Hosea 1

Hosea 1

Hosea anaoa mwanamke mgoni, awafumbulie Waisiraeli ukaidi wao.

1Hili ni neno la Bwana lililomjia Hosea, mwana wa Beri, Uzia na Yotamu na Ahazi na Hizikia walipokuwa wafalme wa Wayuda, naye Yoroboamu, mwana wa Yoasi, alipokuwa mfalme wa Waisiraeli.[#2 Fal. 14:23; Yes. 1:1; Amo. 1:1.]

2Hapo, Bwana alipoanza kusema na Hosea, Bwana akamwambia Hosea: Nenda, ujichukulie mwamamke mgoni, ujipatie nao watoto wa ugoni! Kwani nchi hii inafuata ugoni kwa kumwacha Bwana.

3Akaenda, akamchukua Gomeri, binti Dibulemu; naye akapata mimba, akamzalia mwana wa kiume.

4Bwana akamwambia: Mwite jina lake Izireeli! Kwani kiko bado kitambo kidogo, ndipo, nitakapoulipisha mlango wa Yehu damu za Izireeli na kuukomesha ufalme wa Isiraeli.[#2 Fal. 10:30.]

5Siku ile ndipo, nitakapouvunja upindi wa Isiraeli katika bonde la Izireeli.

6Kisha akapata mimba tena, akazaa mwana wa kike. Bwana akamwambia: Mwite jina lake Hahurumiwi! Kwani sitawahurumia tena walio mlango wa Isiraeli nikiendelea kuwaondolea mabaya yao.[#Hos. 2:1,23.]

7Lakini walio mlango wa Yuda nitawahurumia na kuwaokoa kwa nguvu za Bwana Mungu wao, nisiwaokoe kwa nguvu za pindi wala za panga wala za mapigano wala za farasi, wala kwa nguvu za wapanda farasi.

8Alipokuwa amemzoeza Hahurumiwi, asinyonye maziwa, akapata mimba tena, akazaa mwana wa kiume.

9Bwana akamwambia: Mwite jina lake Si ukoo wangu! Kwani ninyi ham ukoo wangu, nami sitakuwa tena wenu.[#Hos. 2:1,23.]

10Lakini tena hesabu ya wana wa Isiraeli itakuwa kama mchanga wa ufukoni usiopimika wala usiohesabika; itakuwa hapo, hao wanaoambiwa sasa: Ninyi ham ukoo wangu waambiwe: M wanawe Mungu aliye Mwenye uzima.[#1 Mose 22:17; Rom. 9:26.]

11Ndipo, wana wa Yuda na wana wa Isiraeli watakapokusanyika pamoja, wajiwekee kichwa kimoja, wakitoka kwao, waje hapo, kwani siku ile ya Izireeli itakuwa kuu.[#Yes. 11:11-13; Yer. 3:18; Ez. 37:22.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania