Mhubiri 7

Mhubiri 7

Ukweli wa maisha

1Heri sifa njema kuliko manukato ya thamani;[#Mit 22:1; Flp 1:23; Ufu 14:13]

Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.

2Heri kuiendea nyumba ya matanga,[#Mt 5:4]

Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.

3Huzuni ni afadhali kuliko kicheko,[#2 Kor 7:10]

Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.

4Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.

5Heri kusikia laumu ya wenye hekima,

Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;

6Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria,

Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu.

Hayo nayo ni ubatili.

7Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima,[#Kut 23:8]

Na rushwa huuharibu ufahamu.

8Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake,[#Mit 14:29]

Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.

9Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako,[#Yak 1:19; Mit 16:32]

Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.

10Usiseme, Kwa nini siku za kale zilikuwa ni bora kuliko siku hizi?

Maana si kwa hekima unauliza hili.

11Hekima ni njema kama urithi;

Naam, nayo ni bora kwao walionalo jua.

12Kwa maana ulinzi wa hekima ni kama ulinzi wa fedha na ubora wa maarifa ni kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.

13Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?[#Isa 14:27]

14Siku ya kufanikiwa ufurahi,

Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lolote litakalofuata baada yake.

Mafumbo ya maisha

15Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.[#Mhu 8:14]

16Usiwe na haki kupita kiasi;[#Mit 25:16; Flp 3:6; Rum 12:3]

Wala usijiongezee hekima mno;

Kwa nini kujiangamiza mwenyewe?

17Usiwe mwovu kupita kiasi;[#Ayu 15:32]

Wala usiwe mpumbavu;

Kwa nini ufe kabla ya wakati wako?

18Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.

19Hekima ni nguvu zake mwenye hekima,

Zaidi ya wakuu kumi waliomo mjini.

20Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, atendaye mema pasipo kutenda dhambi.[#1 Fal 8:46; 2 Nya 6:36; Mit 20:9; Rum 3:23; Gal 3:22; 1 Yoh 1:8]

21Tena, usitie moyoni mwako maneno yote wasemayo watu; usije ukamsikia mtumishi wako mwenyewe akikutukana.

22Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine.

23Mambo hayo yote mimi nimeyahakikisha katika hekima. Nilisema, Mimi nitakuwa na hekima, lakini imefarakana nami.

24Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?[#Kum 30:11-14; Ayu 11:12; Zab 36:6; Isa 55:8,9; Rum 11:33; 1 Tim 6:16]

25Nikageuka, na moyo wangu ulikazwa katika kujua na kupeleleza, na kuitafuta hekima, na maana ya mambo yaliyoko; ili nifahamu ya kuwa uovu ni upumbavu, na upumbavu ni wazimu.

26Nami nimeona lililo na uchungu kupita mauti; yaani, mwanamke ambaye moyo wake ni mitego na tanzi, na mikono yake ni kama vifungo; yeye ampendezaye Mungu atamponyoka, bali mwenye dhambi atanaswa na yeye.

27Tazama, asema Mhubiri, mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha hili na hili, ili kuitafuta jumla;

28ambayo bado nafsi yangu ningali nikiitafuta, nisiione; mwanamume mmoja katika elfu nimemwona; bali mwanamke mmoja miongoni mwa wote mimi sikumwona.

29Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamepanga mipango mingi.[#Mwa 1:27]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya