Hosea 2

Hosea 2

1Hapo waiteni ndugu zenu Ukoo wangu na maumbu zenu Huhurumiwa![#Hos. 1:6,9.]

Agano la Mungu linavunjwa nao walio ukoo wake.

2Mgombezeni mama yenu! Haya! Mgombezeni!

Kwani yeye siye mke wangu, nami si mumewe.

Na auondoe ugoni wake, usiwe mbele yake,

nao uzinzi wake, usiwe penye maziwa yake,

3nisije kumvua, akawa mwenye uchi,

na kumweka, awe, kama alivyokuwa siku ile, alipozaliwa,

nikamgeuza kuwa kama nyika,

nikamfanya kuwa kama nchi kavu nikimwua kwa kiu.

4Nao wanawe sitawahurumia, kwani ndio wana wa ugoni;

5kwa kuwa mama yao amefanya ugoni,

akatenda yenye soni yeye aliyewachukua mimba,

maana alisema: Nitawafuata wapenzi wangu

wanipao chakula changu na maji yangu,

nayo manyoya yangu ya kondoo na pamba zangu,

nayo mafuta yangu na vinywaji vyangu.

6Kwa hiyo utaniona, nikiiziba njia yako kwa miiba,

nitajenga hata ukuta, asione pake pa kupitia.

7Atakapowakimbilia wapenzi wake, asiwafikie,

atakapowatafuta, asiwaone;

ndipo, atakaposema: Na nije kumrudia mume wangu wa kwanza,

kwani hapo naliona mema kuliko sasa.

8Naye hajui, ya kuwa ni mimi niliyempa

zile ngano na zile pombe na yale mafuta,

ya kuwa ni mimi niliyemzidishia fedha na dhahabu, walizomtolea Baali.

9Kwa hiyo na nirudi kuzichukua ngano zangu, siku zitakapotimia,

nazo pombe zangu, pangu patakapotimia,

nitampokonya nguo zangu za manyoya ya kondoo na za pamba,

alizo nazo za kuufunika uchi wake.

10Sasa nitayafunua yake yenye soni machoni pa wapenzi wake,

tena hakuna mtu atakayemponya mkononi mwangu.

11Nitazikomesha furaha zake zote na sikukuu zake

za miandamo ya mwezi nazo za mapumziko na mikutano yake yote.

12Nitaiharibu mizabibu yake na mikuyu yake,

aliyoisema: Hii ndiyo kipaji, wapenzi wangu walichonipa;

nitaigeuza kuwa misitu, nyama wa porini waile.

13Nitampatilizia siku za kuvitambikia vinyago vya Baali,

alivyovivukizia uvumba

alipojipamba na kuvaa pete zake na ushanga wake

akiwafuata wapenzi wake kwa kunisahau mimi;

ndivyo, asemavyo Bwana.

Mungu analirudia Agano lake la kale.

14Kwa hiyo mtaniona, nikimbembeleza na kumpeleka nyikani,

niseme naye kimoyomoyo.

15Ndiko, nitakakompa mizabibu yake, akitoka huko,

nalo Bonde la Akori nitaligeuza kuwa mlango wa kingojeo;

ndipo, atakapoitika kama hapo, alipokuwa kijana,

alipotoka katika nchi ya Misri kuja huku.

16Ndivyo asemavyo Bwana:

Siku hiyo ndipo, utakaponiita Mume wangu,

usiniite tena Bwana wangu.

17Ndipo, nitakapoyaondoa majina ya vinyago vya Baali kinywani mwako,

visitajwe tena kwa majina yao.

18Siku hiyo nitawafanyia agano

nao nyama wa porini n ndege wa angani na wadudu wa

nchini,

nitayavunja mata na panga na magombano,

yatoke katika nchi hiyo, niwakalishe salama.

19Nitakuposa, uwe wangu kale na kale,

nitakuposa, uwe wangu kwa mashauri yaongokayo

na kwa huruma zenye upole.

20Nitakuposa, uwe wangu kwa kweli;

ndipo, utakapomjua Bwana.

21Siku hiyo ndipo, nitakapoitikia; ndivyo, asemavyo

Bwana;

nitaziitikia mbingu nazo zitaiitikia nchi hii.

22Nayo nchi hii itaziitikia ngano, nazo pombe na mafuta,

nayo hayo yatamwitikia Izireeli (Mungu mpanzi).

23Nami nitampanda katika nchi hii, awe wangu, nimhurumie

Hahurumiwi,

tena nitamwambia Si ukoo wangu: Ndiwe Ukoo wangu,

naye atasema: Ndiwe Mungu wangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania