The chat will start when you send the first message.
1*Roho ya Bwana Mungu inanikalia,
kwa hiyo Bwana amenipaka mafuta,
niwapigie maskini mbiu njema.
Amenituma, niwaponye waliovunjika mioyo,
niwatangazie mateka, ya kuwa watakombolewa,
nao waliofungwa, ya kuwa watatolewa mafungoni,
2niutangaze mwaka wa Bwana upendezao
na siku ya lipizi ya Mungu wetu,
niwatulize mioyo wote wasikitikao,
3niwapoze mioyo yao wausikitikiao Sioni,
nikiwapa vilemba penye majivu
na mafuta ya furaha penye mavazi ya matanga
na mashangilio penye roho za kuzimia,
watu wawaite Mivule iongokayo
na Shamba la Bwana la kujipatia matukuzo.
4Watayajenga mabomoko yako ya kale,
nayo mahame ya siku za mbele watayasimamisha tena,
nayo miji iliyo machungu ya mawe tu watairudishia upya,
ndiyo iliyokuwa imeangamia kwao vizazi na vizazi.
5Wageni watasimama hapo wakiyachunga makundi yenu,
waliotoka nchi nyingine watakuwa wakulima wenu
na watunza mizabibu yenu.
6Nanyi mtaitwa watambikaji wa Bwana,
mtaambiwa: M watumishi wa Mungu wetu;
mapato ya wamizimu mtayala,
nayo matukufu yao yatakuwa mali zenu.*
7Penye soni walizotiwa watapata malipo mara mbili,
penye matusi watalishangilia fungu lao.
Kweli katika nchi yao watakuwa wenye mafungu mawili,
tena watapata kuchangamka kale na kale.
8Kwani mimi Bwana ninapenda maamuzi yapasayo,
nikachukiwa nayo yaliyopokonywa kwa upotovu,
kwa hiyo nitawapa kwa kweli yayapasayo matendo yao,
nitafanya nao agano la kale na kale.
9Mazao yao yatajulikana kwa wamizimu,
nao waliotoka miilini mwao watajulikana
katikati ya makabila ya watu;
wote watakaowaona watawatambua,
ya kuwa ndio mazao yaliyobarikiwa na Bwana.
10Kufurahi nitamfurahia Bwana,
roho yangu itampigia Mungu wangu shangwe,
kwani amenivika mavazi ya wokovu,
akanifunika kwa kanzu ya wongofu,
niwe kama mchumba mume,
akiutengeneza urembo wa kichwani kuwa kama wa mtambikaji,
au kama mchumba mke,
akijipamba na kuvaa vito vyake.
11Kwani kama nchi inavyoyatoa machipukizi yake,
kama shamba linavyozichipuza mbegu zake,
ndivyo, Bwana Mungu atakavyochipuza wongofu
na mashangilio mbele ya wamizimu wote.