Ezekieli 2

Ezekieli 2

Maono ya gombo

1Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.[#Dan 10:11]

2Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.[#Hes 11:25; Amu 13:25; Neh 9:30; Eze 3:24; Yoe 2:28,29]

3Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wameasi juu yangu, naam, hata hivi leo.[#Yer 3:25]

4Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi.[#Eze 3:7]

5Nao, iwe watasikia au hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.[#Eze 3:11; 33:33]

6Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma inakuzunguka, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.[#Mt 10:28; Ebr 11:27; 1 Pet 3:14; Eze 3:26,27]

7Nawe utawaambia maneno yangu, iwe watasikia au hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana.[#Yer 1:7,17; Mt 28:20]

8Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.[#Ufu 10:9]

9Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la kitabu lilikuwa ndani yake.[#Yer 1:9; Eze 3:1; Ufu 5:1]

10Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole![#Isa 3:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya