2 Samweli 15

2 Samweli 15

Absalomu anyakua utawala

1Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.[#2 Sam 12:11; 1 Fal 1:5; Mit 11:2; 16:18]

2Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu yeyote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumishi wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.[#Mit 1:16]

3Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza.[#Mit 12:2]

4Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au kesi aje kwangu, nimpatie haki yake![#Amu 9:29]

5Tena ikawa hapo alipokaribia mtu yeyote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu.[#Zab 12:2]

6Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.[#Rum 16:18]

7Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme, Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea BWANA huko Hebroni.[#2 Sam 2:1]

8Maana mimi mtumishi wako niliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama BWANA akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia BWANA.[#1 Sam 16:2; Mwa 28:20; 1 Sam 1:11; Zab 56:12; 2 Sam 13:38; 14:23,32]

9Naye mfalme akamwambia, Nenda kwa amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni.

10Lakini Absalomu akatuma wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anatawala huko Hebroni.

11Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lolote.[#1 Sam 9:13; 16:3,5; Mwa 20:5; Mit 14:15; Mt 10:16; Rum 16:18,19]

12Absalomu alipokuwa akitoa dhabihu alituma Ahithofeli Mgiloni, Mshauri wake Daudi, aitwe kutoka mji wake, yaani, Gilo. Njama zao zikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu walizidi kuongezeka.[#Zab 41:9; 55:12; Mik 7:5,6; Yos 15:51; Zab 3:1; 43:2]

Daudi akimbia toka Yerusalemu

13Mjumbe akamfikia Daudi, akasema, Mioyo ya watu wa Israeli inashikamana na Absalomu.[#Amu 9:3]

14Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate kwa upesi, na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga.[#2 Sam 19:9]

15Hao watumishi wa mfalme wakamwambia mfalme, Angalia, sisi watumishi wako tu tayari kutenda lolote atakalolichagua bwana wetu mfalme.

16Basi mfalme akatoka na watu wa nyumbani mwake wote wakafuatana naye. Mfalme akaacha wanawake kumi, masuria, ili kuitunza nyumba.[#2 Sam 12:11; 16:21; 20:3]

17Mfalme akatoka, na watu wote wakamfuata; wakakaa kidogo katika Beth-merhaki.[#15:17 Kwa maana ya nyumba ya mwisho.]

18Watumishi wake wote wakapita karibu naye; na Wakerethi wote, na Wapelethi wote, na Wagiti wote, watu mia sita walioandamana naye kutoka Gathi, wakapita mbele ya mfalme.[#2 Sam 8:18]

19Ndipo mfalme akamwambia Itai, Mgiti, Mbona wewe unakwenda pamoja nasi? Rudi, ukakae na mfalme; maana wewe u mgeni, tena u mtu uliyefukuzwa mahali pako mwenyewe.[#2 Sam 18:2]

20Kwa kuwa umekuja jana tu kwa nini nikusumbue leo, na kukuzungusha huku na huko pamoja nasi nami hapa ninaenda niwezapo kwenda? Rudi wewe, ukawarudishe na ndugu zako; rehema na kweli ziwe pamoja nawe.[#1 Sam 23:13]

21Naye Itai akamjibu mfalme akasema, Kama aishivyo BWANA, na bwana wangu mfalme aishivyo, hakika yake kila mahali atakapokuwapo mfalme, bwana wangu, ikiwa ni kwa kufa au ikiwa ni kwa kuishi, ndipo atakapokuwapo na mtumishi wako.[#Rut 1:16; 1 Sam 20:3; 2 Fal 2:2-6; Mit 17:17]

22Basi Daudi akamwambia Itai, Haya, nenda ukavuke. Akavuka Itai, Mgiti na watu wake wote, na watoto wadogo wote waliokuwa pamoja naye.

23Na nchi yote ikalia kwa sauti kuu, nao watu wote wakavuka, mfalme mwenyewe naye akavuka kile kijito Kidroni, na hao watu wote wakavuka, wakielekea njia ya nyika.[#1 Fal 2:37; 2 Nya 30:14; Yn 18:1; 2 Sam 16:2; Mt 3:1-3]

24Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la Agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hadi watu wote walipokwisha kuutoka mji.[#Hes 4:15]

25Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa BWANA atanirudisha, na kunionesha tena sanduku hili, na maskani yake;[#Zab 43:3; 2 Sam 6:17]

26lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema.[#Hes 14:8; 2 Sam 22:20; 1 Fal 10:9; 2 Nya 9:8; Isa 62:4; 1 Sam 3:18]

27Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi, Ahimaasi, mwana wako, na Yonathani, mwana wa Abiathari.[#2 Sam 24:11; 1 Sam 9:9; #15:27 Au, Je! Wewe si mwonaji?]

28Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikia neno la kunipasha habari kutoka kwenu.

29Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko.

30Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akapanda huku akilia; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.[#Zek 14:4; Mt 21:1; Lk 19:20; Mdo 1:12; Est 6:12; Isa 20:2; Yer 14:3; Zab 126:6; Mt 5:4; Rum 12:15]

31Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee BWANA, nakusihi, uugeuze ushauri wa Ahithofeli uwe ubatili.[#Zab 3:1; 55:12; 2 Sam 16:23]

Hushai anakuwa Mpelelezi wa Daudi

32Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake likiwa limeraruliwa, tena akiwa na udongo kichwani mwake.[#2 Sam 1:2; 13:9]

33Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu;[#2 Sam 19:35]

34lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.

35Je! Hawako Sadoki na Abiathari, makuhani, pamoja nawe huko? Basi itakuwa, kila neno utakalolisikia katika jumba la mfalme, utawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani.

36Angalia, wanao huko pamoja nao wana wao wawili, Ahimaasi, mwana wa Sadoki, na Yonathani, mwana wa Abiathari; nanyi kwa mikono yao mtanitumia habari ya kila neno mtakalolisikia.

37Basi Hushai, rafiki wa Daudi, akaingia ndani ya mji; naye Absalomu akafika akaingia Yerusalemu.[#2 Sam 16:15,16; 1 Nya 27:33; Mit 17:17]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya