2 Wamakabayo 5

2 Wamakabayo 5

Yasoni ajaribu kuchukua utawala

1Kama wakati huo Antioko alishambulia Misri mara ya pili.

2Ikatokea ya kuwa, kwa muda wa siku zilizokaribia arubaini, wapanda farasi walionekana angani, wakienda kwa nguvu. Mavazi yao yalifumwa kwa dhahabu; walichukua mikuki, wakapangwa safu safu tayari kwa vita.

3Kulikuwa na wapanda farasi wengine vikosi vikosi; na kushambuliana huku na huko; mtikiso wa ngao, mikuki kila upande, na panga wazi; kutupiana mishale, na kumetameta kwa mavazi ya dhahabu na deraya za kila namna.

4Watu wote waliomba maono hayo yabashiri heri.

5Kukatokea uvumi wa uongo kwamba Antioko amekufa. Basi, Yasoni alichukua watu wasiopungua elfu moja akaushambulia mji kwa ghafla. Askari walinzi waliowekwa juu ya ukuta wakashindwa na kurudishwa nyuma.

6Mwishowe, mji ulipokuwa karibu kukamatwa, Menelao aliikimbilia ngome. Yasoni aliua wenyeji wenzake bila huruma; hakufahamu ya kuwa ushindi juu ya jamaa ni ushindi tu; bali alifanya kana kwamba anateka adui, wala si watu wa nchi yake mwenyewe.

7Lakini hakuupata mji; mwisho wa uasi wake ulikuwa fedheha tu na kuikimbilia tena nchi ya Waamoni.

8Hatimaye alipatwa na mwisho mbaya; kufungwa na Areta, mkuu wa Waarabu; kukimbia mji kwa mji; kufukuzwa na watu wote; kuchukiwa kama mwasi wa sheria; kukirihiwa kama mwuaji wa nchi yake na raia wenzake; na kutupwa Misri.

9Yeye aliyekuwa amehamisha watu wengi kutoka nchi yao katika nchi ya kigeni, alikufa mwenyewe katika nchi ya kigeni alipokuwa akivuka bahari kwenda kwa Walakedemonia, akitumaini kukaribishwa nao kwa kuwa ni jamaa.

10Yeye aliyetupa wengi bila maziko hakuwa na mtu wa kumwombolezea, wala hakuwa na maziko hata, wala mahali pake katika kaburi la baba zake.

Antioko Epifani anateka hekalu nyara

11Basi, habari za mambo hayo zilipomfikia mfalme alidhani kama Uyahudi umefanya uasi. Akatoka Misri kwa hasira nyingi akaushambulia mji akautwaa.

12Akawaagiza askari zake wapige kwa upanga wote watakaowakuta bila kuonesha huruma, na kuwaua watu waliozikimbilia nyumba zao.

13Wakauawa vijana na wazee, na kuharibiwa kabisa wavulana, wanawake na watoto, wanawali na watoto wachanga.

14Katika zile siku tatu waliangamizwa watu elfu themanini, na katika hao elfu arubaini waliuawa katika mapigano ya kushikiliana.

Hekalu kutekwa

15Na watu waliouzwa utumwani hawakupungua hao waliouawa. Wala si hayo tu, ila alithubutu kuingia katika hekalu lililo takatifu kuliko yote duniani, akiongozwa na Menelao, yule aliyekuwa msaliti wa sheria na wa nchi yake.

16Akavishika vyombo vitakatifu kwa mikono yake najisi, na kuvinyang'anya kwa mikono michafu vitu vilivyotolewa na wafalme wengine kwa kuongeza utukufu na fahari ya mahali pale.

17Antioko akajivuna moyoni, asitambue ya kuwa ni dhambi zao waliokaa mjini zilizomtia BWANA Mwenyezi hasira ya kitambo hata akageuza macho yake mbali na mahali.

18Maana isingalikuwa wamefungwa kwa dhambi nyingi, mtu huyu, kama Heliodoro aliyetumwa na mfalme Seleuko kuikagua hazina, angalipigwa na kurudishwa nyuma mara alipothubutu kusogea mbele.

19Lakini BWANA hakulichagua taifa kwa ajili ya mahali, bali mahali kwa ajili ya taifa.

20Kwa hiyo, mahali paliishiriki misiba iliyolipata taifa, hata baadaye paliushiriki ufanisi wake; na mahali palipokataliwa katika ghadhabu ya Mwenyezi palirudishwa tena kwa utukufu mwingi Mfalme Mkuu aliporidhika.

Viongozi wa nchi

21Naye Antioko, akiisha kuchukua talanta elfu moja mia nane katika hekalu, alikwenda nazo Antiokia kwa haraka, na kwa jinsi moyo wake ulivyoinuka alijiona kama angeweza kuvukia nchi kavu kwa jahazi na bahari kwa miguu!

22Aliweka viongozi wa kuwatesa watu: Huko Yerusalemu Filipo, mtu wa Frigia, mwenye tabia ya kishenzi kuliko bwana wake;

23na huko Gerizimu, Androniko. Na pamoja na hao, Menelao aliyewaonea raia wenzake vibaya kupita wote. Tena, katika chuki yake kwa Wayahudi, raia zake,

24alimtuma Apolonio, jemadari wa Wamisia, pamoja na askari elfu ishirini na mbili, akiwaamuru wawaue watu wazima wote, na kuuza utumwani wanawake na vijana.

25Huyu alikuja Yerusalemu akajifanya mtu wa amani. Akangoja hata siku takatifu ya Sabato Wayahudi walipoacha kazi. Ndipo alipowaamuru watu wake wavae silaha zao na kujipanga.

26Wote waliokuja kutazama aliwaua; kisha akaingia mjini kwa haraka na askari zake, akaua watu wengi.

27Lakini Yuda, aitwaye Makabayo, pamoja na wenzake kama tisa, waliponyoka, wakaishi milimani kama waishivyo wanyama, wakiponea mboga za majani ili wasitiwe unajisi kama wengine.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya