2 Wamakabayo 11

2 Wamakabayo 11

Lisia ahusuru Bethsuroni

1Muda kitambo tu baada ya hayo, Lisia, ndugu wa mfalme mtunzaji wake, na waziri wake, aliudhika sana kwa hayo yaliyotokea,

2alikusanya askari wapata elfu nane, pamoja na wapanda farasi wake wote, akawaendea Wayahudi.

3Nia yake ilikuwa kuufanya ule mji makao ya Wagiriki, na kutoza kodi ya hekalu kama ya mahali patakatifu pengine pa mataifa, na kuunadi ukuhani mkuu kila mwaka.

4Hakuijali nguvu ya Mwenyezi Mungu, bali alijivunia makumi elfu ya askari zake, na maelfu ya wapanda farasi wake, na ndovu zake themanini.

5Akaja Uyahudi, akakaribia Bethsuroni, ngome imara mwendo wa kama nusu maili kutoka Yerusalemu, akaihusuru.

6Basi, Makabayo na watu wake walipopata habari ya kuhusuriwa ile ngome, wao, pamoja na watu wote, waliomboleza na kulia, wakimsihi BWANA apeleke malaika mwema kumwokoa Israeli.

7Makabayo mwenyewe alikuwa wa kwanza wa kutwaa silaha, akawaita wengine wamfuate kwa ujasiri wawaokoe ndugu zao. Wakatoka pamoja naye kwa moyo mkuu.

8Hata kabla hawajaenda mbali na Yerusalemu, mpanda farasi alitokea mbele yao, amevikwa nguo nyeupe na kushika silaha za dhahabu.

9Nao wote kwa umoja walimhimidi BWANA mwenye rehema, wakajipa moyo.

10Wakaenda mbele kwa vikosi vyao, pamoja na msaidizi wao wa mbinguni, tayari sasa kupiga, si watu tu, ila wanyama wakali mno na kuta za chuma, kwa kuwa BWANA amewarehemu.

11Wakawarukia adui kama simba, wakaua askari elfu kumi na moja, na wapanda farasi elfu moja na mia sita, wakawakimbiza wengine wote.

12Katika wale waliookoka karibu wote walikuwa wametiwa jeraha na kunyang'anywa kila kitu; hata Lisia mwenyewe alijiokoa kwa kukimbia kwa aibu.

Amani kati ya Lisia na Wayahudi

13Huyu Lisia hakuwa mjinga. Alifikiri juu ya kushindwa kwake, akafahamu kwamba Waebrania hawashindiki kwa kuwa Mwenyezi Mungu yupo upande wao. Basi, alipeleka watu kupatana nao kwa masharti ya haki juu ya mambo yote,

14akiahidi hata kumshawishi mfalme awe rafiki yao.

15Makabayo akayakubali masharti yote ya Lisia, na hivyo alitenda kwa busara na kwa faida ya watu wake, maana maombi yote juu ya Wayahudi aliyoyaandika Makabayo na kumpelekea Lisia yalikubaliwa na mfalme.

16Barua iliyoandikwa na Lisia kwa Wayahudi ilikuwa namna hii: Lisia kwa jamii ya Wayahudi, salamu.

17Wajumbe wenu, Yohana na Absalomu, wameitoa taarifa iliyoandikwa chini na kutaka kujua nia yetu juu ya mambo yaliyomo.

18Basi, nimemwarifu mfalme mambo yote yampasayo kuyajua, naye amekubali yote aliyoyaweza.

19Kama ninyi sasa, kwa upande wenu, mtakaza nia yenu njema kwa serikali, nitajaribu tangu sasa kuitafuta faida yenu.

20Juu ya mambo haya moja moja nimewaagiza mawakili wenu na wangu washauriane nanyi.

21Kwa herini. Mwaka wa mia arubaini na nane, siku ya ishirini na nne ya mwezi Dioskuro.

22Barua ya mfalme ilisema hivi: Mfalme Antioko kwa nduguye Lisia, salamu.

23Kwa kuwa baba yetu amefariki akaenda kwa miungu, ni mapenzi yetu raia za ufalme wetu wastarehe bila wasiwasi na kushughulika na mambo yao wenyewe.

24Tumesikia ya kuwa Wayahudi hawalipendi shauri la baba yetu la kuwaongoza kwenye desturi za Kigiriki, bali huzipendelea mila zao wenyewe, wakiomba ruhusa kuzifuata desturi zao.

25Basi, ni mapenzi yetu taifa hilo pia likae bila wasiwasi, nasi tumekata shauri sasa kuwarudishia hekalu lao na kuwaruhusu waishi kwa kuzifuata desturi za wazee wao.

26Kwa hiyo ni afadhali upeleke watu kwa kuwapa yamini, ili wajue nia yetu na kujituliza moyo na kushughulika na mambo yao kwa furaha.

27Barua ya mfalme kwa taifa la Wayahudi ilisema hivi: Mfalme Antioko kwa baraza ya Wayahudi na kwa Wayahudi wengine salamu.

28Kama hamjambo ndivyo tuombavyo. Sisi huku hatujambo.

29Menelao ametuarifu ya kuwa mnataka kurudi kwenu na kushughulika na kazi zenu.

30Basi, wao warudio hata siku ya thelathini ya mwezi Zanthiko watapewa yamini yetu:

31wana ruhusa kutumia vyakula vyao wenyewe na kuzishika sheria zao kama zamani, wala hakuna atakayesumbuliwa kwa namna yoyote kwa ajili ya tendo alilolitenda kwa kutokujua.

32Nimemleta Menelao ayathibitishe hayo.

33Kwa herini. Mwaka mia moja arubaini na nane, siku ya kumi na tano ya Zanthiko.

34Warumi pia waliwaandikia barua kwa maneno haya: Kwinto Memio na Tito Manio, wajumbe wa Warumi kwa taifa la Wayahudi, salamu.

35Yale masharti yenu yaliyokubaliwa na Lisia, nduguye mfalme sisi pia tumeyakubali.

36Lakini juu ya yale aliyoyaona yamhusu mfalme, lete mtu kwetu mara moja, mkiisha kuwafikiria vema, ili tutangaze masharti ya kufaa. Tunakwenda Antiokia.

37Basi, lete wajumbe upesi tuijue nia yenu.

38Kwa heri. Mwaka mia moja arubaini na nane, siku ya kumi na tano Zanthiko.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya