The chat will start when you send the first message.
1Hizikia akatuma kwa Waisiraeli na kwa Wayuda wote, nao Waefuraimu na Wamanase akawaandikia barua, waje Yerusalemu Nyumbani mwa Bwana Mungu wa Isiraeli kula sikukuu ya Pasaka ya Bwana Mungu wa Isiraeli.[#2 Mambo 35:1.]
2Mfalme na wakuu wake nao mkutano wote wa watu wakafanya shauri huko Yerusalemu kula sikukuu ya Pasaka katika mwezi wa pili.[#2 Mambo 30:15.]
3Kwani hawakuweza kuila siku zile, kwa kuwa watambikaji wa kutosha hawajajieua, nao watu hawakukusanyika Yerusalemu.
4Shauri hili likanyoka machoni pake mfalme napo pao mkutano wote.
5Wakaagiza kupiga mbiu kwa Waisiraeli wote toka Beri-Seba hata Dani, watu waje kula sikukuu ya Pasaka ya Bwana Mungu wa Isiraeli mle Yerusalemu, kwani tangu siku nyingi hawakuila, kama ilivyoandikwa.
6Wajumbe wapigao mbio wakaenda na barua, walizopewa na mfalme na wakuu wake, katika nchi zote za Waisiraeli na za Wayuda, wakasema, kama walivyoagizwa na mfalme: Wana wa Isiraeli rudini kwake Bwana, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Isiraeli! Ndipo, atakaporudi kwao waliosalia kwenu kwa kupona mikononi mwa wafalme wa Asuri.
7Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu walioyavunja maagano ya Bwana Mungu wa baba zao, akawatoa, waangamizwe, kama mnavyoona nanyi.
8Sasa msizishupaze kosi zenu kama baba zenu! Ila mpeni Bwana mikono mkija Patakatifu pake, alipopatakasa kuwa pake kale na kale! Kamtumikieni Bwana Mungu wenu! Ndipo, makali yake yawakayo moto yatakapoondoka kwenu.
9Kwani mkirudi kwake Bwana, ndugu zenu na wana wenu watahurumiwa nao waliowateka na kuwahamisha, wapate kurudi katika nchi hii, kwani Bwana Mungu wenu ni mwenye utu na huruma, hatauondoa uso kwenu, mkirudi kwake.
10Basi, hao wajumbe wapigao mbio wakaenda kuingia mji kwa mji katika nchi ya Efuraimu na ya Manase hata Zebuluni, lakini watu wakawacheka na kuwafyoza.
11Watu wa Aseri tu na wa Manase na wa Zebuluni wakajinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.
12Hata katika nchi ya Yuda mkono wa Mungu ukawako, ukawapa kuwa wenye moyo mmoja wa kulifanya agizo la mfalme na la wakuu, Bwana alilowaambia.
13Katika mwezi wa pili wakakusanyika Yerusalemu watu wengi kuila sikukuu ya Mikate isiyochachwa, ukawa mkutano mkubwa sana.
14Wakainuka, wakapaondoa pote pa kutambikia palipokuwamo Yerusalemu, navyo vivukizo vyote wakaviondoa, wakavitupa katika mto wa Kidoroni.
15Kisha wakachinja wana kondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, kwani watambikaji na Walawi walijieua kwa kuona soni, wakapeleka ng'ombe za tambiko Nyumbani mwa Bwana.[#4 Mose 9:11.]
16Wakasimama mahali pao palipowapasa, kama Maonyo ya Mose aliyekuwa mtu wa Mungu yalivyoagiza. Hao watambikaji wakazinyunyiza damu, walizozipokea mikononi mwa Walawi.[#2 Mambo 29:34.]
17Kwani katika huo mkutano walikuwako wengi wasiojieua; kwa sababu hii Walawi wakawachinjia wote wasiotakata wana kondoo wa Pasaka, wawatakase kuwa wa Bwana.
18Kwani watu wengi sana wa Efuraimu na wa Manase na wa Isakari na wa Zebuluni hawakujitakasa, kwani hawakuila kondoo ya Pasaka, kama ilivyoandikwa. Lakini Hizikia aliwaombea kwamba: Bwana aliye mwema na amwondolee makosa[#2 Mose 12.]
19kila mtu aliyeuelekeza moyo wake kumtafuta Mungu Bwana aliye Mungu wa baba zake, ingawa hakuupata utakaso upapasao Patakatifu.
20Bwana akamsikia Hizikia, akawaponya hao watu.
21Ndivyo, wana wa Isiraeli waliokuwamo Yerusalemu walivyoila sikukuu ya Mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa, nao Walawi na watambikaji wakamshangilia Bwana siku kwa siku na kumpigia Bwana vyombo vyenye sauti za nguvu.
22Naye Hizikia akawaambia Walawi wote waliokuwa wenye akili njema katika kazi ya Bwana maneno yaliyoingia mioyoni mwao, wakaila sikukuu hii ya ushahidi siku saba, wakitoa vipaji vya tambiko vya shukrani, wamshukuru Bwana Mungu wa baba zao.[#2 Mambo 32:6.]
23Kisha mkutano wote ukafanya shauri kuendelea siku saba tena, wakala sikukuu tena siku saba kwa furaha.
24Kwani Hizikia, mfalme wa Wayuda, aliutolea huo mkutano madume ya ng'ombe 1000 na mbuzi na kondoo 7000, nao wakuu waliutolea mkutano madume ya ng'ombe 1000 na mbuzi na kondoo 7000; nao watambikaji walijieua wengi.[#2 Mambo 35:7.]
25Wakafurahi watu wote wa huo mkutano wa Wayuda pamoja na watambikaji na Walawi na mkutano wao wote waliotoka kwa Waisiraeli nao wageni waliotoka katika nchi ya Waisiraeli nao waliokaa katika nchi ya Wayuda.
26Ikawa furaha kubwa mle Yerusalemu, kwani tangu siku za Salomo, mwana wa Dawidi, mfalme wa Waisiraeli, haya kuwamo mle Yerusalemu mambo kama hayo.
27Mwisho watambikaji na Walawi wakainuka, wakawabariki watu; sauti zao zikasikiwa, nayo maombo yao yakafika mbinguni kwenye Kao lake takatifu.