Mifano 27

Mtu asijivune!

1Usijivunie siku ya kesho!

Kwani huyajui, hiyo siku utakayoyazaa.

2Mwingine na akusifu, kisiwe kinywa chako!

Mgeni akusifu, lakini isiwe midomo yako!

3Jiwe ni zito, nao mchanga ni mzigo,

lakini masikitiko ya mpumbavu ni mazito kuliko yote mawili.

4Makali huwaka moto, nayo machafuko hufurikia,

lakini awezaye kusimama penye wivu yuko nani?

5Kuonywa waziwazi ni kwema

kuliko kupendwa na mtu avifichaye.

6Vidonda, anavyokutia mpenzi wako, vina maana ya kweli,

lakini asiyekoma kukunonea ni mchukivu.

7Roho ya mtu ashibaye hubeza hata asali iliyo safi,

lakini roho ya mtu aliye na njaa huona nayo machungu kuwa matamu.

8Kama ndege aliyekimbia tunduni mwake

ndivyo, alivyo mtu aliyekimbia kwao.

9Mafuta na uvumba hufurahisha moyo, nao utamu wa mpenda mwenziwe,

huu ndio unaotoka katika mashauri mema ya roho.

10Usimwache mwenzio wala mwenziwe baba yako!

Wala mwake ndugu yako usimwingie siku, ulipopatwa na mabaya!

Mtu akaaye karibu na mwema kuliko ndugu alioko mbali.

11Mwanangu, erevuka kweli, uufurahishe moyo wangu,

nipate kumjibu mtu, akinitukana!

12Mwerevu wa kweli akiona mabaya kujificha,

lakini wajinga hupita tu, wakapatwa nayo.

13Zichukue nguo zake yeye aliyejitoa kuwa dhamana ya mwingine,

kwa ajili ya mwanamke mgeni mnyang'anye mali zake!

14Mtu akimbariki mwenziwe kwa sauti kuu asubuhi na mapema

huwaziwa, ya kuwa amemwapiza.

15Maji yasiyokoma kuchuruzika toka mchirizini siku ya mvua nyingi

na mwanamke mgomvi ni sawasawa;

16awezaye kumzuia aweza kuuzuia nao upepo,

mkono wake wa kuume huweza kushika nayo mafuta yauingiayo.

17Chuma hunoa chuma;

ndivyo, mtu na uso wa mwenziwe wanavyonoana.

18Alindaye mkuyu hula kuyu zake,

naye awaangaliaye mabwana zake hupata macheo.

19Kama majini uso unayvoelekea uso,

ndivyo, moyo wa mtu unavyouelekea moyo wa mwenziwe.

20Kuzimu nako, watu wanakopotelea, hakushibi,

vivyo hivyo nayo macho ya watu hayashibi.

21Chungu cha kuyeyushia hujaribu fedha, nayo tanuru hujaribu dhahabu,

lakini mtu hujaribiwa nayo, vinywa vya watu vinayomsifia.

22Ijapo umtwange mjinga kwa mchi katika kinu pamoja na mchele,

ujinga wake hautamtoka.

23Sharti ujue vema, jinsi makundi yako yalivyo,

kauelekeze moyo wako kuwaangalia nao ng'ombe!

24Kwani kilimbiko hicho nacho sicho cha kale na kale,

au kiko kilemba cha kifalme kikaliachao vizazi na vizazi?

25Majani makavu yakiisha kuondolewa, hutokea mabichi,

nako milimani hukusanywa majani mazuri ya kula.

26Wana kondoo hukupatia mavazi yako,

nayo madume ni malipo ya kununua shamba.

27Tena yako maziwa ya mbuzi yatoshayo kukulisha wewe

na kuwalisha nao waliomo nyumbani mwako,

hata kuwa posho ya watumishi wako wa kike.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania