The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika siku zile, waamuzi walipoamua, palikuwa na njaa katika nchi hiyo. Ndipo, mtu alipoondoka Beti-Lehemu wa Yuda kwenda kukaa ugenini katika mbuga za Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili wa kiume.
2Jina lake huyu mtu alikuwa Elimeleki, nalo jina lake mkewe alikuwa Naomi, nayo majina ya wanawe wa kiume walikuwa Maloni na Kilioni, ni Waefurati wa Beti-Lehemu wa Yuda. Walipofika kwenye mbuga za Moabu wakakaa huko.
3Kisha Elimeleki, mumewe Naomi, akafa, akaachwa yeye na wanawe wawili.
4Nao wakajichukulia wanawake wa Kimoabu, mmoja jina lake Orpa, wa pili jina lake Ruti, wakakaa huko kama miaka kumi.
5Ndipo, wote wawili Maloni na Kilioni walipokufa, yule mwanamke akasalia yeye tu kwa kufiwa na wanawe wawili na mumewe.
6Kisha akaondoka yeye na wakwewe, atoke kwenye mbuga za Moabu kurudi kwao, kwani alisikia kule kwenye mbuga za Moabu, ya kuwa Bwana amewakagua walio ukoo wake na kuwapa vyakula.
7Akatoka mahali hapo, alipokuwa, pamoja na wakwewe wawili, wakashika njia kwenda kurudi katika nchi ya Yuda.
8Naomi akawaambia wakwewe wawili: Nendeni kurudi kila mtu nyumbani mwa mama yake! Bwana awafanyizie mema, kama mlivyowafanyizia mema wanangu waliokufa, hata mimi.
9Bwana awape, mpate kutulia kila mmoja nyumbani mwa mumewe. Alipowanonea, wakazipaza sauti zao, wakalia machozi.[#Ruti 3:1.]
10Wakamwambia: Tutarudi pamoja na wewe kwa watu wa ukoo wako.
11Naomi akawaambia: Rudini, wanangu! Sababu gani mnataka kwenda na mimi? Niko na wana bado tumboni mwangu, wawe waume wenu?
12Rudini, wanangu, kwenda zenu! Kwani mimi ni mzee, siwezi kupata tena mume. Ijapo niseme: Niko na kingojeo, usiku huu wa leo nipate mume, nizae wana wa kiume,
13je? Ninyi mngeweza kuvumilia, mpaka wakiwa wakubwa? Mngeweza kufungiwa, kwa kuwa hamna waume? Msifanye hivyo, wanangu! Kwani naona uchungu mwingi sana kwa ajili yenu, kwa kuwa mkono wa Bwana umenitokea.[#Iy. 19:21.]
14Ndipo, walipozipaza sauti zao tena, wakalia machozi. Kisha Orpa akamnonea mkwewe, lakini Ruti akaandamana naye.
15Akamwambia: Tazama, dada yako amerudi kwao na kwa Mungu wao; rudi nawe kumfuata dada yako!
16Ruti akamwambia: Usinihimize kukuacha na kwenda kwetu, nisikufuate! Kwani uendako, ndiko, nitakakokwenda nami; ukaako, ndiko, nitakakokaa nami. Ukoo wako ni ukoo wangu, Mungu wako ni Mungu wangu.[#2 Sam. 15:21.]
17Utakakokufa, ndiko, nitakakofia, tena ndiko, ninakotaka kuzikwa; Bwana na anifanyizie hivi na hivi na kuendelea hivyo, kwani ni kufa tu kutakako tutenga mimi na wewe.
18Alipomwona, ya kuwa amejishupaza kwenda naye, akaacha kusema naye.
19Wakaenda wao wawili, mpaka wakifika Beti-Lehemu. Ikawa, walipofika Beti-Lehemu, mji wote ukavurugika kwa ajili yao wakisema: Kumbe huyu siye Naomi?
20Akawaambia: Msiniite Naomi (Apendezaye), ila mniite Mara (Mwenye uchungu). Kwani Mwenyezi amenifanyizia yenye uchungu sana.[#2 Mose 15:23.]
21Nilipokwenda nilikuwa mwenye mali, lakini Bwana amenirudisha mikono mitupu. Mbona mnaniita Naomi? Naye Bwana ametoa ushuhuda wa kunishinda, yeye Mwenyezi ameniumiza vibaya.
22Ndivyo, Naomi alivyorudi pamoja na Ruti, mkwewe wa Kimoabu, alipotoka kwenye mbuga za Moabu kurudi kwao, nao wakafika Beti-Lehemu, mavuno ya mawele yalipoanza.