2 Mambo ya Nyakati 33

2 Mambo ya Nyakati 33

Kutawala kwa Manase

1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka hamsini na mitano.[#2 Fal 21:1]

2Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo yote ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.[#Law 18:24-30; Kum 18:9; 2 Fal 17:11,15; 2 Nya 28:3]

3Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopabomoa Hezekia babaye; akazisimamisha madhabahu za Mabaali, akafanya sanamu za Maashera, akaabudu jeshi lote la mbinguni, na kulitumikia.[#2 Fal 18:4; 2 Nya 30:14; 31:1; Kum 16:21; 4:19; 17:3; 2 Fal 23:5-11; Yer 8:2; Sef 1:5]

4Akajenga madhabahu katika nyumba ya BWANA, pale ndipo alipopanena BWANA, Katika Yerusalemu litakuwako jina langu milele.[#Kum 12:11; 1 Fal 8:29]

5Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika nyua mbili za nyumba ya BWANA.[#2 Nya 4:9]

6Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, na kumkasirisha.[#Law 18:21; Kum 18:10; 2 Nya 28:3; Eze 23:37; 2 Fal 21:6]

7Akaiweka sanamu ya kuchonga aliyoifanya, katika nyumba ya Mungu ambayo Mungu alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;[#2 Fal 21:7; Zab 132:14]

8wala sitawaondoshea miguu tena Israeli katika nchi niliyowaagizia baba zenu; wakiangalia tu kutenda yote niliyowaamuru, yaani, torati yote, na sheria, na maagizo, niliyowaamuru kwa mkono wa Musa.[#2 Sam 7:10]

9Basi Manase aliwapotosha Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, hata wakazidi kufanya mabaya kuliko mataifa, aliowaharibu BWANA mbele ya wana wa Israeli.

Manase atubu na kujirudi

10Naye BWANA akasema na Manase, na watu wake; wala wasiangalie.[#Neh 9:29; Yer 25:4]

11Kwa hiyo BWANA akaleta juu yao makamanda wa jeshi la mfalme wa Ashuru, waliomkamata Manase kwa minyororo, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli.[#Kum 28:36; Ayu 36:8; Zab 107:10,11]

12Hata alipokuwa katika taabu, akamsihi BWANA, Mungu wake, akajinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake.[#Kum 4:30,31; Zab 118:5; 120:1; Yer 31:18-20; Hos 5:15; Yon 2:2; Mik 6:9; Lk 15:16-18; Kut 10:3; 2 Nya 32:26; Lk 18:4; 1 Pet 5:6]

13Akamwomba; naye akamtakabali, akayasikia maombi yake; akamrudisha tena Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akajua ya kwamba BWANA ndiye Mungu.[#1 Nya 5:20; Ezr 8:23; Zab 142:1-7; Omb 3:55,56; Zab 9:16; Dan 4:25]

14Hata baada ya hayo akaujengea mji wa Daudi ukuta wa nje, upande wa magharibi wa Gihoni, bondeni, hata kufika maingilio ya Lango la Sameki; akauzungusha Ofeli, akauinua juu sana; akaweka makamanda wa jeshi katika miji yote ya Yuda yenye maboma.[#1 Fal 1:33; 2 Nya 27:3]

15Akaiondoa miungu migeni, na hiyo sanamu nyumbani mwa BWANA, na madhabahu zote alizozijenga katika mlima wa nyumba ya BWANA, na Yerusalemu, akazitupa nje ya mji.

16Akaijenga madhabahu ya BWANA, akatoa juu yake dhabihu za sadaka za amani, na za shukrani, akawaamuru Yuda wamtumikie BWANA, Mungu wa Israeli.[#Law 7:12]

17Lakini watu wakaendelea kutoa dhabihu katika mahali pa juu, ila wakamtolea BWANA, Mungu wao tu.[#1 Fal 22:43; 2 Fal 15:4; 2 Nya 15:17; 32:12]

Kufa kwa Manase

18Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na maombi yake kwa Mungu wake, na maneno ya waonaji walionena naye kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli, tazama, yameandikwa kati ya mambo ya wafalme wa Israeli.

19Sala yake pia, na jinsi Mungu alivyomtakabali, na dhambi yake yote, na kosa lake, na mahali alipopajenga mahali pa juu, na kupasimamishia Maashera na sanamu za kuchonga, kabla ya kujinyenyekeza; tazama, hayo yameandikwa katika Kumbukumbu ya Hozai.[#33:19 Maana yake ni ‘Waonaji’.]

20Basi Manase akalala na babaze, wakamzika nyumbani mwake; na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.

Kutawala kwa Amoni na kifo chake

21Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka miwili.

22Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kama alivyofanya Manase babaye; Amoni akazitolea dhabihu sanamu zote alizozifanya Manase babaye, akazitumikia.

23Wala hakujinyenyekeza mbele za BWANA, kama Manase babaye alivyojinyenyekeza; lakini huyo Amoni akaongeza makosa juu ya makosa.[#2 Tim 3:13]

24Wakamfanyia fitina watumishi wake, wakamwua katika nyumba yake mwenyewe.[#2 Fal 21:23,24; 2 Nya 24:25,26; 25:27,28; Zab 55:23]

25Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliomfanyia fitina mfalme Amoni; watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme badala yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya