Mpiga mbiu 5

Mpiga mbiu 5

Yaangalie unayoyasema!

1Iangalie miguu yako ukienda Nyumbani mwa Mungu, uje kusikia! Hii inafaa kuliko vipaji vya tambiko, wajinga wanavyovitoa, kwani wao hawajui, ya kuwa hufanya mabaya.[#1 Sam. 15:22.]

2Usibabaike tu kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe mwepesi wa kutoa maneno mbele ya Mungu! Kwani Mungu yuko mbinguni, wewe nawe uko huku nchini, kwa hiyo maneno yako sharti yawe machache.[#Yak. 1:19.]

3Kwani ndoto huja kwa kutumikia mengi, nayo sauti ya mjinga kujulika kwa kusema maneno mengi.[#Mbiu. 10:14; Fano. 10:19.]

4Kama umemwapia Mungu kiapo cho chote, usikawe kukilipa! Kwani hapendezwi na wajinga; cho chote, ulichokiapa, kilipe![#5 Mose 23:21.]

5Ukiwa hukuapa, ni vema, kuliko ukiwa hukilipi, ulichokiapa.[#5 Mose 23:22.]

6Usiache, kinywa chako kiukoseshe mwili wako, wala usimwambie malaika: Hili ni kosa tu! Unataka kwa nini, Mungu ayakasirikie, uliyoyasema, kisha aziangamize kazi za mikono yako?[#Mal. 2:7.]

7Kwani ndoto zikiwa nyingi, nayo maneno yakiwa mengi, mengi ni ya bure; kwa hiyo umwogope Mungu!

Mali ni za bure.

8Ukiona, maskini akikorofishwa, tena mashauri yaliyo sawa nayo mambo yaongokayo yakiondolewa mjini kwa nguvu, usivistaajabu, vikifanyika hivyo! Kwani aliye mkuu yuko na mkuu kumpita amwangaliaye, tena juu yao wote yuko aliye mkuu mwenyewe.

9Kwa ajili ya hayo yote inafaa, nchi ikiwa na mfalme ayatazamaye mashamba, yalimwe.

10Apendaye fedha hashibi fedha, wala apendaye mali hatoshewi na mapato. Hayo nayo ni ya bure.[#Fano. 28:22.]

11Mema yakiwa mengi, basi, nao watakao kuyala huwa wengi; naye mwenyewe hupata nini, isipokuwa hii tu, macho yake yakiyatazama kwa kufurahi.

12Usingizi wa mtu wa kazi ni mtamu, kama anakula vichache au vingi; lakini shibe za mkwasi hazimpatii mapumziko ya kulala usingizi.

13Uko ubaya unaouguza, nami nimeuona chini ya jua, ni huu: mali zilizoangaliwa na mwenyewe mwisho zikimpatia mabaya.

14Mali hizo zikipotea kwa kutumikiwa vibaya, naye akiwa amezaa mtoto, basi, hakuna hata kidogo kitakachokuwa mkononi mwake.

15Vivyo hivyo, alivyotoka tumboni mwa mama yake mwenye uchi, ndivyo, atakavyokwenda tena, kama alivyokuja, asichukue kwa masumbuko yake cho chote cha kwenda nacho mkononi mwake.[#Iy. 1:21; Sh. 49:18.]

16Kweli huu ndio ubaya uuguzao. Vivyo hivyo, alivyokuja, ndivyo, atakavyokwenda; tena anapataje kwa kuusumbukia upepo?

17Naye siku zake zote alizila na kukaa gizani mwenye masikitiko mengi kwa kuugua na kwa kukasirika.

Kunakofaa ni kutoshewa.

18Yasikie, niliyoyaona kuwa mema na mazuri! Ni haya: mtu akila, akinywa na kuona mema kwa masumbuko yake, aliyoyasumbuka chini ya jua siku zote za maisha yake, Mungu alizompa, kwani hili ndilo fungu lake.[#Mbiu. 2:24; Fano. 15:15.]

19Tena mtu ye yote, Mungu aliyemgawia mali na mema ya dunia hii na kumpa uwezo wa kuyala na kulichukua fungu lake na kuyafurahia masumbuko yake, basi, ajue, ya kuwa hilo ndilo gawio lake Mungu.

20Kwani huyu hakumbuki kabisa, jinsi siku zake za kuwapo zilivyo, kwani Mungu humwitikia kwa kuufurahisha moyo wake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania