1 Wamakabayo 4

1 Wamakabayo 4

Vita huko Emao

1Gorgia akatwaa askari elfu tano na wapanda farasi wateule elfu moja, jeshi lake likaondoka usiku

2ili kulishambulia jeshi la Wayahudi na kuwapiga ghafla. Watu wa ngomeni walikuwa viongozi wake.

3Yuda akapata habari, akaondoka, yeye na watu wake hodari, ili alipige jeshi la mfalme lililokuwapo Emao,

4wakati vikosi vingine vimetawanyika.

5Gorgia akaingia katika kambi ya Yuda usiku, asione mtu. Akaenda kuwatafuta milimani, akisema. Watu hawa wanatukimbia.

6Hata kulipopambazuka, Yuda alitokea uwandani na watu elfu tatu, ingawa hawakuwa na silaha na panga kama walivyotaka.

7Wakaiona kambi ya mataifa imara, yenye maboma ya nguvu, na wapanda farasi hodari sana kwa vita wameizunguka.

8Yuda akawaambia wafuasi wake, Msiogope wingi wao, wala msihofu mashambulio yao.

9Kumbukeni jinsi baba zetu walivyookolewa katika Bahari ya Shamu, Farao alipowafuatia na jeshi kubwa.

10Basi, tuzililie mbingu, tuone kama Yeye ataturehemu na kulikumbuka agano lake na baba zetu na kuliharibu jeshi hili usoni petu leo;

11hivyo mataifa yote watajua ya kuwa yupo mmoja anayemkomboa Israeli na kumwokoa.

12Wageni wakainua macho yao wakawaona wanawajia,

13wakatoka kambini kupigana. Nao waliokuwa na Yuda wakapiga tarumbeta,

14na kujitia vitani, mataifa wakashindwa kabisa, wakakimbia uwandani,

15hata wale waliokuwa nyuma wakauawa kwa upanga. Wakafuatia hata Gazara na nyanda za Idumia za Azota na Yamnia, wakaanguka watu wapatao elfu tatu.

16Yuda na kikosi chake waliporudi baada ya kuwafuatia

17aliwaambia watu wake, Msifanye pupa ya mateka, maana kuna mapigano mbele yetu.

18Gorgia na watu wake wako karibu nasi milimani. Basi simameni sasa kupambana na adui na kupigana nao, baadaye tekeni nyara bila hofu.

19Yuda hakudiriki kumaliza maneno yake ila kikosi chao kilionekana wakivizia toka milimani.

20Wakaona jeshi lao limekimbiwa na kambi imeteketezwa, maana moshi uliopanda juu uliwafahamisha yaliyotendeka.

21Nao walipoona hayo waliogopa sana, hata walipoliona jeshi la Yuda uwandani, limepangwa tayari kwa vita,

22walikimbia wote kwenye nchi ya Wafilisti.

23Basi, Yuda alirudi kuiteka kambi, wakapata dhahabu nyingi na fedha, na nguo za samawi na urujuani, na mali nyingi.

24Wakarudi kwao wakiimba wimbo na kuzitolea mbingu shukrani “kwa kuwa yu mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.”

25Israeli alipata wokovu mkuu siku ile.

Juhudi za kwanza za Lisia

26Wale wageni waliookoka walimwendea Lisia wakamsimulia yote yaliyotokea,

27naye alipoyasikia alifadhaika na kuvunjika moyo, kwa kuwa yale aliyoyataka watendewe Waisraeli hayakutendeka, wala mambo aliyoamriwa na mfalme hayakutimizwa.

28Basi, katika mwaka uliofuata, alikusanya askari wateule elfu sitini na wapanda farasi elfu tano kupigana nao.

29Wakaja Idumia, wakapiga kambi Bethsura. Yuda akaenda kukutana nao na watu elfu kumi.

30Akaiona nguvu ya jeshi lao, akasali, akisema: Umehimidiwa, Ee Mwokozi wa Israeli: Uliyeyazuia mashambulio ya yule shujaa kwa mikono wa mtumishi wako Daudi; ukalitia jeshi la Wafilisti katika mkono ya Yonathani, mwana wa Sauli, na ya mchukua silaha zake.[#1 Sam 17:41-54; 14:1-23]

31Ulifunge jeshi hili vile vile katika mikono ya watu wako Israeli, hata adui zetu walionee haya jeshi lao na wapanda farasi wao.

32Uwatie woga na kuuyeyusha ujasiri wa nguvu zao; wayatetemekee maangamizo yao.

33Uwaangushe kwa upanga wa wale wakupendao, na wote walijuao jina lako wakusifu kwa nyimbo.

34Vita vikaanza; wakaanguka wa jeshi la Lisia watu wapatao elfu tano, wakakimbia mbele yao.

35Lisia alipoona wanavyozidi kushindwa, na ujasiri wa Yuda na watu wake unavyozidi, na jinsi walivyokuwa tayari kuishi au kufa kwa ushujaa, aliondoka akaenda Antiokia. Huko akaajiri askari wa mshahara, ili afike tena Uyahudi na jeshi kubwa zaidi.

Kutakasa na kuweka wakfu hekalu

36Yuda na ndugu zake wakasema, Sasa adui zetu wamevunjwa nguvu, basi tupande tukapatakase mahali patakatifu na kupatabaruku.

37Jeshi lote likakusanyika likapanda juu ya mlima Sayuni.

38Wakapaona patakatifu pameachwa ukiwa, na madhabahu yake imetiwa unajisi; milango imechomwa moto, na majani yanaota katika nyua zake kama katika msitu au juu ya mlima, na vyumba vya makuhani vimebomolewa.

39Wakazirarua nguo zao na kulia sana, wakajitia majivu kichwani na kuanguka kifudifudi.

40Wakazipiga tarumbeta za kanuni na kuzililia mbingu.

41Yuda akaweka watu fulani kupigana na wale wa ngomeni, hata atakapokwisha kupatakasa patakatifu,

42Akachagua makuhani wasio na waa, ambao furaha yao ilikuwa katika sheria,

43wakapasafisha patakatifu wakiyatoa mawe yenye unajisi na kuyapeleka nje katika mahali pachafu.

44Wakafanya shauri juu ya madhabahu ya sadaka za kuteketezwa ambayo ilikuwa imetiwa unajisi.

45Wakapata shauri la kufaa, yaani kuibomoa, isije ikawa lawama kwao kwa kuwa imetiwa unajisi na mataifa. Basi, waliibomoa madhabahu,

46wakayaweka mawe yake mahali pa kufaa katika mlima wa hekalu hata atakapokuja nabii wa kuyakatia shauri.

47Wakatwaa mawe yasiyochongwa, kama ilivyoamriwa katika sheria, wakafanya madhabahu mpya, mfano wa ile ya kwanza.[#Kut 20:25; Kum 27:5-6]

48Wakapajenga patakatifu, na sehemu za ndani za nyumba, na kuzitakasa nyua zake.

49Wakafanya vyombo vitakatifu vipya; wakatia kinara, na madhabahu ya kufukizia uvumba, na meza katika hekalu.

50Wakafukiza uvumba juu ya madhabahu, wakaziwasha taa za kinara ili ziangaze hekaluni.

51Wakaweka mikate mezani, na kutungika mapazia, wakazimaliza kazi zote walizoziazimia.

52Wakaondoka mapema siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, yaani Kislevu, mwaka mia moja arubaini na nane,[#1 Mak 1:54]

53wakatoa dhabihu, kama ilivyoamriwa katika sheria, juu ya madhabahu mpya ya sadaka za kuteketezwa waliyokuwa wameifanya.

54Wakati ule ule na siku ile ile iliyotiwa unajisi na mataifa, siku ile iliwekwa wakfu tena kwa nyimbo na vinubi na vinanda na matari.

55Watu wote wakaanguka kifudifudi wakipaza sifa kwa mbingu, kwake aliyewapa ufanisi.

56Wakaiadhimisha sikukuu ya kuitabaruku madhabahu muda wa siku nane, wakileta sadaka za kuteketezwa kwa furaha na kutoa dhabihu ya wokovu na shukrani.

57Pia, waliupamba ukuta wa mbele wa hekalu kwa taji za dhahabu na vigao; wakaweka wakfu malango na vyumba vya makuhani na kuvitia milango.

58Kulikuwa na furaha kubwa kwa watu, na aibu iliyoletwa na mataifa iliondolewa.

59Yuda na ndugu zake, na jamii yote ya Israeli, walikata shauri ya kuwa siku za kuitabaruku madhabahu ziadhimishwe kwa furaha na shangwe kila mwaka kwa wakati wake, muda wa siku nane tangu siku ya ishirini na tano ya mwezi Kislevu.

60Wakati huo walijenga kuta ndefu na minara imara kuuzunguka mlima Sayuni, ili mataifa wasije tena wakawakanyaga kama walivyofanya zamani.

61Akaweka kikosi humo kuulinda. Wakaimarisha Bethsura pia, ili watu wawe na ngome kuelekea Idumia.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya