Yesaya 39

Wajumbe wa Babeli wanamjia Hizikia.

(1-8: 2 Fal. 20:12-19.)

1Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani, mfalme wa Babeli, akatuma barua na matunzo kwake Hizikia kwani alisikia ya kuwa aliugua, akapona.[#2 Mambo 32:31.]

2Hizikia akawafurahia, akawaonyesha nyumba ya kuwekea mali zake, mlimo na fedha na dhahabu na manukato na mafuta mazuri, nayo nyumba yote ya mata yake, nayo yote pia yaliyooneka katika vilimbiko vyake. Hakikuwako kitu, ambacho Hizikia hakuwaonyesha, wala nyumbani mwake, wala katika ufalme wake wote.

3Kisha mfumbuaji Yesaya akaja kwa mfalme Hizikia, akamwuliza: Waume hao wamesema nini? Wametoka wapi wakija kwako? Hizikia akajibu: Wametoka nchi ya mbali, wakaja kwangu toka Babeli.

4Akauliza: Wameona nini katika nyumba yako? Hizikia akajibu: Wameyaona yote yaliyomo nyumbani mwangu, hakuna kitu katika vilimbiko vyangu, ambacho sikuwaonyesha.

5Ndipo, Yesaya alipomwambia Hizikia: Sikia neno la Bwana Mwenye vikosi!

6Tazama! Ziko siku zitakazokuja, ndipo, yote yaliyomo nyumbani mwako, nayo yote, baba zako waliyoyalimbika hata siku hii ya leo, yatakapopelekwa Babeli, hakitasalia hata kimoja; ndivyo, Bwana anavyosema.

7Namo katika wanao wa kiume waliotoka mwilini mwako, uliowazaa mwenyewe, watachukuliwa wengine, watumikie jumbani mwa mfalme wa Babeli.

8Hizikia akamwambia Yesaya: Neno la Bwana, ulilolisema, ni jema, kwani alisema moyoni: Katika siku zangu utakuwako utengemano wa kweli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania