The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Moabu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu aliichoma moto mifupa ya mfalme wa Edomu hata ikawa chokaa; Sef 2:8-11; 2 Fal 3:27[#Isa 15:1—16:14; 25:10-12; Yer 48:1-47; Eze 25:8-11]
2lakini nitatuma moto juu ya Moabu, nao utayateketeza majumba ya Keriothi; na Moabu atakufa pamoja na mshindo, na kelele, na sauti ya tarumbeta;[#Yer 48:41]
3nami nitamkatilia mbali mwamuzi atoke kati yake, nami nitawaua wakuu wake pamoja naye, asema BWANA.[#Hes 24:17; Yer 48:7]
4Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA; wala hawakuzishika amri zake; na maneno yao ya uongo yamewakosesha, ambayo baba zao waliyafuata;[#Law 26:14; 2 Sam 12:9,10; 2 Nya 36:14-17; Neh 1:7; Isa 5:24; 28:15; Eze 20:13,16; Dan 9:11; Yer 16:19]
5lakini nitatuma moto juu ya Yuda, nao utayateketeza majumba ya Yerusalemu. Hukumu kwa Israeli.[#Hos 8:14]
6Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu;[#Isa 29:21; Amo 5:11,12]
7nao hukanyaga vichwa vya maskini katika mavumbi ya nchi na kuwasukuma walioteseka kutoka kwa njia yao; na mtu na baba yake wanamwendea mwanamke mmoja, na kulitia unajisi jina langu takatifu;[#Isa 10:2; Eze 22:11; Law 20:3; Eze 36:20; Rum 2:24]
8nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha.[#Kut 22:26; 1 Kor 10:21]
9Lakini nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini niliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini.[#Hes 21:24; Kum 3:8-11]
10Pia niliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arubaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori.
11Nami nikawainua watu miongoni mwa wana wenu wawe manabii, na katika vijana wenu wawe Wanadhiri; je! Sivyo hivyo, enyi wana wa Israeli? Asema BWANA.[#Amu 13:5; Hes 6:1-8]
12Lakini mliwapa Wanadhiri mvinyo wanywe; mkawaamuru manabii, mkisema, Msifanye unabii.[#Isa 30:10; Mdo 4:18]
13Tazameni, nitawalemea ninyi,
Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda.
14Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio;
Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake;
Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake;
15Wala apindaye upinde hatasimama;
Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka;
Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake;
16Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa
Atakimbia uchi siku ile, asema BWANA.