1 Timotheo 2

1 Timotheo 2

Maagizo kuhusu maombi

1Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;[#Flp 4:6]

2kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.

3Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;[#1 Tim 1:1; 4:10]

4ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.[#Eze 18:23; 2 Pet 3:9]

5Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu;[#Rum 3:29,30; Ebr 12:24]

6ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.[#Gal 1:4; 2:20; Tit 2:14]

7Nami kwa ajili ya huo niliwekwa niwe mhubiri na mtume, (nasema kweli, sisemi uongo), mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli.[#2 Tim 1:11; Gal 2:7,8]

8Basi, nataka wanaume waombe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

9Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;[#1 Pet 3:3-5]

10bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.[#1 Tim 5:10]

11Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.[#Efe 5:22]

12Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe msikivu.[#1 Kor 14:34; Mwa 3:16]

13Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.[#Mwa 1:27; 2:7,21-22; 1 Kor 11:8,9]

14Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.[#Mwa 3:1-6; 2 Kor 11:3]

15Lakini ataokolewa kwa kuzaa kwake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya