Mateo 12

Mateo 12

Kukonyoa masuke.

(1-8: Mar. 2:23-28; Luk. 6:1-5.)

1Siku zile Yesu alipita katika mashamba siku ya mapumziko; nao wanafunzi wake walipoona njaa wakaanza kukonyoa masuke, wakala.[#5 Mose 23:25.]

2Lakini Mafariseo walipoviona wakamwambia: Tazama, wanafunzi wako wanafanya yaliyo mwiko kuyafanya siku ya mapumziko.[#2 Mose 20:10.]

3Naye akawaambia: Hamkusoma, Dawidi alivyofanya alipoona njaa yeye na wenziwe?[#1 Sam. 21:6.]

4Hapo aliingia Nyumbani mwa Mungu, wakaila mikate aliyowekewa Bwana, nayo kuila ni mwiko kwake na kwa wenziwe, huliwa na watambikaji peke yao.[#3 Mose 24:9.]

5Tena hamkusoma katika Maonyo, ya kuwa siku za mapumziko watambikaji wa pale Patakatifu huivunja miiko ya siku ya mapumziko, nao hawakosi?[#4 Mose 28:9-10.]

6Lakini nawaambiani: Hapa yupo aliye mkuu kuliko Patakatifu.

7Lakini kama mngalitambua maana ya neno la kwamba:

Huruma ndizo, nizitakazo, lakini vipaji vya tambiko

sivyo, basi, hamngaliwawazia mabaya wasio na kosa.

8Kwani Mwana wa mtu ni bwana wa siku ya mapumziko.*

Mkono wa kupooza.

(9-14: Mar. 3, 1-6; Luk. 6, 6-11.)

9Alipoondoka huko akaenda kuingia katika nyumba yao ya kuombea.

10Akaona mtu mwenye mkono uliokaukiana. Wakamwuliza wakisema: Iko ruhusa kuponya siku ya mapumziko? maana walitafuta la kumsuta.[#Luk. 14:3.]

11Nay akawaambia: Mwenye kondoo mmoja tu akitumbukiwa naye shimoni siku ya mapumziko, kwenu yuko asiyemkamata na kumwopoa?

12Je? Mtu hapiti kondoo kabisa? Kwa hiyo iko ruhusa kufanya mema siku ya mapumziko.[#Luk. 14:5.]

13Ndipo, alipomwambia yule mtu: Unyoshe mkono wako! Nao, alipounyosha, ukageuka kuwa mzima kama ule mwingine.

14Lakini Mafariseo wakatoka, wakamlia njama ya kumwangamiza.[#Yoh. 5:16.]

Utete uliopondeka.

(15-21: Mar. 3:7-12.)

15Yesu alipoyatambua akaondoka kule.[#Mar. 3:7-12.]

16Watu wengi wakamfuata, akawaponya wote;[#Mat. 8:4.]

17lakini akawatisha, wasimtangaze, kusudi litimie, mfumbuaji Yesaya alilolisema:[#Yes. 42:1-4.]

18Tazameni, huyu ndiye mtoto wangu, niliyemchagua;

ni mpendwa wangu, ambaye Roho yangu inapendezwa naye.

Nitamtia Roho yangu, awatangazie wamizimu,

ya kwamba hukumu yao iko.

19Hatateta, wala hatapiga kelele,

wala mtu hatamsikia kinywa chake majiani.

20Utete uliopondeka hatauvunja kabisa,

wala utambi unaotoka moshi bado hatauzima,

mpaka aitokeze ile hukumu kuwa ya kushinda.

21Jina lake ndilo, wamizimu watakalolingojea.

Kumbeza Roho.

(22-45: Mar. 3:22-30; Luk. 11:14-26,29-32.)

22Hapo akaletewa mwenye pepo aliyekuwa kipofu na bubu. Alipomponya, yule bubu akapata kusema na kuona.

23Ndipo, makundi ya watu waliposhangaa wote wakisema: Kumbe huyu siye mwana wa Dawidi?

24Mafariseo walipoyasikia wakasema: Huyu hafukuzi pepo, isipokuwa kwa nguvu ya Belzebuli aliye mkuu wa pepo.[#Mat. 9:34.]

25Kwa kuyajua hayo mawazo yao, Yesu akawaambia: Kila ufalme unapogombana wao kwa wao huwa mahame tu, nao kila mji au nyumba tu inapogombana wao kwa wao haitasimamika.

26Naye Satani akimfukuza Satani mwenziwe amejigombanisha mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamikaje?

27Nami nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya Belzebuli, Je? Wana wenu huwafukuza kwa nguvu ya nani? Kwa hiyo hao ndio watakaowaumbua.

28Lakini mimi nikiwafukuza pepo kwa nguvu ya Roho ya Mungu, ufalme wa Mungu umekwisha kuwafikia ninyi.[#1 Yoh. 3:8.]

29Au mtu atawezaje kuingia katika nyumba ya mwenye nguvu, aviteke vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Kisha ataweza kuiteka nyumba yake.[#Yes. 49:24.]

30Asiye wa upande wangu hunikataa; naye asiyekusanya pamoja nami hutapanya.[#Mar. 9:40.]

31Kwa hiyo nawaambiani: Kila kosa na kila neno la kumbeza Mungu watu wataondolewa, lakini la kumbeza Roho hawataondolewa.[#Ebr. 6:4,6; 10:26; 1 Yoh. 5:16.]

32Mtu ye yote atakayesema neno la kumkataa Mwana wa mtu ataondolewa; lakini mtu atakayesema neno la kumkataa Roho Mtakatifu hataondolewa, wala katika ulimwengu huu wa sasa, wala katika ule utakaokuja.[#Luk. 12:10; 1 Tim. 1:13,19; Ebr. 10:26-27.]

33Mkipanda mti nzuri, basi mtapata hata matunda mazuri. Au mkipanda mti mwovu, basi, mtapata hata matunda maovu. Kwani mti hutambulikana kwa matunda yake.[#Mat. 7:17.]

34Enyi wana wa nyoka, mnawezaje kusema mema, mlio wabaya? Kwani moyo unayoyajaa, ndiyo, kinywa kinayoyasema.

35Mtu mwema hutoa mema katika kilimbiko chake chema, lakini mtu mbaya hutoa mabaya katika kilimbiko chake kibaya.

36Nami nawaambiani: Siku ya hukumu watu wataulizwa kila neno baya walilolisema.[#Yak. 3:6,9.]

37Kwani kwa maneno yako utapata wongofu, vile vile utapata hukumu kwa maneno yako.

Kielekezo cha mfumbuaji Yona.

38Hapo walikuwapo waandishi na Mafariseo, wakamwuliza wakisema: Mfunzi, twataka, ufanye kielekezo, tukione.[#Mat. 16:1.]

39Naye akajibu akiwaambia: Wao wa ukoo huu mbaya wenye ugoni wanatafuta kielekezo, lakini hawatapata kielekezo, ila kielekezo cha mfumbuaji Yona.

40Kwani kama Yona alivyokuwa tumboni mwa nyangumi siku tatu mchana na usiku, vivyo naye Mwana wa mtu atakuwa ndani ya nchi siku tatu mchana na usiku.[#Yona 2:1-2.]

41Siku ya hukumu waume wa Niniwe watauinukia ukoo huu, wauumbue; kwani walijuta kwa tangazo la Yona. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Yona![#Yona 3:5.]

42Yule mfalme wa kike aliyetoka kusini atauinukia ukoo huu siku ya hukumu auumbue. Kwani yeye alitoka mapeoni kwa nchi, aje kuusikia werevu wa Salomo uliokuwa wa kweli. Tena tazameni, hapa yupo anayempita Salomo![#1 Fal. 10:1-10.]

43Pepo mchafu anapomtoka mtu hupita mahali pasipo na maji akitafuta kituo asikione.

44Halafu husema: Nitarudi nyumbani mwangu, nilimotoka. Anapokuja huiona, ni tupu, tena imefagiwa na kupambwa;

45ndipo, anapokwenda kuchukua pepo saba wengine walio wabaya kuliko yeye, wawe wenziwe; nao huingia, wakae humo: hivyo ya mwisho ya mtu yule yatakuwa mabaya kuliko ya kwanza. Ndivyo, vitakavyowapata wao wa ukoo huu ulio mbaya.[#2 Petr. 2:20.]

Mama na ndugu.

(46-50: Mar. 3:31-35; Luk. 8:19-21.)

46*Alipokuwa akisema bado na makundi ya watu, mara mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje kwa kumtaka, waseme naye. Mtu akamwambia:[#Mat. 13:55.]

47Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje kwa kutaka, waseme na wewe.

48Naye akajibu akimwambia yule aliyesema naye: Mama yangu ni nani? Nao ndugu zangu ni akina nani?[#Luk. 2:49.]

49Akawanyoshea wanafunzi wake mkono, akasema: Watazameni walio mama yangu na ndugu zangu!

50Kwani mtu ye yote atakayeyafanya, ayatakayo Baba yangu alioko mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu na dada yangu na mama yangu.*[#Yoh. 15:14; Rom. 8:29; 2 Kor. 5:16; Ebr. 2:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania