2 Samweli 9

2 Samweli 9

Daudi amhurumia Mefiboshethi

1Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani?[#1 Sam 20:15-17; 18:3; Mit 27:10]

2Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumishi wako ndiye.[#2 Sam 16:1; 19:17]

3Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu yeyote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu.[#2 Sam 4:4; Kum 10:15; 1 Sam 20:14; Mt 5:44,45; Lk 6:36; Tit 3:3,4]

4Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.[#2 Sam 17:27]

5Basi mfalme Daudi akatuma watu, na kumwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari.

6Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumishi wako!

7Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, babu yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima.[#Mwa 43:18,23; 50:21; 1 Sam 12:19-24; Yer 52:33]

8Akasujudu, akasema, Mimi mtumishi wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?[#1 Sam 24:14; 2 Sam 16:9]

9Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mjukuu wa bwana wako.[#2 Sam 16:4; 19:29; Isa 32:8]

10Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumishi wako; nawe utamletea mjukuu wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu siku zote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini.[#2 Sam 19:17]

11Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumishi wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kuhusu Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme.[#2 Sam 16:1-4; 19:24-30; Mit 12:17]

12Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi.[#1 Nya 8:34]

13Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula siku zote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.[#2 Sam 19:33,36; 2 Fal 25:29; Yer 52:33,34]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya