1 Wamakabayo 13

1 Wamakabayo 13

SIMONI KUHANI MKUU NA MTAWALA WA WAYAHUDI

Simoni kuwa kiongozi

1Simoni akasikia kama Trifoni alikuwa amepanga jeshi kubwa kuishambulia nchi ya Uyahudi na kuiharibu kabisa.

2Aliona jinsi watu walivyokuwa wakitetemeka kwa hofu. Akapanda kwenda Yerusalemu akawakusanya watu

3akawatia moyo, akiwaambia; Ninyi wenyewe mnajua kazi tulizozifanya kwa ajili ya sheria na patakatifu, mimi na ndugu zangu na wote wa nyumba ya baba yangu; tena mnajua vita na shida zilizotupata.

4Kwa sababu hiyo ndugu zangu wote wamekufa kwa ajili ya Israeli, nami peke yangu nimesalia.

5Basi, isiwe kwangu kutaka kujiokoa nafsi yangu wakati wa taabu, maana mimi si bora kuliko ndugu zangu.

6Hakika nitalipiza kisasi kwa ajili ya taifa langu na patakatifu na wake zetu na watoto wetu, kwa kuwa mataifa yote wamekusanyika kwa uadui ili kutuharibu.

7Mara watu walipoyasikia maneno hayo roho zao zilifufuka.

8Wakaitika kwa sauti kubwa, wakisema, Wewe u kiongozi wetu, mahali pa Yuda na Yonathani, ndugu zako.

9Piga vita vyetu, na lolote utakalotuamuru tutalifanya.

10Akawachagua watu wote wa vita, akafanya haraka kuzimaliza kuta za Yerusalemu na kuuzungusha maboma.

11Akamtuma Yonathani mwana wa Absalomu pamoja na jeshi kubwa kidogo, aende Yafa; naye aliwafukuza waliokuwamo akaikalia.

Hila na usaliti wa Trifoni

12Trifoni akaondoka Tolemaisi na jeshi kubwa kuingia Uyahudi, na Yonathani alikuwa pamoja naye, mfungwa.

13Simoni akapiga kambi Adida kuuelekea uwanda.

14Trifoni aliposikia ya kuwa Simoni ameinuka mahali pa nduguye Yonathani, tena yu tayari kwa vita, alituma wajumbe kwake kusema.

15Tumemshika ndugu yako Yonathani kwa sababu ya fedha anayodaiwa na hazina ya mfalme kwa ajili ya zile kazi alizopewa.

16Basi, lete talanta mia moja za fedha, na wana wake wawili wawe wadhamini, yaani kumdhaminia asitufanyie matata atakapofunguliwa, nasi tutamweka huru.

17Simoni alijua ya kuwa wanasema kwa hila, lakini alipeleka ile fedha na wale watoto, isiwe labda watu watamchukia na kusema,

18Hakumpelekea fedha na watoto, ndiyo sababu ameuawa.

19Basi, aliwapeleka wale watoto na zile talanta mia, lakini Trifoni alidanganya tu, wala hakumfungua Yonathani.

20Baada ya hayo, Trifoni alikuja kuishambulia nchi na kuiharibu, akizunguka kwa njia ya Adora. Simoni na jeshi lake walifuatana naye kila mahali, wakiambiana naye kandokando.

21Askari wa ngomeni walipeleka wajumbe kwa Trifoni kumhimiza aje kwao kwa njia ya nyika na kuwaletea chakula.

22Trifoni aliweka tayari wapanda farasi wake wote kuwaendea, lakini usiku ule kulianguka theluji nyingi sana, kwa hiyo hakuweza kwenda. Basi aliondoka akaenda Gileadi.

23Alipokaribia Baskama alimwua Yonathani akamzika pale.

24Kisha akageuka akairejea nchi yake.

Kaburi la Yonathani

25Simoni akapeleka watu kuitwaa mifupa ya nduguye Yonathani, akamzika Modini, mji wa baba zake.

26Kukawa kilio kikuu katika Israeli yote, wakamwombolezea siku nyingi.

27Simoni akajenga kaburi la baba yake na ndugu zake kwa jiwe lililosuguliwa vizuri nyuma na mbele, akiliinua juu sana lipate kuonekana.

28Akasimamisha piramidi saba za mawe kwa mfulizo kuwa ukumbusho wa baba yake na mama yake na ndugu zake wanne.

29Akafanya mitambo ya kusimamishia nguzo kubwa kuyazunguka; na juu ya nguzo alitia silaha za kila namna kuwa ukumbusho wa daima, na kando ya silaha alichora merikebu za kuonekana na wote wasafirio baharini.

30Kaburi hili alilolijenga Modini lipo hata leo.

Yuda kapata kujitegemea

31Trifoni akamfanyia hila yule kijana, mfalme Antioko, akamwua,

32akajifanya mfalme mahali pake akaivaa taji la Asia, ikawa baa kubwa kwa nchi.

33Simoni akazijenga ngome za Uyahudi na malango na mapingo, akaweka akiba ya chakula ngomeni.

34Simoni akachagua watu, akawapeleka kwa mfalme Demetrio kuomba nchi iachiliwe, maana kazi ya Trifoni ilikuwa kuteka nyara tu.

35Mfalme Demetrio akamrudishia jibu kwa maneno haya akimwandikia hivi:

36Mfalme Demetrio kwa kuhani mkuu, Simoni, rafiki wa wafalme, na kwa wazee na taifa la Wayahudi, salamu.

37Tumeipokea taji la dhahabu mliyotuletea, na tawi la mitende; nasi tu tayari kufanya amani ya daima nanyi, na kuwaandikia watumishi wetu wawaachilieni.

38Mambo yote tuliyowathibitishia yamethibitika. Ngome mlizozijenga ziwe zenu.

39Na kwa habari za ukosefu wowote na makosa yoyote mliyoyafanya, twayasamehe, pamoja na yale malipo ya mfalme mliyodaiwa nasi. Na kama ikiwapo kodi nyingine itozwayo Yerusalemu, isitozwe tena.

40Wakiwapo watu kwenu wanaostahili kuandikwa katika wafuasi wetu, na waandikwe.

41Basi, katika mwaka wa mia moja na sabini nira ya mataifa iliondolewa katika Israeli.

42Watu wakaanza kuandika katika taarifa zao, Katika mwaka wa kwanza wa Simoni, kuhani mkuu maarufu, jemadari na kiongozi wa Israeli.

Simoni ateka Gazara

43Siku zile alipiga kambi Gazara, akapanga jeshi lake kuizunguka; akaunda mtambo wa kuhusuria, akausongeza karibu na mji, akapiga mnara akautwaa.[#2 Mak 10:32-38]

44Askari waliokuwamo katika ule mtambo wakaruka, wakaingia katika mji, kukawa ghasia kubwa mjini.

45Wenyeji na wake zao na watoto wao wakapanda juu ya ukuta, wakalia kwa sauti kuu, wakimwomba Simoni afanye yamini nao.

46Wakasema, Usitutendee kwa kadiri ya ubaya wetu ila kwa kadiri ya rehema zako.

47Basi, Simoni alipatanishwa nao. Lakini aliwatoa katika mji, akazitakasa nyumba zenye sanamu za miungu, akaingia mjini kwa nyimbo na shukrani.

48Akautoa uchafu wote katika mji, akaweka humo watu wenye kuishika sheria, akaufanya imara kuliko ulivyokuwa kwanza, akajijengea nyumba yake.

Simoni apata ngome ya Yerusalemu

49Huko nyuma, watu katika ngome ya Yerusalemu walizuiwa wasitoke kwenda katika nchi kununua na kuuza. Chakula kilikuwa shida, na wengi wao walikufa kwa njaa.

50Wakamlilia Simoni awape yamini, akawapa; akawatoa humo akaitakasa ngome na unajisi wake.

51Akaingia siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa pili, mwaka wa mia moja sabini na moja, kwa shukrani, na kwa matawi ya mitende, na vinubi na matari na zeze, na kwa zaburi na nyimbo, kwa sababu adui mkubwa ameondolewa katika Israeli.

52Akaagiza siku hiyo iadhimishwe kwa furaha kila mwaka. Mlima wa hekalu kando ya ngome aliuimarisha zaidi, akakaa pale pamoja na watu wake.

53Simoni aliona ya kuwa mwanawe Yohana yu mtu hodari, akamfanya jemadari wa jeshi lake lote. Akakaa Gazara.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya