The chat will start when you send the first message.
1Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu[#1 Nya 6:27; Rut 1:2]
2naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto.
3Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea BWANA wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa BWANA, walikuwako huko.[#Kum 12:5; Yos 18:1; Amu 18:31; Zab 78:60; Yer 7:12-14]
4Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, wanaume kwa wanawake, sehemu zao;
5lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa BWANA alikuwa amemfunga tumbo.[#Mwa 30:2]
6Ila mwenzake humchokoza sana, ili kumwuudhi, kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo.
7Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula.[#Kut 23:14; Kum 16:16; Lk 2:41]
8Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwa nini huli? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?[#Rut 4:15]
9Ndipo Hana akainuka, walipokula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA.[#1 Sam 3:3]
10Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana.[#Ayu 7:11; 10:1; Hes 30:3; 2 Sam 17:8]
11Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utayaangalia mateso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikia kichwani kamwe.[#Hes 6:5; Mwa 28:20; Hes 21:2; 30:3-8; Amu 11:30; Mhu 5:4; Mwa 29:32; Kut 4:31; 2 Sam 16:12; Zab 25:18; Mwa 8:1; 30:22; Zab 132:1,2]
12Ikawa, hapo alipoendelea kuomba mbele za BWANA, Eli akamwangalia kinywa chake.
13Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa.
14Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hadi lini? Achilia mbali divai yako.
15Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za BWANA.[#Zab 62:8]
16Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa.[#2 Kor 6:15]
17Ndipo Eli akajibu, akasema, Nenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba.[#Amu 18:6; 1 Sam 25:35; Lk 7:50; 8:48; Zab 20:4,5]
18Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukuhuzunika tena.[#Mwa 33:15; Rut 2:13; Mhu 9:7; Yn 16:24]
19Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaomba mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka.[#Mwa 30:22]
20Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; akamwita Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.
21Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake.
22Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa kunyonya, hapo ndipo nitakapomleta, ili awepo mbele za BWANA, akae huko daima.[#Lk 2:22; 1 Sam 2:11; 3:1]
23Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hadi utakapomwachisha kunyonya; BWANA na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hadi akamwachisha kunyonya.[#Hes 30:7; 2 Sam 7:25]
24Naye alipomwachisha kunyonya, akamchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo.[#Kum 12:5; #1:24 Au, ng'ombe wa miaka mitatu.]
25Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli.
26Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba BWANA.
27Niliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba;[#Mt 7:7]
28kwa sababu hiyo mimi nami nimempa BWANA mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA. Naye akamwabudu BWANA huko.[#Mwa 24:26,52]