The chat will start when you send the first message.
1Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu.
2Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake.[#Isa 46:11; 45:1]
3Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake.
4Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye.[#Isa 44:7; 43:10; 48:12; Mdo 15:18; Ufu 1:11,17]
5Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja.
6Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Jipe moyo.
7Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.
8Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Abrahamu, rafiki yangu;[#Mwa 18:19; Neh 9:7; 2 Nya 20:7; Yak 2:23]
9wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa;
10usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kulia wa haki yangu.[#Kum 31:6; Rum 8:31]
11Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia.[#Kut 23:22; Zek 12:3]
12Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.
13Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kulia, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.
14Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli.[#Ayu 19:25]
15Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.[#Mik 4:13; 2 Kor 10:4,5]
16Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.[#Yer 51:2]
17Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.
18Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.[#Isa 35:6,7; Zab 107:35]
19Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja;
20ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.[#Ayu 12:9]
21Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.
22Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuoneshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye.
23Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja.[#Kum 18:22; Yer 10:5]
24Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo.
25Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawakanyaga watawala kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi apondaye udongo.[#Ezr 1:2]
26Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu.
27Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema.
28Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno.[#Isa 63:5; Dan 2:10]
29Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo mtupu.