Mateo 9

Mateo 9

Mgonjwa wa kupooza.

(1-8: Mar. 2:1-12; Luk. 5:17-26.)

1*Akaingia chomboni, akavuka, akafika mjini mwake yeye.[#Mat. 4:13.]

2Papo hapo wakamletea mgonjwa wa kupooza aliyelala kitandani. Yesu alipoona, walivyomtegemea, akamwambia mwenye kupooza: Tulia, mwanangu! Makosa yako yameondolea.

3Ndipo, waandishi waliokuwako waliposema mioyoni: Huyu anambeza Mungu.[#Mar. 2:7.]

4Kwa kuyajua hayo mawazo yao Yesu akasema: Mbona mnawaza mabaya mioyoni mwenu?[#Mat. 12:25; Yoh. 2:25.]

5Kwani kilicho chepesi ni kipi? kusema: Makosa yako yameondolewa! au kusema: Inuka, uende?

6Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, - basi, akamwambia mwenye kupooza: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako!

7Ndipo, alipoinuka akaenda nyumbani kwake.

8Lakini makundi ya watu walipoyaona wakaogopa, wakamtukuza Mungu aliyewapa watu nguvu kama hizo.*

Kuitwa kwa Mateo.

(9-13: Mar. 2:13-17; Luk. 5:27-32.)

9*Yesu alipotoka huko, aende zake, akaona mtu anayeitwa Mateo, amekaa forodhani. Akamwambia: Nifuata! Akainuka, akamfuata.

10Ikawa, alipokaa chakulani nyumbani mwake, ndipo, walipokuja watoza kodi na wakosaji wengi, wakakaa chakulani pamoja na Yesu na wanafunzi wake.

11Mafariseo walipowaona wakawaambia wanafunzi wake: Kwa nini mfunzi wenu anakula pamoja na watoza kodi na wakosaji?[#Luk. 15:2.]

12Yesu alipoyasikia akasema: walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa.[#Luk. 16:15; Rom. 3:23.]

13Lakini nendeni zenu, mkajifunze maana ya neno hili:

Huruma ndizo, nizitakazo, lakini vipaji vya tambiko sivyo. Kwani sikujia kuwaita wongofu, ila wakosaji.*

Kufunga.

(14-17: Mar. 2: 18-22; Luk. 5:33-38.)

14Ndipo, walipomjia wanafunzi wa Yohana wakisema: Kwa nini sisi na Mafariseo hufunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?[#Mat. 11:19; Luk. 18:12.]

15Yesu akawaambia: Walioalikwa arusini hawawezi kusikitika hapo, bwana arusi akingali pamoja nao. Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; ndipo, watakapofunga. Hakuna mtu anayetia kiraka cha nguo mpya katika kanzu chakavu,[#Yoh. 3:29; Ufu. 22:17.]

16kwani kinaondoa pote paliposhonwa katika kanzu, hivyo tundu lake litakuwa kubwa zaidi.[#Yoh. 1:17.]

17Wala watu hawatii mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani wakiitia mle, viriba vitapasuka, mvinyo imwagike, navyo viriba vitaangamia. Ila hutia mvinyo mpya katika viriba vipya; hivyo vyote viwili vitakaa.[#Rom. 10:4; Gal. 5:1.]

Binti Yairo.

(18-26: Mar. 5:22-43; Luk. 8:41-56.)

18*Alipokuwa akiwaambia haya, mara akaja jumbe, akamwangukia akisema: Binti yangu amekufa sasa hivi; lakini uje umbandikie mkono wako! mdipo atakapokuwa mzima tena.

19Yesu akaondoka, akafuatana naye pamoja na wanafunzi wake.

20Mara akaja mwanamke mwenye kutoka damu miaka 12, akamjia nyuma, akaligusa pindo la nguo yake,

21maana alisema moyoni: Hata nikiigusa nguo yake tu nitapona.[#Mat. 14:36.]

22Lakini Yesu akageuka, akamwona, akasema: Tulia, mwanangu! Kunitegemea kwako kumekuponya. Yule mwanamke akapona saa ileile.

23Yesu alipoingia nyumbani mwa jumbe akawaona wapiga filimbi na kundi la watu, wakiomboleza,

24akasema: Ondokeni! Kwani kijana hakufa, ila amelala usingizi tu; ndipo, walipomcheka sana.[#Yoh. 11:11; 14:25.]

25Lakini wale watu walipokwisha fukuzwa, akaingia, akamshika mkono wake; ndipo, yule kijana alipoinuka.

26Habari hizi zikatoka, zikaenea katika nchi ile yote.*

Vipofu wawili.

27Yesu alipotoka huko, aende zake, wakamfuata vipofu wawili, wakapaza sauti za kuita: Tuhurumie, mwana wa Dawidi!

28Alipoingia nyumbani, wale vipofu wakamjia. Yesu akawauliza: Mwanitegemea kwamba: Naweza kufanya hivyo? Wakamwambia: Ndio, Bwana.

29Ndipo, alipowagusa macho akisema: Hayo, mliyoyategemea, na myapate vivyo hivyo![#Mat. 8:13.]

30Ndipo, macho yao yalipofumbuka. Kisha Yesu akawakemea akisema: Angalieni, mtu hata mmoja asiyasikie haya![#Mat. 8:4.]

31Lakini wale walipotoka wakamsimulia po pote katika nchi ile yote.

Bubu.

32Hao walipotoka, mara wakamletea bubu aliyepagawa na pepo. Naye pepo alipokwisha fukuzwa, yule bubu akaweza kusema.

33Makundi ya watu wakastaajabu wakisema: Tangu zamani havijaonekana katika Isiraeli vilivyo kama hivi.

34Lakini Mafariseo wakasema: Nguvu ya mkuu wa pepo ndiyo, huyu anayofukuzia pepo.[#Mat. 12:24-32.]

35*Yesu akawa akizunguka mijini mote na vijijini, akawafundisha katika nyumba zao za kuombea, akautangaza Utume mwema wa ufalme, akaponya ugonjwa wote na unyonge wote.[#Mat. 4:23.]

36Lakini alipowatazama makundi ya watu akawaonea uchungu, kwani walikuwa wamechoka kwa kuteswa na kutawanyishwa kama kondoo wasio na mchungaji.[#Mat. 14:14; Mar. 6:34; Ez. 34:5-6.]

37Ndipo, alipowaambia wanafunzi wake: Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.[#Luk. 10:2.]

38Mwombeni mwenye mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake!*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania