuaji wa Bwana, jina lake Odedi. Huyu akavitokea vile vikosi, vilipoingia Samaria, akawaambia: Tazameni! Kwa kuwa Bwana Mungu wa baba zenu amewakasirikia sana Wayuda, akawatia mikononi mwenu, lakini ninyi kwa machafuko mkamwaga kwao damu nyingi zilizofika hata mbinguni.[#1 Mose 18:21; Ezr. 9:6.]

10Sasa ninyi mwataka kuwanyenyekeza kwa nguvu hawa wana wa Yuda na wa Yerusalemu, wawe watumwa na vijakazi wenu. Lakini nanyi mliyojipatia kwake Bwana Mungu wenu sizo manza tu, mlizozikora?

11Kwa hiyo nisikieni sasa, mrudishe kwao mateka, mliyoyateka kwa ndugu zenu! Kwani nanyi makali ya Bwana yawakayo moto yanawakalia.

12Ndipo, walipoinuka waume waliokuwa wakuu wa wana wa Efuraimu, ndio Azaria, mwana wa Yohana, Berekia, mwana wa Mesilemoti, na Hizikia, mwana wa Salumu, na Amasa, mwana wa Hadilai; hawa wakawainukia waliotoka vitani,

13wakawaambia: Msiyalete mateka yenu hapa! Kwani hivyo tutakora manza kwa Bwana, nanyi mnataka kweli kuyaongeza makosa yetu na manza zetu, kwani manza zetu ni nyingi, nayo makali yawakayo moto yanatukalia sisi Waisiraeli.

14Ndipo, wapiga vita walipoyaacha mateka yao machoni pao wakuu napo pao mkutano wote pamoja na zile mali, walizozinyang'anya;

15nao wale waume waliotajwa hapa juu majina yao wakainuka kuyachukua hayo mateka, kisha wote waliokuwa uchi wakawavika wakiwapa nguo na viatu na kuvitoa mlemle katika mapokonyo, kisha wakawapa vyakula na vya kunywa na mafuta ya kukipaka, nao wote waliojikwaakwaa wakawapandisha punda, wakawapeleka kwa ndugu zao Yeriko, ule mji wenye mitende, kisha wakarudi Samaria.[#Fano. 25:21-22.]

Mungu anampatiliza Ahazi.

16Siku zile mfalme Ahazi akatuma kwao wafalme wa Asuri, waje kumsaidia,

17kwa maana Waedomu walikuja tena, wakawapiga, wakachukua mateka.

18Nao Wafilisti wakaiingia miji ya nchi ya tambarare na miji ya kusini katika nchi ya Yuda na kunyang'anya mali, wakateka Beti-Semesi na Ayaloni na Gederoti na Soko na mitaa yake na Timuna na mitaa yake na Gimuzo na mitaa yake, wakakaa humo.

19Kwani Bwana aliwanyenyekeza Wayuda kwa ajili ya Ahazi, mfalme wa Waisiraeli, kwani aliwalegeza Wayuda alipomvunjia Bwana maagano.

20Ndipo, Tilgati-Pilneseri, mfalme wa Asuri, alipomjia, lakini akamsonga, hakumpatia nguvu.

21Kwani Ahazi alichukua kwa nguvu yaliyokuwamo Nyumbani mwa Bwana namo nyumbani mwa mfalme nazo mali za wakuu, akampa mfalme wa Asuri, lakini hakusaidiwa naye.

22Papo hapo, aliposongeka, yeye mfalme Ahazi akazidi kumvunjia Bwana maagano,

23akaitumikia miungu ya Damasko iliyompiga, akasema: kwa kuwa miungu ya wafalme wa Ushami ndiyo iliyowasaidia, basi, nitaitambikia hiyohiyo, wanisadie; nayo ndiyo iliyomkwaza mwenyewe na Waisiraeli wote.

24Kisha Ahazi akavikusanya vyombo vya Nyumba ya Mungu, akavivunjavunja hivyo vyombo vya Nyumba ya Mungu, akaifunga milango ya Nyumba ya Bwana, akajitengenezea pa kutambikia pembeni po pote mle Yerusalemu.

25Hata kila mji mmoja wa Yuda akautengenezea vilima vya kuvukizia miungu mingine juu yao; ndivyo, alivyomkasirisha Bwana Mungu wa baba zake.

Kufa kwake Ahazi.

26Mambo yake mengine na njia zake zote, za kwanza na za mwisho, tunaziona, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli.

27Kisha Ahazi akaja kulala na baba zake, wakamzika katika mji wa Yerusalemu, kwani hawakumpeleka penye makaburi ya wafalme wa Waisraeli. Naye mwanawe Hizikia akawa mfalme mahali pake.[#2 Mambo 21:20.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania