The chat will start when you send the first message.
1Kisha akatembea na kuingia mwenyewe mji kwa mji na kijiji kwa kijiji, akiutangaza Utume mwema wa ufalme wa Mungu nao wale kumi na wawili walikuwa pamoja naye,[#Luk. 4:43.]
2hata wanawake wengine waliokuwa wameponywa pepo wabaya na magonjwa; ndio Maria anayeitwa Magadalene aliyetokwa na pepo saba,[#Mar. 15:40-41; 16:9.]
3na Yohana, mkewe Kuza aliyekuwa mshika mali wa Herode, na Susana na wengine wengi, wakawatumikia na kuwagawia, waliyokuwa nayo.
4*Lakini lilipokusanyika kundi la watu wengi na kumwendea toka kila mji, akasema kwa mfano:
5Mpanzi alitoka kuzimiaga mbegu zake. Ikawa, alipozimiaga, nyingine zikaangukia njiani, zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.
6Nyingine zikaangukia mwambani, zikaota, mara zikanyauka, kwa kuwa hazina mchanga mbichi.
7Nyingine zikaangukia miibani katikati, nayo miiba ikaota pamoja nazo, ikazisonga.
8Nyingine zikaangukia penye mchanga mwema, zikaota, zikazaa punje mia. Alipoyasema haya akapaza sauti kwamba: Mwenye masikio yanayosikia na asikie!
9Wanafunzi wake walipomwuliza maana ya mfano huu,[#Yes. 6:9-10.]
10akasema: Ninyi mmepewa kuyatambua mafumbo ya ufalme wa Mungu, lakini wale wengine huambiwa kwa mifano, kusudi watazame, lakini wasione, wasikilize, lakini wasijue maana.
11Nao mfano maana yake ni hii: mbegu ndio Neno la Mungu.[#1 Petr. 1:23.]
12Zilizoko njiani ndio wenye kulisikia; kisha huja Msengenyaji, akaliondoa Neno mioyoni mwao, wasipate kulitegemea na kuokoka.
13Nazo zilizoko mwambani ndio hao: wanapolisikia Neno hulipokea kwa furaha, lakini hawana mizizi, hulitegemea kitambo kidogo, kisha siku za kujaribiwa hujitenga.
14Lakini zilizoangukia miibani ndio hao: wanalisikia, lakini huenda zao, Neno likisongwa nayo masumbuko na mali nyingi na furaha za ulimwenguni; hivyo hawaivishi punje.
15Lakini zilizoko penye mchanga mzuri ndio hao: wanalisikia Neno na kulishika katika mioyo iliyo mizuri na miema; ndio wanaozaa matunda kwa kuvumilia.*
16Hakuna mwenye kuwasha taa anayeifunika kwa chombo au anayeiweka mvunguni mwa kitanda; ila huiweka juu ya mwango, maana wanaoingia waone mwanga.[#Luk. 11:33; Mat. 5:15; Mar. 4:21.]
17Kwani hakuna ililofichwa lisiloonekana halafu; wala hakuna njama isiyotambulikana halafu na kutokea waziwazi.[#Mat. 10:26.]
18Basi, mwangalie, jinsi mnavyosikia! Kwani aliye na mali atapewa; lakini asiye na kitu atachukuliwa hata kile, alichokiwaza kuwa chake.[#Luk. 19:26.]
19Kisha mama yake na ndugu zake wakamjia, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya kundi la watu.
20Alipopashwa habari kwamba: Mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuonana na wewe,
21akajibu akiwaambia: Mama yangu na ndugu zangu ndio hawa wanaolisikia Neno la Mungu na kulifanya.
22Ikawa siku moja, mwenyewe akajipakia chomboni na wanafunzi wake, akawaambia: Tuvuke kwenda ng'ambo ya ziwa! Wakatweka matanga.
23Walipoendelea baharini, akalala usingizi. Kukashuka msukosuko wa upepo ziwani, chombo kikajaa maji, wakafikisha kuangamia.
24Ndipo, walipomjia, wakamwamsha wakisema: Bwana, Bwana, tunaangamia! Naye alipoinuka, akaukaripia upepo na mawimbi ya maji, yakatulia, kukawa kimya.
25Kisha akawaambia: Tegemeo lenu liko wapi? Kwa kuogopa wakastaajabu tu, wakasemezana wao kwa wao: Ni mtu gani huyu, ya kuwa anaagiza hata upepo na maji, nayo yanamtii!
26Walipokwisha kuvuka, wakafika katika nchi ya Wagerasi iliyoelekea Galilea.
27Aliposhuka pwani akakutana na mwanamume wa mji ule aliyekuwa na pepo; huyo siku nyingi hakuvaa nguo, wala hakukaa nyumbani, ila hukaa penye makaburi.
28Alipomwona Yesu akapiga kelele, akamwangukia, akapaza sauti akisema: Tuko na jambo gani, mimi na wewe Yesu, Mwana wa Mungu Alioko huko juu? Nakuomba wewe, usiniumize.
29Kwani alikuwa amemwagiza yule pepo mchafu, amtoke yule mtu. Kwani mara nyingi alikuwa amemsukumasukuma, naye alikuwa amefungwa kwa minyororo na kwa mapingu na kulindwa, akavivunja vile vifungo, akakimbizwa na pepo kwenda mahali pasipo na watu.
30Yesu alipomwuliza: Jina lako nani? akasema: Maelfu. Kwani alikuwa ameingiwa na pepo wengi.
31Nao wakambembeleza, asiwaagize kwenda zao kuzimuni.
32Basi, kulikuwako kundi la nguruwe wengiwengi waliokuwako malishoni mlimani. Wakambembeleza, awape ruhusa ya kuwaingia wale. Alipowapa ruhusa,
33pepo wakamtoka yule mtu, wakawaingia nguruwe; ndipo, kundi lilipotelemka mbio mwambani, wakaingia ziwani, wakatoswa.
34Lakini wachungaji walipoliona lililofanyika, wakakimbia, wakalitangaza mjini na mashambani.
35Watu wakatoka kwenda kulitazama lililofanyika; walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo, anavyokaa miguuni pa Yesu, amevaa nguo, tena ana akili zake, wakashikwa na woga.
36Nao walioyaona wakawasimulia, mwenye pepo alivyoponywa.
37Kwa hiyo watu waliokuwa wengi katika nchi za pembenipembeni za Wagerasi wakamwomba wote, aondoke kwao, kwani walishikwa na woga mkubwa. Alipojipakia chomboni, arudi,
38yule mtu aliyetokwa na pepo akamwomba, afuatane naye. Lakini yeye akamwaga akisema:
39Rudi nyumbani mwako, ukayasimulie yote, Mungu aliyokutendea! Ndipo, alipokwenda zake, akayatangaza katika mji mzima yote, Yesu aliyomtendea.
40Yesu aliporudi, kundi la watu likampokea. Kwani wote walikuwa wakimngoja.
41Mara akaja mtu, jina lake Yairo; huyo alikuwa jumbe wa nyumba ya kuombea. Akamwangukia Yesu miguuni, akambembeleza, aje nyumbani mwake,
42kwani mwanawe wa kike wa pekee aliyekuwa mwenye miaka 12 aliingia kufani. Alipokwenda naye, watu wengi sana wakamsongasonga.
43Kukawa na mwanamke mwenye ugonjwa wa kutoka damu tangu miaka 12. Kwa kuwa hakuweza kuponywa na mtu ye yote,
44akamjia nyuma, akaligusa pindo la nguo yake. Papo hapo kijitojito cha damu yake kikakoma.
45Yesu akasema: Yuko nani aliyenigusa? Walipokana wote, Petero akasema: Bwana, makundi ya watu wanakusonga na kubanana.
46Yesu akasema: Yuko aliyenigusa, kwani nimetambua, jinsi nguvu ilivyonitoka.
47Yule mwanamke alipoona, ya kuwa hakufichika, akaja na kutetemeka, akamwangukia, akamweleza mbele ya watu wote sababu ya kumgusa na jinsi alivyopona papo hapo.
48Naye akamwambia: Mwanangu, kunitegemea kwako kumekuponya, nenda na kutengemana![#Luk. 7:50.]
49Angali akisema, akaja mtu wa jumbe wa nyumba ya kuombea, akasema: Binti yako amekwisha kufa, usimsumbue mfunzi tena!
50Yesu alipoyasikia akamwambia: Usiogope nitegemea tu! Atapona.
51Alipoingia nyumbani hakumpa mtu ruhusa kuingia pamoja naye, ila Petero na Yohana na Yakobo na baba yake mwana na mama yake.
52Kwa kuwa wote waliomboleza na kumlilia, akasema: Msilie! kwani hakufa, ila amelala usingizi tu.[#Luk. 7:13.]
53Ndipo, walipomcheka sana, maana walijua, ya kuwa amekwisha kufa.
54Kisha akamshika mkono wake, akapaza sauti akisema: Mtoto, inuka!
55Papo hapo roho yake ikarudi, akafufuka; naye akawaagiza, apewe chakula.
56Wazazi wake washangaa. Naye akawakataza, wasimwambie mtu lililofanyika.[#Luk. 5:14; Mar. 7:36.]