The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Waagize wana wa Isiraeli, watoe makambini wote walio wenye ukoma nao wote walio wenye kisonono nao wote waliojipatia uchafu kwa kugusa mfu.
3Sharti mwatoe, kama ni mume au kama ni mke, na kuwatuma kwenda nje ya makambi, wasiyachafue makambi, mimi ninamokaa katikati yao.[#4 Mose 12:14; 35:34.]
4Wana wa Isiraeli wakayafanya na kuwatuma kwenda nje ya makambi; kama Bwana alivyomwambia Mose, ndivyo, wana wa Isiraeli walivyoyafanya.
5Bwana akamwambia Mose kwamba:
6Waambie wana wa Isiraeli: Mtu mume au mke akifanya kosa lo lote la kimtu na kumvunjia Bwana maagano, mtu huyo atakuwa amekora manza.[#3 Mose 6:2-7.]
7Hao sharti wayaungame makosa yao, waliyoyafanya, kisha wazilipe manza zao, walizozikora, na kumrudishia mwenyewe, waliyemkosea, mali zake sawasawa na kuongeza fungu la tano.
8Kama mtu huyo hakuacha ndugu anayepasa kupewa hayo malipo ya manza, sharti Bwana apewe hayo malipo ya manza, yawe yake mtambikaji, wakiisha kutoa humo dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya upozi ya kumpatia upozi.
9Navyo vipaji vyote vya tambiko, wana wa Isiraeli watakavyovitoa kuwa vitakatifu vya kumnyanyulia Bwana, na wampelekee mtambikaji, navyo vitakuwa vyake.[#4 Mose 18:8.]
10Vipaji vyo vyote, mtu atakavyovitoa kuwa vitakatifu, vitakuwa vyake mtambikaji, navyo vyote, mtu atakavyompa mtambikaji, vitakuwa vyake.
11Bwana akamwambia Mose kwamba:
12Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Kama mke wa mtu anakosa na kumvunjia mumewe maagano yake,
13mtu akilala naye kwa ugoni, vikafichika machoni pa mumewe, asijulikane, ya kuwa amejichafua, kwa kuwa hakuwako shahidi, wala hakufumaniwa,
14lakini wivu ukiwaka moto rohoni mwake mumee, amwonee mkewe wivu kwa kwamba amejichafua, au pengine wivu ukiwaka moto rohoni mwake mumewe, amwonee mkewe wivu, naye haujichafua,
15basi, vikiwa hivyo sharti mume ampeleke mkewe kwa mtambikaji pamoja na kumpelekea toleo lake, vibaba viwili vya unga wa mawele, lakini asiumiminie mafuta, wala asiweke uvumba juu yake, kwani ni kilaji cha tambiko cha wivu, tena ni kilaji cha tambiko cha ukumbusho cha kukumbushia manza, alizozikora.
16Naye mtambikaji na ampeleke huyo mwanamke, amsimamishe mbele yake Bwana,
17kisha mtambikaji achote maji matakatifu kwa chombo cha udongo, kisha achote hata vumbi kidogo lililoko chini Kaoni, alitie katika hayo maji.[#2 Mose 30:18.]
18Mtambikaji akiisha kumsimamisha huyo mwanamke mbele ya Bwana na kuzifungua nywele za kichwani pake, na ampe mkononi mwake hicho kilaji cha tambiko cha ukumbusho, nacho ni kilaji cha tambiko cha wivu, lakini yale maji machungu yenye maapizo mtambikaji sharti ayashike mkononi mwake.
19Kisha mtambikaji na amwapishe na kumwambia huyo mwanamke: Kama mtu hakulala kwako, nawe hukukosa na kujichafua ukimtumia mwingine kuwa kama mumeo, hutapatwa na apizo lo lote la haya maji machungu yenye maapizo.
20Lakini kama umekosa na kujichafua ukimtumia mwingine kuwa kama mumeo, mtu ye yote akilala kwako kwa ugoni asiye mumeo, basi, yatakupata.
21Kisha mtambikaji na amwapishe huyo mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, mtambikaji akimwambia huyo mwanamke: Bwana na akuweke kuwa kielekezo cha kuapizwa katikati yao walio ukoo wako akivipoozesha viuno vyako pamoja na kulivimbisha tumbo lako!
22Nayo maji haya yenye maapizo na yaingie mwilini mwako, yalivimbishe tumbo lako pamoja na kuvipoozesha viuno vyako! Naye huyo mwanamke sharti aitikie na kusema: Amin. Amin.
23Kisha mtambikaji na ayaandike haya maapizo chuoni na kuyafuta kwa yale maji machungu.
24Kisha na amnyweshe huyo mwanamke hayo maji machungu yenye maapizo, yamwingie.
25Kisha mtambikaji na akichukue kilaji cha tambiko cha wivu mkononi mwa mwanamke, akipitishe motoni mbele ya Bwana na kumtolea mezani pa kutambikia.
26Hapo mtambikaji na achukue gao moja la kilaji cha tambiko kilicho cha ukumbusho wake mwanamke, akichome moto mezani pa kutambikia, kisha amnyweshe mwanamke yale maji.
27Akiisha kumnywesha hayo maji, naye akiwa amejichafua na kumvunjia mumewe maagano yake, basi, hayo maji machungu yenye maapizo yatakapomwingia yatalivimbisha tumbo lake pamoja na kuvipoozesha viuno vyake; ndivyo, huyu mwanamke atakavyokuwa ameapizwa kwao walio ukoo wake.
28Lakini kama mwanamke huyu hakujichafua, akiwa ametakata, hatapatwa na jambo lo lote, ila atazaa watoto tena.
29Haya ndiyo maonyo yao wenye wivu, mwanamke akiwa amekosa na kujipatia uchafu kwa kutumia mwingine kuwa kama mumewe,
30au wivu ukiwaka moto rohoni mwa mtu, amwonee mkewe wivu, amsimamishe huyo mwanamke mbele ya Bwana, mtambikaji amfanyizie mambo yote ya haya maonyo.
31Hapo mumewe atakuwa hana manza zo zote tena, lakini mwanamke aliye hivyo hana budi kujitwika manza, alizozikora.