Mashangilio 144

Mashangilio 144

Kumtukuza na kumwomba Mungu.

1Na atukuzwe Bwana aliye mwamba wangu! Ndiye aliyeifundisha mikono yangu kupiga vita, ijue hata kupiga konde kwenye mapigano.[#Sh. 18:35.]

2Ndiye aniendeaye kwa upole, ni ngome yangu na boma langu. Kwa kuwa ngao yangu na kimbilio langu ndiye aniponyaye, yeye ndiye awashurutishaye walio ukoo wangu, wanitii.[#Sh. 18:3.]

3Bwana, mtu ndio nini, ukimjua? Mwana wa mtu naye, usipomsahau?[#Sh. 8:5.]

4Mtu hufanana kuwa kama mvuke, siku zake hupita kama kivuli.[#Iy. 14:2.]

5Bwana, ziinamishe mbingu zako, utelemke! Iguse milima, itoke moshi![#Sh. 18:10; 104:32.]

6Mulikisha umeme, uwatapanye! Ipige mishale yako, uwastushe!

7Utume mkono wako toka juu, uniopoe! Kwenye maji mengi uniponye! Nitoe mikononi mwao walio wageni tu!

8Maana vinywa vyao husema maneno ya bure, mikono yao ya kuume ni yenye uwongo.[#Sh. 144:11; Ez. 17:18.]

9Mungu, nitakuimbia wimbo mpya pamoja na kukupigia pango lenye nyuzi kumi.[#Sh. 33:2-3.]

10Yeye ndiye awapatiaye wokovu nao wafalme, naye mtumishi wake Dawidi humwopoa, upanga mbaya usimpige.

11Niopoe na kuniponya mikononi mwao walio wageni tu! Maana vinywa vyao husema maneno ya bure, mikono yao ya kuume ni yenye uwongo.[#Sh. 144:8.]

12Wana wetu wa kiume katika ujana wao tunawaombea, wakue kama miti ya kupandwa iliyotunzwa vizuri! Nao wana wetu wa kike na wawe kama nguzo zilizochorwa vizuri kuwa mapambo yao majumba matukufu.[#Sh. 128:3.]

13Vichanja vyetu na viwe vimejaa, vipate kutoa vilaji viwavyo vyote! Kondoo wetu na wawe wengi sana wakizaa maelfu na maelfu mashambani kwetu!

14Ng'ombe wetu na wawe wenye mimba, wasipatwe na kidei wala na mengine yawamalizayo, pasiwe na vilio nyuani petu!

15Wenye shangwe ni ukoo wa watu wayapatayo yayo hayo. Wenye shangwe ni ukoo wa watu, Bwana akiwa Mungu wao.[#5 Mose 33:29.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania