2 Samweli 2

2 Samweli 2

Daudi atiwa mafuta kuwa mfalme wa Yuda

1Ikawa baada ya hayo, Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Niupandie mji wowote wa Yuda? BWANA akamwambia, Haya! Panda. Daudi akasema, Niupandie mji upi? Akasema, Hebroni.[#Hes 27:21; Amu 1:1; 1 Sam 23:2-9; 30:7,8; 1 Fal 2:11]

2Basi Daudi akapanda aende huko, pamoja na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mkewe Nabali, wa Karmeli.[#1 Sam 25:42-43]

3Daudi naye akawapandisha watu wake waliokuwa pamoja naye, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; wakakaa katika miji ya Hebroni.[#1 Sam 27:2]

4Basi watu wa Yuda wakaenda, wakamtia Daudi mafuta huko, awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.[#1 Sam 31:11-13; 2 Sam 5:5]

Wakamwambia Daudi wakasema, Watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Sauli.

5Basi Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabesh-gileadi, na kuwaambia, Na mbarikiwe ninyi na BWANA, kwa kuwa mmemtendea bwana wenu fadhili hii, yaani Sauli, mkamzika.[#Zab 115:15]

6BWANA naye sasa awatendee ninyi fadhili na kweli; mimi nami nitawalipeni fadhili hiyo, kwa sababu mmetenda jambo hilo.[#2 Tim 1:16; Mt 5:44]

7Basi sasa, mikono yenu na itiwe nguvu, nanyi iweni mashujaa; maana Sauli, bwana wenu, amekufa, tena nyumba ya Yuda wamenitia mimi mafuta niwe mfalme wao.

Ishboshethi mfalme wa Israeli

8Basi Abneri, mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Sauli, alikuwa amemtwaa Ishboshethi, mwana wa Sauli, na kumvusha na kumpeleka Mahanaimu;[#1 Sam 14:50; 17:55; Mwa 32:2; 2 Sam 17:27]

9akamweka awe mfalme wa Gileadi, na Waasheri, na Yezreeli, na Efraimu, na Benyamini, na juu ya Israeli wote.

10(Huyo Ishboshethi, mwana wa Sauli, alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka miwili.) Lakini nyumba ya Yuda waliandamana na Daudi.[#2:10 Pia Ishbali ‘Kwa maana ya mtu wa aibu’.]

11Na wakati Daudi alipotawala Hebroni juu ya nyumba ya Yuda ulikuwa miaka saba na miezi sita.

Vita vya Gibeoni

12Basi Abneri, mwana wa Neri, na watumishi wa Ishboshethi, mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.[#Yos 9:3; 18:25; Isa 28:21]

13Huyo Yoabu naye, mwana wa Seruya, na watumishi wa Daudi, wakatoka, wakakutana nao karibu na ziwa la Gibeoni; wakaketi, hawa upande huu wa ziwa, na hawa upande huu wa ziwa.[#Yer 41:12]

14Abneri akamwambia Yoabu, Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya! Na waondoke.[#Mit 10:23; 13:10]

15Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na wawili wa watumishi wa Daudi.

16Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni.[#2:16 kwa maana ya mahali pa ncha za upanga]

17Vita vile vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli, mbele ya watumishi wa Daudi.[#1 Fal 20:11]

18Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu.[#1 Nya 2:16; 12:8; Zab 18:33; Wim 2:17; 8:14]

19Naye Asaheli akamfuatia Abneri; na katika kwenda kwake hakugeuka kwenda mkono wa kulia wala mkono wa kushoto katika kumfuatia Abneri.

20Basi Abneri akatazama nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi.

21Basi Abneri akamwambia, Geuka mkono wa kulia au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha kumfuata.[#1 Sam 17:42]

22Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi; kwa nini nikupige hadi chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu, ndugu yako?

23Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo, akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa, wakasimama.[#2 Sam 3:27; 4:6]

24Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo walipoufikia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni.[#Yos 9:3; 10:2]

25Nao wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya mlima.

26Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao?[#Ayu 18:2; 19:2; Zab 4:2; Mdo 7:26]

27Naye Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao, wasiwafuatie kila mtu ndugu yake.[#Mit 17:14; 20:18; Lk 14:31,32]

28Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena.

29Wakaenda Abneri na watu wake usiku ule wote kati ya ile Araba; wakavuka Yordani, wakapita kati ya Bithroni yote, wakaja Mahanaimu.[#Wim 2:17; Mwa 32:2; Yos 21:38; 2 Sam 17:24]

30Akarudi Yoabu naye kutoka kumfuatia Abneri; na alipokwisha kuwakusanya watu wote pamoja, wa hao watumishi wa Daudi walipungukiwa na watu kumi na tisa pamoja na Asaheli.

31Ila watumishi wa Daudi walikuwa wamewapiga watu wa Benyamini, na watu wa Abneri, hata wakafa watu mia tatu na sitini.

32Nao wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake, lililokuwako Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, wakapambazukiwa huko Hebroni.[#Mwa 47:29,30; 49:29; Amu 8:32; 2 Sam 17:23; 19:37]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya