Yesaya 37

Hizikia anaomba wokovu kwa Bwana na kuupata.

(1-38: 2 Fal. 19:1-37.)

1Ikawa, mfalme Hizikia alipoyasikia, akazirarua nguo zake, akajifunga gunia, akaingia Nyumbani mwa Bwana.[#1 Mose 37:29.]

2Akamtuma Eliakimu aliyekuwa mtunza nyumba ya mfalme na Sebuna aliyekuwa mwandishi na watambikaji wazee waliokuwa wamejifunga magunia kwenda kwa mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi.

3Wakamwambia: Hivi ndivyo, Hizikia anavyosema: Siku hii ya leo ni siku ya kusongwa na ya kupatilizwa na ya kutupwa, kwani watoto wamefikisha kuzaliwa, lakini nguvu za kuwazaa haziko.

4Labda Bwana Mungu wako ameyasikia yale maneno ya mkuu wa askari, ambayo bwana wake, mfalme wa Asuri, alimtuma kumbeua Mungu Mwenye uzima kwa kuyasema; Bwana Mungu wako na ampatilizie yale maneno, aliyoyasikia! Nawe na uje kuwaombea waliosalia walioko bado!

5Wakaja hao watumishi wa mfalme Hizikia kwake Yesaya.

6Yesaya akawaambia: Mwambieni bwana wenu hivi: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Usiyaogope yale maneno, uliyoyasikia, vijana wa mfalme wa Asuri waliyonitukana nayo!

7Utaniona, nikimtia roho nyingine, asikie habari, kisha arudi katika nchi ya kwao, nako huko kwao nitamwangusha kwa upanga.

8Mkuu wa askari aliporudi akamkuta mfalme wa Asuri, akipiga vita Libuna, kwani alisikia, ya kuwa mfalme ameondoka Lakisi.

9Huko mfalme akasikia habari ya Tirihaka, mfalme wa Nubi, kwamba: Tazama, ametoka kukupelekea vita! Ndipo, alipotuma wajumbe kwake Hizikia kwamba:

10Hivyo mtamwambia Hizikia, mfalme wa Yuda, mkisema: Asikudanganye Mungu wako, wewe umwegemeaye kwamba: Yerusalemu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Asuri.

11Kumbuka, uliyoyasikia mwenyewe, wafalme wa Asuri waliyozifanyizia nchi zote wakiziangamiza na kuzitia mwiko wa kuwapo! Nawe utapona?

12Je? Miungu ya wamizimu iliwaponya, baba zangu walipowamaliza, wale watu wa Gozani na wa Harani na wa Resefu nao wana wa Edeni walioko Tilasari?[#Yes. 36:18.]

13Yuko wapi mfalme wa Hamati, naye mfalme wa Arpadi, naye mfalme wa mji wa Sefarwaimu, naye wa Hena, naye wa Iwa?

14Hizikia alipozichukua barua hizo mikononi mwa wajumbe, akazisoma; kisha akapanda kwenda Nyumbani mwa Bwana. Humo Hizikia akazizingua mbele yake Bwana,

15kisha Hizikia akamlalamikia Bwana akisema:

16Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, uyakaliaye Makerubi, wewe ndiwe Mungu peke yako wa nchi zote za kifalme, wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi.

17Bwana, litege sikio lako, usikie! Bwana, yafumbue macho yako, uone! Yasikie haya maneno yote ya Saniheribu, aliyoyatuma, akubeue uliye Mungu Mwenye uzima!

18Ni kweli, Bwana, wafalme wa Asuri wameziangamiza zile nchi zote na mashamba yao,

19wakaitupa miungu yao motoni, kwani hiyo siyo miungu, ila ni kazi za mikono ya watu, ni miti na mawe tu, kwa hiyo waliweza kuiharibu.

20Bwana Mungu wetu, tuokoe sasa mkononi mwake! Ndipo, nchi zote za kifalme zitakapojua, ya kuwa wewe ndiwe Bwana peke yako.[#Yes. 40:5.]

21Ndipo, Yesaya, mwana wa Amosi, alipotuma kwake Hizikia kumwambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli, uliyemlalamikia kwa ajili ya Saniheribu, mfalme wa Asuri.

22Hili ndilo neno, Bwana alilolisema kwa ajili yake: Mwanamwali binti Sioni, amekubeza na kukufyoza; binti Yerusalemu, amekutingishia kichwa nyuma yako.

23Ni nani, uliyembeua na kumtukana? Ni nani, uliyempalizia sauti na kuyaelekeza macho yako juu? Ni Mtakatifu wa Isiraeli.

24Bwana ndiye, uliyembeua vinywani mwa watumishi wako ukisema: Kwa kuwa magari yangu ni mengi, nimepanda milimani juu huko ndani Libanoni, nikaikata miangati yake mirefu na mivinje yake iliyochaguliwa, nikafika kwake huko juu kileleni, msitu unakokuwa kama shamba lake la miti.[#Yes. 14:8.]

25Nilipochimba nikapata maji ya kunywa, tena nikaikausha mito yote ya Misri kwa nyayo za miguu yangu.

26Je? Hujasikia kwamba: Niliyoyafanya kale, niliyoyalinganisha siku za mbele, sasa nimeyaleta, yatimie; wewe ukawa wa kutowesha miji yenye maboma, iwe machungu ya mawe na mabomoko.

27Nao waliokaa humo mikono yao ikawa mifupi, wakastuka, wakaingiwa na soni, wakawa kama mapalizi ya shambani au kama ndago za uwandani au kama majani yameayo juu ya kipaa au kama shamba linyaukalo pasipo kuzaa.

28Ninakujua kukaa kwako na kutoka kwako na kuingia kwako; ninavijua navyo, unavyovikasirikia.

29Kwa sababu unanikasirikia, majivuno yako yakapanda kuingia masikioni mwangu, nitakutia pete yangu puani mwako, nayo hatamu yangu midomoni mwako, kisha nitakurudisha katika njia ileile, uliyokuja nayo.[#5 Mose 32:27.]

30Hiki kitakuwa kielekezo chako, Hizikia: Mwaka huu mtakula yaliyojipanda yenyewe, mwaka wa pili mtakula yaliyoota mashinani, mwaka wa tatu mmwage mbegu, mvune. Nayo mizabibu mtapanda, myale matunda yao.

31Ndipo, masao yao waliopona wa mlango wa Yuda watakapotia mizizi chini, kisha watazaa matunda juu.[#Yes. 27:6.]

32Kwani Yerusalemu yatatokea masao, nako mlimani kwa Sioni watatokea waliopona. Wivu wake Bwana Mwenye vikosi utayafanya hayo.

33Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya mfalme wa Asuri: Hatauingia mji huu, wala hatapiga humu mshale, wala hataukaribishia ngao, wala hataujengea boma la kuuzingia.

34Njia, aliyokuja nayo, ileile atarudi nayo. Lakini humu mjini hatamwingia; ndiyo, asemavyo Bwana.

35Nitaukingia mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Dawidi.

36Akatokea malaika wa Bwana, akapiga makambini kwa Waasuri watu 185000. Walipoamka asubuhi wakawaona hao wote, ya kuwa wamekufa, ni mizoga tu.[#Yes. 17:14; 31:8.]

37Ndipo, Saniheribu, mfalme wa Asuri, alipoondoka, aende zake, akarudi kwao, akakaa Niniwe.

38Ikawa, alipoomba nyumbani mwa mungu wake Nisiroki, ndipo, wanawe, Adarameleki na Sareseri walipompiga kwa upanga, ksha wakaikimbilia nchi ya Ararati, naye mwanawe Esari-Hadoni akawa mfalme mahali pake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania