Nehemia 6

Nehemia 6

Nehemia analimaliza jengo la boma.

1Kisha Sanibalati na Tobia na Mwarabu Gesemu nao adui zetu wengine wakasikia, ya kuwa nimelijenga boma, usisalie ufa humo; lakini siku zile sijatia bado milango malangoni.

2Ndipo, Sanibalati na Gesemu walipotuma kwangu kwamba: Njoo, tukutane pamoja penye vijiji vilivyomo bondeni kwa Ono! Kwani waliwaza kunifanyizia mabaya.

3Nikatuma wajumbe kwao kwamba: Mimi nina kazi kubwa ya kuifanya, kwa hiyo siwezi kushuka. Mbona niiache kazi hii, ikome, nikishuka kuja kwenu?

4Wakatuma kwangu kama mara nne kuniambia maneno yayo hayo, nami nikawajibu yayo hayo.

5Kisha Sanibalati akatuma kijana wake kwangu mara ya tano kuniambia yayo hayo, hata barua iliyo wazi ilikuwa mkononi mwake.

6Humo yalikuwa yameandikwa haya: Katika wamizimu yanasimuliwa, naye Gasemu anayasema, ya kuwa wewe na wayuda mnawaza kumwinukia mfalme, kwa sababu hii unalijenga boma, wewe upate kuwa mfalme wao, na mengine kama hayo.[#Ezr. 4:12.]

7Umeweka hata wafumbuaji, wakutangaze mle Yerusalemu kwamba: Huyu ni mfalme katika nchi ya Yuda! Maneno kama hayo mfalme naye atasimuliwa, kwa hiyo njoo sasa, tupige shauri pamoja!

8Kisha nikatuma kwake kwamba: Mambo kama hayo, unayoyasema wewe, hayakufanyika, ila wewe unayatunga mwenyewe moyoni mwako.

9Kwani wao wote walitaka kutuogopesha tu kwa kwamba: Hivyo mikono yao italegea, isifanye kazi, jengo hilo lisimalizike. Sasa wewe Mungu, ishupaze mikono yetu!

10Mimi nikaenda kuingia nyumbani mwa Semaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, naye alikuwa amefungiwa; akaniambia: Na tukutane Nyumbani mwa Mungu, katikati ya Jumba hilo, tuifunge milango ya Jumba hilo, kwani wako wanaokuja kukuua, nao watakuja usiku huu, wakuue.

11Nikamjibu: Mtu kama mimi anawezaje kutoroka? Tena mtu kama mimi akiingia humo Jumbani atawezaje kupona? Sitakuja.

12Nalikuwa nimetambua, nikaona, ya kuwa siye Mungu aliyemtuma, aniambie huo ufumbuaji, ila Tobia na Sanibalati walikuwa wamempenyezea mali.

13Naye alipenyezewa mali, kusudi niingiwe na woga, niyafanye hayo ya kumkosea Mungu, wapate kulitokeza jina langu kuwa baya, wanitukane.[#4 Mose 18:7.]

14Mungu wangu, yakumbuke hayo matendo ya Tobia na ya Sanibalati! Mkumbuke naye mfumbuaji mke Noadia na wale wafumbuaji wengine waliotaka kuniogopesha![#Neh. 4:4-5.]

15Boma likamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli kwa siku hamsini na mbili.

16Adui zetu wote walipoyasikia haya, wakaogopa wao wamizimu wote waliokaa na kutuzunguka, wakazimia kabisa machoni pao kwa kujua, ya kuwa jengo hilo limefanywa kwa nguvu zitokazo kwake Mungu.

17Tena katika siku hizo, walikuwako wakuu wa miji ya Wayuda waliompelekea Tobia barua nyingi, nazo za Tobia zikafika kwao.

18Kwani katika nchi ya Yuda walikuwako wengi waliomwapia kumsaidia, kwani alikuwa mkwewe Sekania, mwana wa Ara; naye mwanawe Yohana alimwoa binti Mesulamu, mwana wa Berekia.

19Mimi nami wakanisimulia mambo yake mema, nayo niliyoyasema wakamtolea. Hata Tobia mwenyewe akatuma kwangu barua za kuniogopesha.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania