2 Samweli 6

2 Samweli 6

Daudi aleta sanduku la Agano Yerusalemu

1Basi Daudi akakusanya tena wateule wote wa Israeli, watu elfu thelathini.

2Akaondoka Daudi akaenda pamoja na watu wote waliokuwa naye, mpaka Baala wa Yuda, ili kulipandisha kutoka huko sanduku la Mungu lililoitwa kwa jina, naam, jina la BWANA wa majeshi akaaye juu ya makerubi.[#Kut 25:22; 1 Nya 13:5; 1 Sam 4:4; Zab 80:1]

3Wakaliweka sanduku la Mungu juu ya gari jipya, wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu, iliyoko kilimani; nao Uza na Ahio wana wa Abinadabu wakaliendesha lile gari jipya.[#1 Sam 7:1-2; Hes 7:9]

4Wakalitoa katika nyumba ya Abinadabu iliyoko kilimani, pamoja na sanduku la BWANA; na huyo Ahio akatangulia mbele ya sanduku.

5Daudi na nyumba yote ya Israeli wakacheza mbele za BWANA kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa kayamba, na kwa matoazi.

6Hata walipofika kwenye uga wa Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walijikwaa.[#Hes 4:15]

7Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza; naye Mungu akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu.[#1 Sam 6:19]

8Daudi akaona uchungu kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.[#6:8 Kwa maana ya adhabu ya Uza.]

9Naye Daudi akamwogopa BWANA siku ile; akasema, Litanijiaje sanduku la BWANA?[#Hes 17:12,13; 1 Sam 5:10,11; Zab 119:120; Lk 5:8]

10Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la BWANA kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti.

11Sanduku la BWANA akalitia katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akambariki Obed-edomu, na nyumba yake yote.[#1 Nya 26:4-5; Mwa 30:27; 39:5; Mit 3:9,10; Isa 61:9]

12Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, BWANA ameibariki nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu. Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji wa Daudi, kwa shangwe.

13Hata ikawa, watu waliolichukua sanduku la BWANA walipokwisha kwenda hatua sita, akachinja fahali na ndama mnono.[#Hes 4:15; Yos 3:3; 1 Nya 15:2,15; 1 Fal 8:5; 2 Nya 5:6]

14Daudi akacheza mbele za BWANA kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.[#Kut 15:20; Amu 11:34; 21:21; Zab 30:11; 1 Sam 2:18; 1 Nya 15:27]

15Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la BWANA kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.

16Ikawa, sanduku la BWANA lilipoingia mji wa Daudi, Mikali binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za BWANA; akamdharau moyoni mwake.

17Wakaliingiza sanduku la BWANA, na kuliweka mahali pake, katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za BWANA.[#1 Nya 15:1; Zab 132:8; 1 Fal 8:5]

18Kisha Daudi alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani akawabariki watu kwa jina la BWANA wa majeshi.

19Akawagawia watu wote, mkutano wote wa Israeli, wanaume kwa wanawake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu. Basi watu wote wakaenda zao, kila mtu nyumbani kwake.[#1 Nya 16:43]

20Ndipo Daudi akarudi ili awabariki watu wa nyumbani mwake. Na Mikali, binti Sauli, akatoka nje aende kumlaki Daudi, naye akasema, Mfalme wa Israeli alikuwa mtukufu leo namna gani, akijifunua mwili wake mbele ya vijakazi vya watumishi wake, mfano wa watu baradhuli mmojawapo, ajifunuavyo mwili wake mbele ya watu, asipokuwa na haya![#Mhu 7:16; Isa 59:15; 1 Sam 19:24; Amu 9:4]

21Daudi akamwambia Mikali, Ilikuwa mbele za BWANA, aliyenichagua mimi juu ya baba yako, na juu ya nyumba yake, ili kuniweka niwe mkuu juu ya watu wa BWANA, juu ya Israeli; kwa hiyo mimi nitacheza mbele za BWANA.[#1 Sam 13:14; 15:28]

22Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa.

23Basi Mikali, binti Sauli, hakuwa na mtoto hata siku ya kufa kwake.[#1 Sam 15:35; Isa 22:14]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya