2 Wamakabayo 10

2 Wamakabayo 10

Hekalu kutakaswa

1Huko nyuma Makabayo na wafuasi wake, wakiongozwa na BWANA, walilitwaa hekalu tena, na mji pia.

2Wakazibomoa madhabahu zilizojengwa na wageni sokoni, na kuviharibu viwanja vya miungu yao.

3Wakiisha kulitakasa hekalu walijenga madhabahu mpya ya kutolea dhabihu, wakapata moto kwa kugonganisha mawe, wakatoa dhabihu, ambazo hazikutolewa kwa muda wa miaka miwili. Wakafukiza uvumba na kuwasha taa na kuweka mikate ya wonyesho.

4Baada ya kufanya hayo walianguka kifudifudi wakamwomba BWANA wasipatwe tena na mambo mabaya kama hayo; bali, wakianguka tena katika dhambi, awarudi kwa kiasi, asiwatie tena katika mikono ya washenzi wakufuru.

5Ikatokea ya kuwa, siku ile hekalu lilipotiwa unajisi na wageni, siku ile ile lilitakaswa; yaani, siku ya ishirini na tano ya mwezi ule, ndio Kislevu.

6Waliiadhimisha kwa siku nane kwa mashangilio kama maadhimisho ya sikukuu ya vibanda, wakikumbuka ya kuwa, si zamani sana, wakati wa sikukuu ya vibanda walikuwa wakizungukazunguka milimani na pangoni kama wanyama.

7Ndiyo sababu walichukua fimbo zilizopambwa majani, na matawi, na majani ya mitende, wakapaza nyimbo za shukrani kwake Yeye aliyewafanikisha na kuwawezesha kupatakasa mahali pake mwenyewe.

8Wakaagiza pia, kwa shauri la watu wote, iwekwe sheria kwamba taifa lote la Wayahudi waziadhimishe siku hizo kila mwaka.

6. VITA VYA YUDA MAKABAYO NA MATAIFA JIRANI NA LISIA WAZIRI WA EUPATORI

Fedheha ya Tolemayo Makroni

9Basi, hizi ni habari za mwisho za Antioko aliyeitwa Epifani.

Kutawazwa kwa Antioko Eupatori

10Sasa tutaeleza yaliyotokea wakati wa Antioko Eupatori, mwana wa yule mwovu, tukitaja kwa ufupi maafa makuu ya vita vyake.[#1 Mak 6:17]

11Mtu huyu, alipourithi ufalme, alimweka Lisia kuwa waziri wake na jemadari mkuu wa Koele-Shamu na Foinike.

12Ikawa Tolemayo, aliyeitwa Makroni, alikuwa akionesha mfano mwema wa kuwatendea Wayahudi kwa haki – kwa sababu ya mambo mengi yasiyo haki waliyokuwa wametendwa – akijaribu kuchukuana nao kwa amani.

13Kwa sababu hiyo alishtakiwa na rafiki za mfalme mbele ya Eupatori; tena, kila upande alisikia watu wakimwita “msaliti” kwa sababu aliacha kisiwa cha Kipro, alichokabidhiwa na Filometo, na kumfuata Antioko Epifani. Basi kwa jinsi alivyofedheheka alikula sumu akajiua.

Shughuli za vita katika Idumaya

14Gorgia alipofanywa kiongozi wa nchi ile alijipatia jeshi la askari wageni wa mshahara akapigana na Wayahudi kila mara.

15Pamoja na hayo, Waidumaya, walioshika ngome kadha wa kadha imara sana, waliwasumbua Wayahudi, wakiongeza uadui kwa kuwapokea watu waliowakimbilia kutoka Yerusalemu.

16Lakini Makabayo na watu wake, wakiisha kuomba dua na kumsihi Mungu ajiweke upande wao, walizishambulia ngome za Waidumaya kwa nguvu, wakazitwaa.

17Walirudisha nyuma askari waliopigana ukutani, wakaua wote waliokutana nao, wakiangamiza watu wasiopungua elfu ishirini.

18Wengine, wasiopungua elfu tisa, waliikimbilia minara miwili, imara sana, iliyokuwa na vitu vyote viwezavyo kuhitajiwa wakati wa kuhusuriwa.

19Basi, Makabayo aliwaacha Simoni na Yusufu, pamoja na Zakayo na kikosi chake, watu wa kutosha kwa mazingio, naye mwenyewe alikwenda kule alikotakiwa zaidi.

20Lakini watu wengine wa Simoni, waliokuwa na choyo, walikubali kupewa rushwa na wale wa ndani ya minara, hata, wakiisha kupewa drakma elfu sabini, waliacha wengine watoke kwa siri.

21Habari hizo zilipomfikia Makabayo, aliwakusanya wakuu wa watu, akawashtaki ya kuwa wamewauza ndugu zao kwa fedha kwa kuwaweka adui zao huru kupigana nao.

22Akawaua wale wasaliti, akaishambulia minara akaitwaa.

23Katika kazi zote za vita alifaulu; na katika ngome hizi mbili watu waliowaua walikuwa zaidi ya elfu ishirini.

Yuda amshinda Timotheo

24Ndipo Timotheo, ambaye alishindwa kwanza na Wayahudi, alikusanya jeshi kubwa la askari wageni, na kikosi kikubwa kidogo cha askari wapanda farasi wa Asia. Akaja kana kwamba anataka kushambulia Uyahudi kwa nguvu.

25Alipokaribia, Makabayo na watu wake walijitia vumbi kichwani na kujivika gunia kiunoni,

26wakimwomba Mungu. Wakaanguka juu ya daraja mbele ya madhabahu, wakamsihi awafadhili, awe adui kwa adui zao na mtesi kwa watesi wao, kama sheria isemavyo waziwazi.

27Kisha wakaondoka katika kusali, wakatwaa silaha zao, wakatoka mjini wakaenda mbele, mwendo mrefu kidogo; hata walipofika karibu na adui walisimama.

28Kulipokucha asubuhi, yale majeshi mawili yalianza kupigana. Hawa wengine walikuwa na tumaini la kufanikiwa na kushinda kwa sababu pamoja na ujasiri wao wenyewe, walimtegemea BWANA waliyemkimbilia; hali wengine walisukumizwa vitani na ukakamavu wao tu.

29Vita vilipokuwa vikali zaidi, adui wakaona watu watano watukufu wakitoka mbinguni juu ya farasi wenye matandiko ya dhahabu na kutangulia mbele ya Wayahudi.

30Nao walimzunguka Makabayo na kumfunika kwa ngao zao na kumlinda asitiwe jeraha, na huku walikuwa wakiwatupia adui mishale na radi hata walipofushwa macho, wakaingia wasiwasi na fadhaa, wakakatwa vipande vipande.

31Wakauawa watu elfu ishirini na tano na mia tano, pamoja na wapanda farasi mia sita.

32Timotheo mwenyewe aliikimbilia ngome iitwayo Gaza, ngome imara sana chini ya amri ya Kaerea.

33Askari wa Makabayo wakaizingira ngome muda wa siku ishirini na nne kwa moyo wa furaha.

34Wale wa ndani, wakiitumainia nguvu ya ngome, waliwalaumu vibaya sana kwa matukano na makufuru.

35Lakini siku ya ishirini na tano alfajiri, vijana ishirini wa jeshi la Makabayo, wakitiwa uchungu sana kwa yale makufuru, waliushambulia ukuta kwa ujasiri, na katika ghadhabu yao walimpiga kwa upanga kila waliyemkuta.

36Wengine wakawafuata, wakiwazunguka adui kwa nyuma, wakaitia minara moto wakawateketeza wakufuru wangali hai. Wengine wakaivunja milango wakaingiza askari waliobaki. Hivyo waliutwaa mji.

37Wakamwua Timotheo, aliyekuwa amejificha katika tangi, pamoja na nduguye Kaerea, na Apolofani.

38Wakiisha fanya hayo yote, waliimba nyimbo za shukrani, wakimhimidi BWANA kwa fadhili zake nyingi kwa Waisraeli na kwa kuwapa ushindi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya