Mifano 1

Mifano 1

Kualika watu, waje kuerevuka.

1Waje kujua werevu wa kweli na kuonyeka,[#1 Fal. 4:29-32.]

2wajue kutambua maneno ya utambuzi,

3waje kuonyeka, wapate akili,

tena wapate wongofu na mashauri mema yaongokayo,

4waerevushe wajinga,

nao wavulana wawajulishe kuwaza mambo mioyoni!

5Naye mwerevu wa kweli ayasikie, auongeze ujuzi wake,

naye mtambuzi ajipatie wongozi mwema.

6atambue mifano na vitendawili,

hata maneno ya werevu wa kweli na mafumbo yao!

7Kumcha Bwana ndio mwanzo wa ujuzi,

lakini wajinga huubeza werevu wa kweli kwa kukataa kuonyeka.

8Mwanangu, sikia, baba yako akikuchapa,

usiyabeue maonyo ya mama yako!

9Kwani hayo ni kilemba kipendezacho kichwani pako

na mkufu wa pambo shingoni pako.

Kuonya watu, wasidanganyike.

10Mwanangu wakosaji wakikubembeleza, usiwaitikie!

11Wakikuambia: Twende pamoja, tuvizie kumwaga damu,

tena tumwotee bure asiyekosa,

12kama kuzimu tuwameze, wakingali wa hai,

wao wamchao Mungu wawe kama wengine washukao shimoni,

13tuzipate mali zao zote zenye kima,

tuzijaze nyumba zetu mateka,

14kisha nawe utapiga kura pamoja nasi,

sisi sote pia tutakuwa bia moja tu:

15mwanangu, hao usishike njia moja nao,

uzuie mguu wako, usikanyage mikondo yao!

16Kwani miguu yao hukimbilia mabaya,

hupiga mbio kuja kumwaga damu.

17Ni bure, wavu ukiwa umetandwa

machoni pao wote walio wenye mabawa.

18Hivyo wao huvizia kumwaga damu zao wenyewe

na kuziotea roho zao wenyewe.

19Ndivyo, zilivyo njia zao wote wanaotamani mali tu,

maana giza huzichukua roho zao wenyewe.

Mapatilizo yao wasiosikia.

20Werevu wa kweli hupiga mbiu barabarani,

huipaza sauti yake viwanjani;

21hutangaza pembeni penye njia pasipo na makelele mengi,

napo pa kuingia malangoni, namo mjini husema maneno yake:

22Mpaka lini mtayapenda mapumbavu, ninyi wapumbavu?

nanyi wafyozaji mtapendezwa na ufyozaji mpaka lini?

nanyi wajinga mtauchukia ujuzi mpaka lini?

23Geukeni kwa kuonywa na mimi!

Mtaniona, nikiwamwagia roho yangu,

nikiwajulisha maneno yangu.

24Kwa kuwa niliwaita, mkakataa kunisikia,

kwa kuwa niliukunjua mkono wangu,

lakini hakuwako aliyeuangalia,

25mkayaacha mashauri yangu yote,

hamkutaka kuonywa na mimi:

26kwa hiyo mimi nami nitacheka, mkiangamia,

nitawasimanga, mastuko yatakapowajia;

27hayo mastuko yatawajia kama mvua yenye umeme,

nao mwangamizo utawatukia kama upepo wa kilazoni,

nayo masongano na mahangaiko yatawajia.

28Hapo ndipo, watakaponiita, lakini sitawaitikia,

watanitafuta kwa bidii tangu asubuhi, lakini hawataniona.

29Kwa kuwa waliuchukia ujuzi,

hawakutaka kumcha Bwana,

30wala hawakuyapenda mashauri yangu,

wakakataa po pote kuonywa na mimi,

31kwa hiyo watayala mazao ya njia zao,

wayashibe mashauri yao.

32Kwani kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua,

nako kujikalia tu kwao wapumbavu kutawaangamiza.

33Lakini atakayenisikia atakaa na kutulia,

atatengemana pasipo kuona kibaya kitakachomstusha.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania