Yesaya 42

Mtumishi wa Bwana ni mwanga wao wamizimu na kiongozi wao walio wake.

1Mtazameni mtumishi wangu, nimshikizaye!

Mtazameni mteule wangu,

ambaye Roho yangu inapendezwa naye!

Nitamtia Roho yangu, awatolee wamizimu habari,

ya kwamba hukumu yao iko.

2Hatapiga kelele, wala hatalia,

wala hatapaza sauti yake njiani.

3Utete uliokunjika hatauvunja,

wala utambi unaotoka moshi bado hatauzima,

aitokeze ile hukumu kuwa ya kweli.

4Hatazimia, wala hatashindika,

mpaka yanyokayo ayashikize katika nchi,

navyo visiwa vitayangoja maonyo yake.

5Hivi ndivyo, anavyosema Mungu Bwana

aliyeziumba mbingu na kuziwamba,

aliyeitanda nchi na mazao yake;

watu walioko aliwapa pumzi,

nazo roho aliwapa wao watembeao huku.

6(Anasema:) Mimi Bwana nimekuita, kwa kuwa ni mwongofu,

na nikushike mkono wa kukulinda,

nikuweke kuwa agano la watu na mwanga wa wamizimu,

7ufumbue macho ya vipofu, utoe wafungwa kifungoni,

nao wakaao gizani uwatoe nyumbani, wanamolindwa.

8Mimi ni Bwana, hili ndilo Jina langu.

Sitampa mwingine utukufu wangu,

wala sitavipa vinyago mashangilio yangu.

9Mkitazama, yale ya kwanza yametimia,

tena sasa mimi ninatangaza mapya;

yanapokuwa hayajatokea bado, nawapasha ninyi habari zao.

10Mwimbieni Bwana wimbo mpya

na kumshangilia kwenye mapeo ya nchi,

ninyi mtembeao baharini nayo yote yaliyomo,

ninyi visiwa nao wakaao huko!

11Nazo nyika na miji iliyoko ipaze sauti

pamoja na vijiji, Wakedari wakaamo!

Wakaao magengeni na wapige shangwe,

nako vilimani kileleni na wapige makelele!

12Na wamtukuze Bwana!

Na wayatangaze mashangilio yake visiwani!

13Bwana atatokea kama mwenye nguvu,

kama mpiga vita atauamsha ukali,

atapiga yowe na vilio, awatolee adui zake nguvu.

14Nimenyamaza tangu kale, nikatulia na kujizuia;

lakini sasa nitalia pamoja na kufoka na kutweta

kama mwanamke anayezaa.

15Nitachoma milima na vilima,

niyanyaushe majani yao yote,

nayo majito nitayageuza kuwa nchi kavu,

hata mabwawa nitayakausha.

16Lakini vipofu nitawatembeza katika njia, wasizozijua,

katika mikondo, wasiyoijua, nitawaendesha,

nitaligeuza giza lililoko mbele yao kuwa mwanga,

napo palipopotoka nitapanyosha.

Maneno haya nitayafanya, sitayaacha.

17Hapo watakuwa wamerudi nyuma kwa kutiwa soni kabisa

wao walioviegemea vinyago,

walioviambia vinyago vilivyoyeyushwa kwa shaba:

Ninyi m miungu yetu.

18Ninyi viziwi, sikilizeni!

Ninyi vipofu, chungulieni, mpate kuona!

19Kipofu yuko nani, asipokuwa mtumishi wangu?

Aliye kiziwi kama mjumbe wangu wa kumtuma yuko nani?

Yuko nani aliye kipofu kama mpendwa?

Yuko nani aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana?

20Uliona mengi, lakini hukuyaangalia;

alikuzibua masikio, lakini hayakusikia.

21Bwana kwa hivyo, alivyo mwongofu,

akapendezwa kuyakuza na kuyatukuza Maonyo.

22Lakini sasa ukoo huu ni ukoo wa watu

walionyang'anywa na kupokonywa mali zao,

wote pia wamenaswa miinani,

wakafichwa nyumbani mwa kufungia watu,

wakatekwa, tena hakuna aliyewaopoa,

wakapokonywa mali zao, tena hakuna aliyesema: Rudisha!

23Kwenu yuko nani atakayeyasikia hayo?

Yuko nani atakayeyaangalia atakapoyasikia huko nyuma?

24Ni nani aliyemtoa Yakobo, apokonywe mali zake?

Ni nani aliyemtia Isiraeli mikononi mwa wanyang'anyi?

Si mimi Bwana, waliyemkosea,

walipokataa kuzishika njia zangu

na kuyasikia Maonyo yangu?

25Ndipo, alipowamiminia makali yake

yaliyo yenye moto na makorofi ya vita,

yakamzunguka na kumchoma lakini hakujua maana,

yakamwunguza, lakini hayakumfikia moyoni.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania